1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha na afya wa G20 wakutana mjini Roma

Sylvia Mwehozi
29 Oktoba 2021

Mawaziri wa fedha na afya kutoka kundi la nchi zilizoendelea kiuchumi duniani za G20 wamesema watachukua hatua za kuhakikisha kwamba asilimia 70 ya watu duniani wanapatiwa chanjo ya Covid-19 kufikia katikati ya 2022.

https://p.dw.com/p/42MFr
Italien | G20 Gipfel in Rom
Picha: Pavel Bednyakov/Sputnik/dpa/picture alliance

Mawaziri hao waliokutana mjini Roma kabla ya kuanza mkutano wa kilele wa viongozi wa G20 mwishoni mwa juma hili, wameshindwa kukubaliana juu ya mfumo tofauti wa ufadhili uliopendekezwa na Marekani na Indonesia, lakini wamesema kwamba kikosi kazi kilichoundwa kitaangalia njia za kuhamasisha ufadhili utakaoboresha utayari wa kukabiliana na kuzuia majanga.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na mawaziri hao imesema kuwa "katika kusaidia kusukuma malengo ya dunia ya utoaji chanjo kwa angalau asilimia 40 ya idadi ya watu katika nchi zote kufikia mwishoni mwa mwaka 2021 na asilimia 70 kufikia katikati ya mwaka 2022, tutachukua hatua za kuboresha usambazaji chanjo na bidhaa muhimu za matibabu katika nchi zinazoendelea".

Aidha mawaziri hao wameunda kikosi cha pamoja cha masuala ya fedha na afya kitakachowezesha mazungumzo na ushirikiano wa kimataifa katika masuala yanayohusiana na kuzuia majanga, utayari na dharura za kiafya. Wanasema kikosi hicho kimeundwa kwasababu janga la Covid-19 limetoa changamoto katika uwezo wa ulimwengu kuratibu mapambano.

Wameahidi kuunga mkono juhudi za pamoja katika kutoa upatikanaji chanjo salama, nafuu, zenye ubora na ufanisi hususan katika nchi za kipato cha kati na chini.

Italien | G20 Gipfel in Rom | Protest
Wanaharakati nje ya mkutano wa G20Picha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kwamba ulimwengu unakimbilia katika janga la mabadiliko ya tabia nchi na kusema viongozi wa G20 wanapaswa kuchukua hatua zaidi katika kuyasaidia mataifa maskini. Akizungumza kuelekea mkutano wa kilele wa G20, Guterres amewaeleza waandishi wa habari kwamba "kuna kiwango cha hatari ya kukosa imani" baina ya mataifa na akaongeza kwamba ana matumaini mkutano huo wa siku mbili utalijadili hilo.

Pia ametoa wito kwa mataifa tajiri kufanya vyema kwenye ahadi ya muda mrefu ya kutoa dola bilioni 100 kwa mwaka kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na kitisho kinachoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kiongozi huyo ameyataka mataifa ya G20 kutoa ufadhili zaidi kwa nchi maskini, kupitia msamaha wa madeni na kuimarisha upatikanaji wa chanjo za Covid-19. Wito kama huo pia umetolewa na mashirika ya kiutu ambayo yanataka chanjo ya Covid-19 kupatikana kwa usawa, ulinzi zaidi wa mazingira na misaada zaidi kwa nchi maskini.