1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yamepamba moto Idlib na kuwatimua malaki ya watu

Oumilkheir Hamidou
16 Januari 2020

Dazeni kadhaa ya wanamgambo na raia wameuliwa katika mkoa wa Idlib nchini Syria kufuatia opereshini za vikosi vya serikali kutaka kuingia katika ngome hiyo ya mwisho ya waasi.

https://p.dw.com/p/3WJXZ
Syrien Angriffe in der Provinz Idlib
Picha: picture-alliance/AA/I. Idilbi

Wimbi la hivi karibuni kabisa la matumizi ya nguvu lililofuatia hujuma za angani zilizoangamiza maisha ya watu 18 jumatano, limevunja makubaliano ya kuweka chini silaha yaliyotangazwa na Urusi na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki-makubaliano ambayo kimsingi hayajawahi kutekelezwa."Mapigano yameripuka usiku wa manani kusini mwa mji wa Maaret al-Numan, huku mizinga ikifyetuliwa licha ya makubaliano ya kuweka chini silaha kati ya Urusi na Uturuki" amesema Rami Abdel Rahman, mkuu wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam lenye makao yake nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mapigano yamelenga maeneo ya kusini mwa mji wa Maaret al-Numan- kitovu cha mashambulio ya vikosi ya serikali ya Syria.

Wapiganaji wasiopungua 22 wanaoipinga serikali wameuwawa, wengi wao ni wanachama wa Hayat Tahrir al Sham, kundi linalowajumuisha wapiganaji waliokuwa wakishirikiana zamani na mtandao wa kigaidi wa al Qaida nchini Syria.

Wakimbizi wa Syria mjini Idlib
Wakimbizi wa Syria mjini IdlibPicha: picture-alliance/AA/E. Turkoglu

 Baridi kali inayochanganyika na mvua inatishia maisha pia ya wanaokimbia mapigano

Wanajeshi 17 wa serikali na wanamgambo wanaoshirikiana nao, nao pia wameuwawa katika mapigano hayo-shirikia hilo linalosimamia masuala ya haki za binaadam limesema.

Ram Abdel Rahman ameongeza kusema vikosi vya serikali viko umbali wa kilomita saba tu karibu na mji wa Maaret al-Numan, mji ambao ni mojawapo ya ngome za upinzani dhidi ya utawala wa rais Bashar al Assad.

Katika mji wa idlib, raia 18 wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika hujuma za ndege za kivita za Urusi na Syria. Maripota wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, wameshuhudia hali ya vurugu iliyofuatia hujuma hizo zilizovunja majumba kadhaa .

Mustafa anaemiliki duka katika mtaa huo amefanikiwa kuyanusuru maisha yake kabla hujuma hizo kutokea alipoondoka kwenda kutafuta vipuri mtaa mwengine. Ameliambia shirika la habari la AFP aliporejea duka lake limeteketezwa na watumishi wake wanne wamefunikwa na vifusi. Hajasema kama wamenusurika au la.

Mji wa Idlib unahujumiwa mtindo mmoja tangu wiki kadhaa zilizopita na kusababisha maelfu kuyapa kisogo maskani yao. Shirika la Umoja wa Mataifa linalosiimamia huduma za kiutu OCHA linasema tangu decemba mosi iliyopita watu laki tatu wameyapa kisogo maskani yao, wengi wao kutoka kusini mwa Idlib na kuelekea katika maeneo ya kaskazini. Baridi kali inayofuatiwa na mvua inayatia hatarini pia maisha ya maelfu ya watu.