1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka Iran iwekewe upya vikwazo

21 Agosti 2020

Marekani imeufahamisha rasmi Umoja wa Mataifa kuhusiana na matakwa yake ya vikwazo kwa Iran virudishwe. Hayo yamepelekea upinzani kutoka kwa Urusi na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3hHIn
USA | Außenminister Mike Pompeo
Picha: AFP/M. Segar

Marafiki wa Marekani kutoka Ulaya pia wameonyesha upinzani, wakiitaja hatua hiyo kuwa kinyume cha sheria.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amemfahamisha rais wa Baraza hilo la Usalama akisema Iran imekiuka pakubwa mkataba wa mwaka 2015 wa nyuklia jambo linalotoa nafasi ya kuwekwa vikwazo hivyo kwa mara nyengine tena.

"Marekani haitokubali kamwe mfadhili mkubwa wa ugaidi duniani kununua na kuuza ndege, magari ya kivita, makombora na silaha zengine bila udhibiti. Vikwazo hivi vya Umoja wa Mataifa vitaendeleza marufuku ya kununua silaha," alisema Pompeo.

Urusi kupitia naibu balozi wake katika Umoja wa Mataifa imeikosoa Marekani

Marufuku hayo ya Iran kununua silaha yalikuwa yanakamilika Oktoba 18. Yanaizuia Iran pia kufanya majaribio ya makombora na urutubishaji wa urani.

UN-Sicherheitsrat New York 2016 | Waffenembargo Libyen
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiwa kikaoniPicha: Imago Images/Xinhua

Mara baada ya hatua hiyo ya Marekani naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyansky  ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akiishambulia Marekani kwa kutoheshimu sheria na kufanya kile inachotaka bila kumshauri yeyote.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani nchi ambazo ni wanachama wa mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015, wameungana na Urusi kuipinga hatua hiyo ya Marekani licha ya kuwa nchi hizo za Ulaya ni marafiki wa Marekani, jambo linaloashiria kibarua cha Marekani katika suala hilo.

Trump aliiondoa Marekani kwenye mkataba wa nyuklia na Iran mwaka 2018

Iran yenyewe imeikosoa Marekani kwa hatua hiyo iliyochukua. Majid Ravanchi ni Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa.

USA | UN- Sicherheitsrat | Iranischer Botschafter Majid Takht Ravanchi
Balozi wa Iran Umoja wa Mataifa Majid Takht RavanchiPicha: Getty Images/S. Platt

"Kulingana na hoja za kisheia, Marekani si mshiriki wa mkataba wa nyuklia na haina haki ya kukitumia kipengele cha kurudisha tena vikwazo na tafsiri yake ya azimio 2231 haiwezi uubadilisha ukweli," alisema Majid.

Rais Donald Trump mwaka 2018 aliiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba huo wa mwaka 2015 ambao unajumuisha nchi sita zenye nguvu duniani pamoja na Iran. Marekani inashikilia kwamba chini ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bado ina haki ya kukirudisha kipengee cha kuiwekea tena Iran vikwazo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Usimamizi wa Niashati ya Nyuklia limeripoti kuhusiana na Iran kwenda kinyume na makubaliano hayo ingawa Iran yenyewe inasema hiyo inatokana na Marekani kukiuka makubaliano hayo kwa kujiondoa na kisha kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kimataifa.