1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya Khashoggi: Uturuki yawashtaki Wasaudi 20

25 Machi 2020

Uturuki imewashtaki raia wa Saudi Arabia wanaotuhumiwa kumuua mwandishi habari Jamal Khashoggi, akiwemo aliyekuwa naibu mkuu wa kitengo cha ujasusi, mshauri wa familia hiyo ya kifalme pamoja na washukiwa wengine 18.

https://p.dw.com/p/3a1uv
Ermordeter Saudischer Journalist Jamal Khashoggi
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Kupitia taarifa, ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Istanbul imesema imekamilisha uchunguzi wa mauaji ya mwandishi huyo wa habari aliyeuawa kinyama katika Ubalozi wa Saudia mjini Istanbul mnamo mwaka 2018.

Mauaji hayo yalilaaniwa vikali kote duniani na hivyo kulipaka tope jina la mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia Arabia Mohammed bin Salman.

Baadhi ya serikali za magharibi kikiwemo pia kitengo cha ujasusi cha Marekani CIA, kilimnyooshea kidole cha lawama Mohammed bin Salman wakimtuhumu kuwa aliagiza mauaji ya mwandishi huyo, tuhuma ambazo Saudia zimekanusha.

Symbolbild | Polizei in der Türkei
Askari polisi wa Uturuki akilinda karibu na ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, ambako Kashoggi aliingia kwa mara ya mwisho kabla ya kutoweka, Oktoba 2, 2018.Picha: Getty Images/O. Orsal

Hata hivyo, washukiwa wote wa mauaji hayo tayari wameondoka Uturuki na Saudi Arabia imekataa wito wa Uturuki wa kuwarudisha nchini humo ili wahukumiwe.

Badala yake Saudia inasisitiza kuwa mahakama zake zina uwezo wa kuendelea na kesi hiyo. Tayari watu 11 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi wamepandishwa kizimbani nchini Saudia Arabia.

Kupitia taarifa, ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Istanbul inayoongozwa na Irfan Fidan amesema kuwa Ahmed Al Asiri na Saud al Qahtani walikuwa na nia mbaya iliyolenga kushawishi mauaji ya Mwandishi huyo wa Habari ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Ufalme wa Saudia.

Ofisi hiyo vile vile imesema kuwa inawatuhumu watu wengine 18 kwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi akiwemo raia mmoja wa Marekani na mwandishi katika gazeti la Washington Post na inapendekeza kifungo cha maisha gerezani kwa 18 hao.

Saudi Arabien | Prinz Mohammed bin Salman
Mrithi wa kiti cha Ufalme nchini Saudi Arabia Mohammed bin Salman amenyooshewa kidole cha lawama kuhusu mauaji ya Khashoggi.Picha: picture-alliance/abaca/Balkis Press

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mashtaka dhidi ya washukiwa hao yalitokana na uchunguzi wa rekodi zao za simu, safari zao za kuingia na kutoka Uturuki, uwepo wao katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, taarifa za mashahidi pamoja na uchunguzi wa kompyuta na simu ya Khashoggi.

Khashoggi ambaye alikuwa akiishi Marekani, alikwenda katika Ubalozi wa Saudia mjini Istanbul mnamo Oktoba 2 mwaka 2018 kwa ajili ya kuchukua nyaraka ambazo zingemuwezesha kufunga ndoa na mchumba wake raia wa Uturuki. Hata hivyo, baada ya kuingia ndani ya Ubalozi huo hakutoka tena na hadi leo mwili wake haujapatikana.

Timu ya watu 15 kutoka Saudia ambao wanawajibika moja kwa moja kwa bin Salman walisafiri hadi Uturuki kukutana na Khashoggi ndani ya Ubalozi huo.

Maafisa wa Uturuki wanadai kuwa Khashoggi aliuawa ndani ya Ubalozi huo na kisha mwili wake ukakatwa vipande vipande.

Haya yanajiri baada ya mahakama ya Saudia mnamo Disemba kuwahukumu kifo watu watano na wengine watatu kupewa kifungo cha gerezani kwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi lakini mwendesha mashtaka wa Saudia alisema hakuna ushahidi wowote wa kuwahusisha Qahtani au Asiri na mauaji hayo.