1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya mpakani Azerbaijan, Armenia yauwa wanajeshi 49

Mohammed Khelef
13 Septemba 2022

Urusi imezitolea wito Azerbaijan na Armenia kukomesha uhasama na kutekeleza makubaliano iliyoyasimamia ya kusitisha mapigano, wakati huu mapigano ya mpakani kati ya nchi hizo mbili yakipoteza wanajeshi 49 wa Azerbaijan.

https://p.dw.com/p/4Glqj
Archivbild I Konflikt Berg-Karabach
Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Kwenye ripoti yake, wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi ilisema imefanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano kunakoanza saa 3:00  asubuhi kwa majira ya Moscow, na kwamba inatarajia pande zote mbili zitayaheshimu. 

Urusi, ambayo yenyewe inaendesha mashambulizi dhidi ya Ukraine, ilisema ina wasiwasi sana na kuibuka upya kwa mapigano kati ya mahasimu hao wawili. 

Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan, amesema mapema hii leo kwenye hotuba yake bungeni kwamba ingawa mapigano makali yamepunguwa, lakini bado kuna mapigano ya hapa na pale kwenye baadhi ya maeneo. 

Vyombo vya habari nchini Azerbaijan vimeripoti kwamba mapigano yalizuka tena robo saa tu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano. 

Kila upande unaulaumu mwengine kwa kuzuka upya kwa mapigano haya. Kwa upande wake, Armenia ilisema kwamba miji kadhaa ya mpakani ilishambuliwa kwa makombora alfajiri ya leo, ndipo nayo ikajibu kile ilichokiita uchokozi wa kiwango cha juu wa Azerbaijan. 

Waziri Mkuu Pashinyan aliituhumu Azerbaijan kwa mashambulizi hayo akisema yametokana na ukweli kwamba haitaki kufikia muafaka juu ya mkoa wa Nagorno-Karabakh, jimbo lililo ndani ya Azerbaijan lakini linalokaliwa na watu wenye asili ya Armenia.

Mawaziri wa ulinzi wa Urusi na Armenia walizungumza kwa njia ya simu asubuhi ya leo na kukubaliana kuchukuwa hatua za kurejesha hali ya kawaida. 

Urusi, ambayo ina kituo chake cha kijeshi ndani ya Armenia, ndiye mpatanishi mkuu kwenye eneo hilo, licha ya kuwa mshirika wa Armenia kupitia Jumuiya ya Usalama wa Pamoja. 

Azerbaijan, Uturuki zailaumu Armenia

Archivbild I Konflikt Berg-Karabach
Wanajeshi mitaani katika mkoa wa Nagorno-Kabarakh.Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Kwa upande wake, Azerbaijan, ambayo imekuwa ikiituhumu Armeniakwa kufanya shughuli za kijasusi na kuongeza idadi ya silaha kwenye mpaka wake, imesema maeneo yake ya kijeshi yalishambuliwa na Armenia. 

Uturuki, ambayo ni mwanachana wa Muungano wa Kijeshi wa NATO,  inaunga mkono Azerbaijan, ambaye wakaazi wake wengi ni Waislamu wanaojinasibisha na Uturuki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mesut Cavusoglu, alizungumza na mwenzake wa Azerbaijan, Jehyun Bayramov na kuitolea wito Armenia "kukomesha uchokozi" wake.

Kwenye taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, alisema hakuna suluhisho la kijeshi kwenye mzozo wa mataifa hayo mawili ya Caucas, na badala yake yanapaswa kumaliza tafauti zao mezani.

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, pia alimtolea wito Waziri Mkuu wa Armenia, Pashinyan kuzuwia makabiliano zaidi ya mpakani.