1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu hatma ya Mali yakwama

25 Agosti 2020

Mazungumzo kati ya wawakilishi wa mataifa ya Afrika Magharibi na viongozi wa jeshi la Mali yameshindwa kufikia makubaliano ya jinsi ya kurejesha utawala wa kiraia nchini humo baada ya mapinduzi ya wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/3hSKb
Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern
Mazungumzo kati ya viongozi wa jeshi na ujumbe wa ECOWAS.Picha: Reuters/M. Keita

Mkwamo katika suala nyeti la kuirejesha Mali chini ya utawala wa kiraia umeibuka baada ya majenerali wa jeshi kukataa pendekezo hilo na kutaka kupewa miaka mitatu ya kipindi cha mpito kitakachoongozwa na mwanajeshi.

Msemaji wa kundi la wanajeshi waliongooza mapinduzi Kanali Ismael Wague amesema licha ya majadiliano yanayoendelea mpango wa mwisho wa kipindi cha mpito nchini Mali utaamuliwa na makamanda wa jeshi baada ya masahuriano mapana na makundi mengine ya kiraia.

Msimamo huo wa baraza la kijeshi wa kuitisha uchaguzi baada ya miaka mitatu ulitolewa kwa mara ya kwanza siku ya Jumapili lakini tangu wakati huo umekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa raia wa Mali na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS.

ECOWAS -- Jumuiya ya mataifa 15 -- ilituma ujumbe wa ngazi ya juu mjini Bamako siku ya Jumamosi kuhimiza matakwa yake ya kurejea kwa utawala wa kiraia nchini Mali.

ECOWAS: Serikali ya Mali itakundwa na wao wenyewe 

Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern | Goodluck Jonathan
Mkuu wa ujumbe wa ECOWAS (mwenye kofia) Goodluck JonathanPicha: Reuters/M. Kalapo

Mkuu wa Ujumbe wa  ECOWAS ambaye pia ni rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amesema wamefanikiwa kupata makubaliano katika baadhi ya masuala muhimu lakini wamepeana muda wa kuyatafakari mengine ambayo hawakufia mwafaka.

Zaidi kuhusu msimamo wa ECOWAS kuelekea hatma ya utawala nchini Mali, Jonathan amesema "ECOWAS hatutokuja na kuwawekea serikali watu wa Mali, iwe serikali ya kuchauliwa au serikali ya kuteueliwa ya kipindi cha mpito ni lazamia iamuliwe na watu wa Mali."

Hayo yanajiri wakati duru zimearifu rais aliyepinduliwa Ibrahim Boubacar Keita, ambaye ECOWAS ilishinikiza kurejeshwa madarakani amearifu kuwa hana nia ya kuendelea tena kuongoza nchi hiyo.

Keita amekaririwa akisema kuwa alijiuzulu kwa hiyari na sasa anataka kuona taifa hilo linapata serikali ya mpito itakayorejesha utawala wa kidemokrasia.

Ahadi bila vitendo? 

Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern
Picha: Reuters/M. Keita

Kundi la wanajeshi lililompindua Keita Agosti 18 liliahidi siku moja baada ya mapinduzi kuwa litaunda kipindi cha mpito kitakachoongozwa na raia na kuitisha uchaguzi mkuu katika muda mfupi unaokuja.

Viongozi wakuu wa ECOWAS wanatarajiwa kuwa na mkutano wa pamoja siku ya Jumatano kuamua jinsi ya kushughulikia mzozo wa Mali, wakitiliia maana jinsi mapinduzi ya mwisho nchini humo ya mwaka 2012 yalivyoitikisa kanda hiyo na kuchochea kuibuika kwa uasi wa makundi ya itikadi kali.

ECOWAS tayari imetishia kuiwekea vikwazo Mali iwapo ufumbuzi hautapatikana kuhusu nani ataongoza nchi hiyo wakati wa kipindi cha mpito na lini hasa uchaguzi mkuu utaitishwa kurejesha utawala wa kiraia.