1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo akutana na Mfalme wa Saudia kwa mazungumzo

Amina Mjahid Sekione Kitojo
24 Juni 2019

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amezungumzia mvutano wa kikanda unaoendelea na Mfalme Salman wa Saudi Arabia kama sehemu ya shinikizo la kidiplomasia la kuunda muungano wa kidunia dhidi ya Iran.

https://p.dw.com/p/3L0Bn
Mike Pompeo in Saudi Arabien
Picha: Getty Images/J. Martin

Mfalme Salman na Mike Pompeo walitathmini uhusiano wa kimkakati na maendeleo ya hivi karibuni ya eneo hilo na yale ya kimataifa. Pompeo alisema Marekani inatafuta muungano wa kidunia dhidi ya Iran aliyoiita dola kubwa linalofadhili ugaidi.

Mazungumzo yao yalituwama juu ya mashambulizi dhidi ya meli za mafuta katika Guba ya kiarabu baada ya mashambulizi ya hivi karibu dhidi ya matanki hayo ambapo Marekani iliilaumu Iran kwa shambulio hilo.

USA 2019 Trafficking in Persons report | Mike Pompeo, Außenminister in Washington
Waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo Picha: Reuters/Y. Gripas

"Tulikuwa na mkutano wa kufana na Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud leo kujadili wasiwasi wa kikanda uliopo na umuhimu wa kukuza usalama wa baharini katika eneo la Hormuz” aliandika hayo WaziriPompeo katika mtandao wake wa kijamii wa twitter muda mfupi tu baada ya  mkutano wake na Mfalme Salman.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani pia alikutana na mwanamfalme aliye na ushawishi Mohammed bin Salman katika bandari ya Magharibi mjini Jeddah kabla ya kuondoka kuelekea Umoja wa Falme za kiarabu.

Marekani na Saudi Arabia ziko pamoja kutokomeza uchokozi wa Iran pamoja na Ugaidi

Wizara ya habari ya Saudia imesema kukutana kwa viongozi hao wawili ni ishara ya wazi kuwa mataifa hayo mawili yamesimama pamoja kusitisha shughuli za uchokozi za Iran na kudhibiti ugaidi. Hata hivyo Iran imesema vikosi vyake haivitajizuwiya kudungua ndege zaidi za Marekani kutoka katika anga yake.

Ziara hii ya Pompeo imekuja saa chache baada ya waasi wa Houthi wanaofungamanishwa na Iran kushambulia uwanja wa ndege wa Abha Kusini Magharibi mwa Saudi Arabia kwa kutumia ndege isiokuwa na rubani na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine 21 wakijeruhiwa.

US-Drohne Global Hawk
Ndege ya Marekani iliyodunguliwa katika eneo la HormuzPicha: picture-alliance/US Air Force/Zumapress

Wiki iliyopitaIraniliidungua ndege isiyokuwa na Rubani ya Marekani na kwa kujibu hilo taifa hilo likatangaza vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Wakati huo huo maafisa wa Ulaya wameonekana kutozungumzia suala la Marekani kutaka kuunda muungano wa kidunia dhidi ya Iran wakisema ajenda yao kuu ni kuhakikisha mvutano kati ya mataifa hayo mawili hauendelei huku wakiwa na matumaini ya kuyaokoa makubaliano ya Iran juu ya kudhibiti mpango wake wa nyuklia.

Ufaransa, Ujerumani, Uingereza Urusi na China wanabakia kuwa ndani ya mkataba huo ambao Marekani ulijiondoa mwaka uliopita.

Vyanzo: Reuters/ap/afp