1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapanga kuwajibika zaidi Mali

19 Februari 2013

Juhudid za kuisaidia Mali zimeshika kasi huku Marekani ikiahidi kuwajibika moja kwa moja,uchaguzi huru utakapoitishwa

https://p.dw.com/p/17gvn
Wakimbizi wa Mali karibu na mpaka na MauritaniaPicha: DW/J.M. Oumar

Marekani inafikiria kuwajibika zaidi kijeshi nchini Mali ambako wanajeshi wa Ufaransa wanapambana na wafuasi wa itikadi kali. Katika wakati ambapo Ufaransa imeanzisha rasmi ushirikiano wake na Mali, Ujerumani imeidhinisha mpango wa kutumwa hadi wanajeshi 330 nchini Mali na Umoja wa Ulaya unapanga kuitisha mkutano wa wafadhili mwezi Mei mwaka huu.

Uamuzi wa Marekani unafungamanishwa na sharti la kuitishwa uchaguzi mkuu nchini Mali. Hadi wakati huu Marekani imekuwa ikiisaidia Ufaransa kwa kuipatia maelezo na ndege za kijeshi chapa C-17.

Lakini Marekani haikuweza kushirikiana moja kwa moja na jeshi la Mali kwa sababu ya kukosekana serikali iliyochaguliwa kwa njia za kidemokrasia, kukamata nafasi ya wale walioingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya Machi mwaka jana, hayo ni kwa mujibu wa Seneta Chris Coons, ambaye ni mwenyekiti wa tume ya baraza la Seneti linaloshughulikia sera za nje, tawi la Afrika.

Akiwa ziarani mjini Bamako Seneta Coons amesema "watu wanaweza kutegemea msaada wa ziada na wa moja kwa moja wa Marekani katika eneo hilo, mara baada ya uchaguzi.

Bwana Coons yuko ziarani mjini Bamako akiongoza ujumbe wa bunge la Marekani, Congress, wakiwemo wafuasi wa vyama vyote viwili, Democratic na Republican, kwa lengo la kukutana na rais wa mpito, Dioncounda Traoré, pamoja na maafisa wa kijeshi wa Ufaransa na Afrika.

Rais Traoré aliwahi kuelezea uwezekano wa kuitisha uchaguzi hadi ifikapo Julai 31 mwaka huu lakini baadhi waliitaja tarehe hiyo kuwa ni mapema mno kutokana na matatizo yanayoikaba Mali ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu, mfarakano jeshini na malaki ya watu walioyapa kisogo maskani yao.

Mkutano wa wafadhili kutishwa haraka

)
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano wa Umoja wa Ulaya kuhusu MaliPicha: JOHN THYS/AFP/Getty Images

Ufaransa imetangaza kuanza upya ushirikiano wake na Mali, uliositishwa baada ya mapinduzi ya Machi 22 mwaka jana. Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ufaransa, Pascal Canfin, ametangaza habari hizo katika mji wa kati wa Mopti alikoitembelea hospitali moja inayofadhiliwa na Ufaransa na Ubeligiji. Hii leo waziri Canfin amepangiwa kukutana na rais wa mpito, Dioncounda Traoré.

Mjini Berlin baraza la mawaziri la serikali kuu ya Ujerumani limeidhinisha mpango wa kutumwa hadi wanajeshi 330 kusaidia vikosi vya kiafrika nchini Mali. Wanajeshi wa Ujerumani ni sehemu ya tume ya wanajeshi wa Umoja wa Ulaya watakaowapatia mafunzo wanajeshi wa Mali.

Naye mwenyekiti wa halmshauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, amesema wanapanga kuitisha duru mpya ya mkutano wa wafadahili wa Mali katikati ya mwezi May mwaka huu kwa lengo kama alivyosema la "kuunga mkono utaratibu wa kuimarisha utulivu, umoja, maendeleo na amani nchini Mali." Kauli hiyo ameitoa baada ya mazungumzo yake pamoja na waziri mkuu Django Cissoko jana mjini Brussels.

Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya uliamua kutoa Euro milioni 250 za msaada wa maendeleo kwa Mali, fedha ambazo zilizuiliwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Machi mwaka jana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo