1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa G20 waikosoa uvamizi wa Urusi, Ukraine

Lilian Mtono
22 Februari 2024

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa mataifa ya Magharibi yaliyopo kwenye kundi la Mataifa tajiri na yanayoinukia kiuchumi G20 wameishambulia Urusi kwa kuivamia Ukraine katika mkutano wao unaofanyika nchini Brazil.

https://p.dw.com/p/4cjng
Rio de Janeiro, Brazil | Mwaziri wa mambo ya Nje wa mataifa ya G20
Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka mataifa ya G20Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron amesema kwenye kikao cha ndani kwamba Urusi inatakiwa kuwajibika kwa uvamizi huo, hayo ikiwa ni kulingana taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Australia, Canada, Ujerumani, Italia, Ufaransa na Norway pia walitoa maoni kama hayo katika siku ya kwanza ya mkutano huo wa siku mbili.

Soma pia:Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G20 wakutana Brazil

Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Espen Barth Eide(ESPEN BART AIDA) aliwaambia waandishi wa habari kwamba mwenzao wa Urusi Sergei Lavrov alimjibu Cameron kwa utulivu kwa orodha ya hoja kinzani kuhusiana na kile kinachoendelea nchini Ukraine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock kwa upande wake alitoa wito kwa kundi hilo kushinikiza kuhusu suluhu katika vita hivyo na kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati.