1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aviation- EU-safety

Sekione Kitojo20 Aprili 2010

Halmashauri ya umoja wa Ulaya imesema kuwa mawaziri wa usafiri wa umoja huo wamekubaliana kulegeza masharti yaliyowekwa dhidi ya safari za anga kutokana na wingu la majivu.

https://p.dw.com/p/N0vl
Wingu la jivu la volcano likitoka kutoka katika volcano iliyolipuka nchini Iceland.Picha: picture-alliance/dpa

Halmashauri ya Ulaya imesema kuwa mawaziri wa usafiri wa umoja wa Ulaya wamekubaliana kulegeza , masharti yaliyowekwa kwa ajili ya safari za anga kutokana na wingu la majivu yanayotoka kutoka katika volcano iliyoripuka nchini Iceland.

Kuanzia leo asubuhi, tutashuhudia ndege nyingi za abiria zikianza kusafiri, kamishna wa usafiri wa umoja wa Ulaya Siim Kallas amewaambia waandishi habari baada ya mkutano uliochukua muda mrefu kupitia njia ya mawasiliano ya video baina ya mawaziri wa usafirishaji wa umoja wa Ulaya.

Haiwezekani kuwa na muafaka utakaoleta hatari katika usalama wa wasafiri. Maamuzi yote ni lazima yawe katika msingi wa ushahidi wa kisayansi pamoja na tathmini ya wataalamu, ameongeza kamishna huyo, wakati mashirika ya ndege katika bara la Ulaya pamoja na abiria wakiendelea na siku ya tano ya kufutwa kwa safari za anga.

Tangazo hilo limetolewa kwa wakati mmoja mjini Brussels na Madrid, ambako waziri wa usafirishaji wa Hispania Jose Blanco , ambaye nchi yake inashikilia kwa sasa urais wa umoja wa Ulaya , amesema kuwa safari za anga zitaruhusiwa katika maeneo ambayo wingi wa majivu umepungua kuanzia saa mbili asubuhi saa za Ulaya ya kati.

Uamuzi wa uwezekano wa kuruhusiwa kwa safari za anga umeratibiwa kwa ushirikiano wa mawaziri wa mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya. Eneo la tatu ambalo halikuathirika na majivu hayo maafisa wameona hakuna kikwazo.

Mamlaka ya safari za anga nchini Ireland imesema katika taarifa kuwa katika maeneo ambayo hayana wingu mkubwa wa majivu , mataifa yanapaswa kuziruhusu safari za ndege, zikiungwa mkono na data zilizopo, ikiwa ni pamoja na ushauri kutoka kwa jumuiya ya wanasayansi.

Kwa upande wake , Uingereza, Ufaransa na mataifa mengine yametangaza yataanza kuondoa masharti hayo ya kupiga marufuku safari za anga kuanzia leo.

Wasafiri wameanza kusafiri tena na wasafiri ambao wameshindwa kusafiri kwa muda mrefu wamewasili hatimaye katika viwanja viwili vikuu vya mjini Paris leo Jumanne baada ya siku tano za kupigwa marufuku safari hizo kutokana na wingu la majivu ya volcano.

Uwanja wa ndege wa mjini Brussels umefunguliwa tena kwa safari chache leo Jumanne. Lakini viwanja vyote vya Denmark vitaendelea kufungwa hadi takriban saa mbili kesho Jumatano kutokana na wingu hilo la majivu ya volcano.

Wakati huo huo volcano iliyosababisha mtafaruku katika usafiri barani Ulaya inaendelea kuripuka na kutoa moto zaidi kuliko moshi wenye majivu na kutoa wingu jepesi la majivu hayo imeeleza ofisi ya utabiri wa hali ya hewa ya Iceland.

Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE /AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman