1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbeki ana kibarua kigumu Cote d'Ivoire

Oumilkher Hamidou6 Desemba 2010

Mgogoro wa kisiasa nchini Cote d Ívoire unaendelea na sasa Rais Laurent Gbagbo na mpinzani wake Alassane Ouattara - kila mmoja ametangaza baraza lake la mawaziri.

https://p.dw.com/p/QQrF
Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara
Laurent Gbagbo na Alassane OuattaraPicha: AP/DW

Imebidi mpatanishi wa Umoja wa Afrika aingilie kati kwa mara nyingine nchini humo Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Bwana Thabo Mbeki, ambae si mara ya kwanza kuwa mpatanishi katika mzozo wa Cote d'Ivoire, hakupokewa kwa moyo mkunjufu na wanasiasa wa nchi hio.

Inaelekea hakuna anaetaka kuregeza msimamo wake, baina ya pande mbili zinazohasimiana; Waziri mkuu wa zamani Alassane Ouattara ambae amepata ushindi katika uchaguzi wa Rais, na Rais aliemaliza mda wake Laurent Gbagbo.

Mazungumzo ya Bwana Mbeki na wanasiasa hao hayajafikia chochote. Raia wa kwanza wameanza kuikimbia nchi yao, wakielekea hasa mpaka na Liberia wakihofia kutokea vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki (kushoto) akijibu maswali ya waandishi wa habari akiwa na kiongozi wa upinzani, Alassane Ouatarra. (Picha ya AP/Thibault Camus)
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki (kushoto) akijibu maswali ya waandishi wa habari akiwa na kiongozi wa upinzani, Alassane Ouatarra. (Picha ya AP/Thibault Camus)Picha: AP

Tangu miaka kadhaa hakujakuwepo Rais aliechaguliwa kidemokrasia nchini Cote d'Ivoire. Hali inayojiri wakati huu si dalili nzuri kwa nchi hio.

Ilitarajiwa kua hatimae, baada ya mda mrefu wa shida zilizoambatana na matatizo ya kiuchumi, mafanikio ya uchaguzi wa November yangerejesha matumaini ya hali bora ya kiuchumi na kisiasa, ya taifa hilo muhimu kabisa katika eneo la magharibi mwa bara la Afrika.

Kulikuwepo matumaini kwamba hatimae serikali halali itaiwezesha Cote d'Ivoire kuwa taifa lenye mafanikio kama ilivyokua awali; nchi iliyotengamana kiuchumi, yenye kuwa na mali ghafi, mfumo bora wa elimu na ustawi wa jamii.

Cote d'Ivoire ilitarajiwa kurejea katika hali yake ya zamani, nchi iliyoongoza kiuchumi eneo zima la Afrika ya magharibi.

Hayo ndio yaliyokua matumaini ya Jumuia ya kimataifa, ambayo tangu miaka saba, imegharamia kwa mamiliyoni ya dola za marekani, tume ya Umoja wa mataifa katika nchi hiyo. Hayo ndio yaliyokua pia matumaini ya nchi jirani, ambazo zinahitaji usalama wa nchi hio, kwa kua baadhi yake hutumia bandari ya Abidjan, mji mkuu wa kiuchumi wa Cote d'Ivoire. Na hayo ndio yaliyokua pia matarajio ya wafanyabiashara wa nchi hio, ambao kwa mda mrefu wamekua wakikumbwa na matatizo chungu nzima.

Cote d'Ivoire iliwahi kuwa taifa lenye nguvu. Hadi miaka ya themanini, baadhi ya wazazi nchini Ufaransa, waliwapeleka watoto wao kusomea katika vyuo vikuu vya nchi hio, kwa kua Cote d'Ivoire ilikua na viwango vya juu kabisa vya elimu; na taifa lenye usalama. Wengine walisema Abidjan ni Manhtan ya Afrika ya magharibi. Eneo la kaskazini lenye kua na madini, mashamba ya kakao na mafanikio ya kibiashara kutokana na bandari ya Abidjan, yalilifanya taifa la Cote d'Ivoire na raia wake kuwa na mafanikio makubwa. Yote hayo hakuna kilichosalia.

Uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka wa 2000. Na tangu jaribio la mapinduzi ya kijeshi la mwaka wa 2002, nchi imegawayika. Eneo la kaskazini mwa nchi hio linadhibitiwa na waasi wa "Forces Nouvelles", wakati ambako serikali inatawala sehemu ya kusini mwa nchi. Hali ni kua kaskazini wala kusini, hakuna usalama. Gari zinasimamishwa barabarani na abiria wanayang'nywa pesa. Hakuna usalama wa kutosha, kusafirisha bidhaa kutoka nchi jirani.

Uchumi wa Cote d'Ivoire umeanguka kwa kiwango ambacho ni vigumu kulinganisha na hali iliyotokea katika nchi nyingine yeyote ile barani Afrika.

Ni dhahiri kua waathirika wa kwanza ni raia wa Cote d'Ivoire wenyewe; ambao wengi wao ni vijana. Miliyoni nane hawana ajira. Vijana. Jungu linaloweza kulipuka kufuatia mzozo uliopo. Hawa ndio wanaweza kuchochea machafuko. Na hatari zaidi ni wale ambao wanaounga mkono viongozi hawa wawili wanaohasimiana. kwa upande mmoja Bwana Alassane Ouattara, ambae jumuia ya kimataifa inamuunga mkono na kusema yeye ndie kapata ushindi katika uchaguzi wa Rais, anaungwa mkono na waasi wa "Forces Nouvelles". Na kwa upande mwingine Rais aliemaliza mda wake Laurent Gbabo anaungwa mkono na wanamgambo "Jeunes Patriotes" pamoja na jeshi.

Pande zote mbili ziko tayari kwa matumizi ya nguvu. Na pande zote mbili ziliwahi kuonyesha zilivyotayari kutumia nguvu; hata kabla ya uchaguzi kufanyika.

Kwamba Cote d'Ivoire inaweza kuutatua mzozo ulioko yenyewe na kuelekea njia ya amani; hakuna anaeamini. Hakuna nia ya kisiasa ya kumaliza mzozo uliopo.

Nchini Cote d'Ivoire, kumesainiwa idadi kubwa ya makubaliano kuliko hata idadi ya makubaliano iliyowahi kuwepo baada ya vita vya pili vya dunia, amesema mwenyekiti wa Halmashauri ya biashara ya nchi hio; Bwana Jean-Loui Billon.

Hata hivyo kila upande umekua ukitumia vyombo vyake vya habari kupaka matope upande mwingine na kuchochea chuki dhidi yake. Bwana Ouattara na Bwana Gbagbo, wote wawili wanachukuliwa kua "wakongwe" wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire. Wanafahamiana na wamekua wakikabiliana tangu miaka ya tisini. Hata hivyo wote wawili hawaamini demokratia, badala yake wafisadi; na kila mmoja anayapigania maslahi yake.

Kwa kua wanasiasa hawawajibiki, Cote d'Ivoire iko hatarini kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Na hii ni hatari kubwa kwa eneo lote la Afrika ya magharibi. Nchi hio ni nguzo ya usalama na utengamano katika eneo la Afrika ya magharibi, linalotumiwa hasa wakati huu kwa biashara haramu kuelekea Ulaya. Ikiwa Cote d'Ivoire itaingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, hali hii itaziathiri pia Liberia na Sierra Leonne ambazo bado zina majeraha ya macafuko ya kikabila mnamo miaka michache iliyopita. Na hali hii itaziathiri pia nchi jirani za eneo la Sahel; Mali na Burkinafaso.

Usalama wa eneo zima utakua mashakani. Ndio maana Umoja wa Afrika na Jumuia ya kimataifa kwa ujumla zinatakiwa kuzidisha juhudi zake za kuleta amani mnamo siku zijazo.

Mwandishi:Ute Schaeffer (Afrika-Nahost)/ Jean Francois Gisimba

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman