1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaishutumu Iran kuvuruga amani Mashariki ya Kati

Isaac Gamba
30 Aprili 2018

Waziri mpya wa mamabo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameishutumu Iran kwa shughuli zake katika kanda ya Mashariki ya Kati, ambazo amesema zinaivurga kanda hiyo.

https://p.dw.com/p/2wuNQ
Saudi-Arabien PK Außenminister Adel al-Jubeir und US-Außenminister Mike Pompeo
Picha: Reuters/F. Al Nasser

Katika ziara  yake ya kwanza nje ya nchi  saa kadhaa baada ya kuapishwa Mike Pompeo alikutana na viongozi wa Saudi Arabia  na Israel nchi mbili ambazo zinamahusiano maalumu ya kimkakati na Marekani na ambazo pia zina adui wa pamoja Iran  huku waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu akisisitiza kuwa makubaliano ya nyukilia na Iran lazima yabadilishwe au yavunjwe ingawa mataifa mengi makubwa duniani  yanayaona makubaliano hayo kuwa ndiyo njia inayoweza kuizuia Iran isiwe na silaha za nyukilia.

Akizungumza pembezoni mwa waziri mkuu wa Israel baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa masaa mawili mjini Telaviv  waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo  alisema nia ya Iran kutaka kutawala siasa za  Mashariki ya Kati bado ipo palepale na akasema hawatapuuza vitendo hivyo vya Iran kama ilivyokuwa kwa utawala uliotangulia.

Amesisitiza kuwa rais Donald Trump atajiondoa kwenye makubaliano ya nyukilia na Iran  iwapo hayatafanyiwa mabadiliko huku waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu akiongeza kuwa kiu ya Iran kutaka kutengeneza bomu la nyukilia lazima izuiwe ikiwa ni pamoja na uchokozi wake.  Hata hivyo akizungumza kwa simu na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron  rais wa Iran Hassan Rouhani amesema makubaliano ya nyukilia na Iran hayawezi kujadiliwa upya.

 Netanyahu ampongeza Trump

Israel PK Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: REUTERS

Ama kwa upande mwingine waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu amempongeza tena rais Donald Trump kwa uamuzi wake wa kutangaza kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel  na kuwa wanasubiri kwa hamu kubwa kushuhudia utekelezaji wa hatua hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari  Mike Pompeo ameishutumu Iran kwa kuvuruga amani ya Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kuunga mkono utawala wa kikatili wa  rais wa Syria Bashar al- Assad pamoja na waasi wakishia nchini Yemen.  Amesema  Iran inayaunga mkono makundi ya kigaidi na pia kutoa silaha kwa waasi wa houthi nchini Yemen  huku pia akiishutumu kwa kufanya kampeni za mashambulizi ya kimatandao.

Viongozi wa nchi zote mbili Saudi Arabia na Israel  walionekana kufurahishwa  na hatua ya Mike Pompeo kama ilivyo kuwa kwa Trump kuzijumuisha nchi hizo katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu ashike rasmi wadhifa huo.

Awali Mike  Pompeo alikutana na mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdul-Aziz mjini  Riyadhi  baada ya hafla ya chakula cha jioni na mwana mfalme Mohamed bin Salman.

Akiwa Jordan mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amekutana na mwenzake wa Jordan Ayman al -Safadi katika mji mkuu wa nchi hiyo ambapo viongozi hao mbali na kujadili mahusiano kati ya nchi hizo mbili, ametoa mwito pia kwa Palestina na Israel kurudi katika meza ya mazungumzo ya amani na kuongeza kuwa Marekani inaamini katika suluhisho la mataifa mawili huku pia  ajenda ya kukutana na viongozi wa Palestina ikionekana kutokuwepo katika ziara yake hiyo ya  Mashariki ya Kati  mnamo wakati Palestina ikiishutumu Marekani kwa uamuzi wake wa kutangaza kuhamisha ubalozi wake kutoka mjini Tel Aviv na kuupeleka Jerusalem.

Hata hivyo aligusia vurugu ambazo zimekuwa zikitokea katika ukanda wa Gaza na kusema kuwa Marekani inaamini Israel ina haki pia ya kujilinda dhidi ya vurugu hizo. Ziara hiyo ya Mike Pompeo mashariki ya Kati inatarajiwa kukamilika leo.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/DPAE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga