1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Hatua zilizoko sasa hazitoshi kudhibiti COVID-19

Sylvia Mwehozi
29 Machi 2021

Kansela Angela Merkel ameyashinikiza majimbo 16 ya Ujerumani, kuongeza juhudi za kudhibiti ongezeko la maambukizi ya COVID-19, na kugusia uwezekano wa kuanzisha marufuku ya kutotoka nje ili kudhibiti wimbi la tatu. 

https://p.dw.com/p/3rJPF
Bundeskanzlerin Angela Merkel zu Gast bei Anne Will
Picha: Wolfgang Borrs/NDR/dpa/picture alliance

Merkelameelezea kutoridhishwa kwake na baadhi ya majimbo yaliyoamua  kutosimamisha shughuli za kiuchumi zilizokuwa zimeanza kurejea taratibu, hata wakati idadi ya maambukizi kwa wakaazi 100,000 ndani ya kipindi cha siku saba ikipindukia 100 hatua ambayo yeye na wakuu wa majimbo walikubaliana mapema mwezi huu. Maambukizi ya COVID-19 yameongezeka haraka katika wiki za hivi karibuni, yakichangiwa na aina mpya ya virusi.

"Sasa inabidi tuchukue hatua zinazofaa kwa umakini sana. Baadhi ya majimbo wanafanya hivyo, wengine hawafanyi hivyo na ikiwa ndivyo katika siku zijazo basi nitazingatia hilo, hilo ni jukumu langu. Tunawezaje kuchukua mwelekeo wa pamoja? Bado sijafanya uamuzi lakini sheria zinatubana kuzuia maambukizi jambo ambalo hivi sasa halifanyiki."

Awali mkuu wa utumishi katika serikali ya Merkel Helge Braun alionya Jumapili  kuwa nchi iko katika hatari zaidi ya janga hilo na kuzidisha hofu kwamba wimbi la tatu linaweza kusababisha aina mpya ya virusi.

Mchakato wa utoaji chanjo Ujerumani umekuwa wa kusuasusa tangu mwanzo ukitatizwa na changamoto ya usambazaji. Hadi kufikia Jumapili (28.03.20219 ni asilimia 10.3 ya idadi jumla ya watu ambao tayari wamepatiwa dozi ya kwanza, ikiwa ni viwango vya chini kulinganisha na nchi zingine kama Israel, Marekani na Uingereza.

Bundeskanzlerin Angela Merkel zu Gast bei Anne Will
Kansela Merkel katika mahojiano na kituo cha ARDPicha: Wolfgang Borrs/NDR/dpa/picture alliance

Kansela huyo ameongeza kuwa ikiwa majimbo yatashindwa kutekeleza hatua kwa umakini unaofaa kuna uwezekano wa kuzingatia kuchukua hatua kali za nchi nzima. Mojawapo ya hatua hizo itakuwa ni kuwataka wafanyabiashara kuwapima wafanyakazi wao ambao hawawezi kufanya kazi kutokea nyumbani. Merkel anaamini kwamba hatua zilizoko sasa hazitoshi kukabiliana na wimbi la tatu la maambukizi.

Kulingana na bi Merkel, hatua zinazohitajika ni pamoja na kuzuia watu kutoka nje, vizuizi vya watu kuwasiliana, kuvaa barakoa sambamba na mikakati ya upimaji katika maeneo yote, iwe shuleni au katika biashara angalau mara mbili kwa wiki. Ujerumani ilisifiwa namna ilivyoshughulikia wimbi la kwanza la maambukizi lakini inapambana kudhibiti maambukizi mapya ya tangu wimbi la pili mwaka uliopita.Merkel abatilisha mpango wa kufunga maduka wakati wa Pasaka

Merkel alikutana na viongozi wa majimbo wiki iliyopita na kukubaliana kuchukua hatua kali wakati wa sikukuu za pasaka ambapo maduka yote yangefungwa. Hata hivyo walibadilisha uamuzi huo siku mbili baadae na kukiri kwamba vizuizi hivyo vingeumiza sana uchumi. Akikabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye bungeni, Kansela Merkel alijitwisha mzigo wa lawama na kuomba radhi akiwataka wajerumani wamsamehe kwamba yalikuwa ni makosa yake.

Merkel anatarajiwa kukutana tena na viongozi wa majimbo Aprili 12, lakini kutokana na idadi ya maambukizi kuongezeka wengi wanaona kuwa hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.