1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoinukia kiuchumi yadai upunguzaji mkubwa wa gesi za carbon.

Kitojo, Sekione8 Julai 2008

Mataifa matano makubwa yanayoinukia kiuchumi leo yamejitayarisha kuchukua msimamo mgumu dhidi ya utoaji gesi zinazoharibu mazingira.

https://p.dw.com/p/EYkv
Viongozi wa kundi la mataifa tajiri ya G8 wakipanda miti kuashiria mapambano dhidi ya ongezeko la ujoto duniani.Picha: AP


►◄




Mataifa matano makubwa yanayoinukia kiuchumi leo yamejitayarisha kuchukua msimamo mgumu dhidi ya utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira pamoja na usalama wa uhaba wa chakula, kabla ya mazungumzo yao kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na mataifa tajiri yenye viwanda ya kundi ya G8.



Katika taarifa yao , mataifa hayo matano yanayoimarika kiuchumi yameyataka mataifa ya G8 kubeba majukumu yao katika mabadiliko ya hali ya hewa kwa kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira kwa asilimia 80- 95 chini ya kiwango cha utoaji wa gesi hizo cha mwaka 1990 ifikapo mwaka 2050.

Mexico, Brazil, China, India na Afrika kusini pia zimeyataka mataifa yote yaliyoendelea kuchukua jukumu la upunguzaji kwa kiasi kikubwa cha utoaji wa gesi hizo katika msingi wa lengo la kipindi cha kati cha asilimia 25-40 chini ya kiwango cha mwaka 1990 ifikapo 2020.

Majadiliano ya upunguzaji wa utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira yanapaswa kutilia maanani majukumu ya kihistoria pamoja na uwezo kama njia bora ya haki, mataifa hayo matano yamesema katika tamko la pamoja.

Pia mataifa hayo yamesema kuwa wanaitaka jumuiya ya kimataifa , hususan mataifa yaliyoendelea , kuhimiza mifumo endelevu ya matumizi pamoja na mitindo ya maisha inayokubaliana na upunguzaji wa mahitaji.

Mataifa hayo matano yametoa msimamo wao wakati wa mkutano kabla ya kujiunga na majadiliano na mataifa ya G8 siku ya Jumatano, ikiwa ni siku ya mwisho ya mkutano huo wa mataifa tajiri unaofanyika katika kisiwa kilichoko kaskazini mwa Japan cha Hokaido.

Hapo mapema viongozi wa G8 walisema kuwa watafanyakazi pamoja na karibu mataifa 200 katika mazungumzo ya umoja wa mataifa ya mabadiliko ya hali ya hewa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza kuwa taarifa hiyo ya pamoja na kundi la mataifa ya G8 ni zingatio muhimu kuliko taarifa iliyotolewa katika mkutano wa mwaka jana.

Lakini waziri wa mazingira wa Afrika kusini amesema kuwa lengo la mataifa ya G8 ni kauli mbiu tupu, wakati mataifa hayo matano yamesema kuwa mataifa yaliyoendelea yanapaswa kuonyesha njia kwa kuwa viongozi ili kufanikisha hatua ya upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira.Wakati huo huo afisa mwandamizi wa umoja wa mataifa amesema kuwa taarifa ya pamoja ya kundi la mataifa ya G8 kuhusu upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira, ina mambo muhimu yenye manufaa lakini kutokuwa na malengo ya muda mfupi yenye tarakimu maalum ni tatizo kubwa.

Wakati huo huo viongozi wa kundi hilo la mataifa tajiri, G8 watatangaza hatua mpya dhidi ya Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na hatua za kifedha, kuhusiana na uchaguzi uliofanyika nchini humo ambao unapingwa vikali, wameeleza maafisa wa Japan.