1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Macron wasisitiza utandawazi Davos

Sekione Kitojo
25 Januari 2018

Wahariri wa magazeti  ya  Ujerumani  leo wanazungumzia kuhusu hotuba za viongozi wa Ujerumani na  Ufaransa katika kongamano  la Davos na silaha za  Ujerumani kutumiwa  na majeshi ya Uturuki dhidi ya  Wakurdi wa Syria.

https://p.dw.com/p/2rUWW
Schweiz Davos - Angela Merkel beim World Economics Forum (WEF)
Kansela Angela Merkel akihutubia kongamano la kiuchumi mjini DavosPicha: picture-alliance/AP Photo/Keystone/L. Gillieron

Gazeti  la  Frankfurter Rundschau kuhusiana  na  hotuba  za  kansela Angela Merkel  na  rais wa Ufaransa Emmanuel Macron  katika kongamano  la  kiuchumi  la  Davos  linaandika:

"Haishangazi, lakini  ni  muhimu. Wakati kansela  Angela  Merkel  na rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron walichozungumza  katika kongamano  la  kiuchumi  mjini  Davos, kuhusu  umuhimu  wa  dunia kufanyakazi  kwa  pamoja, na  anayekusudiwa  kuelezwa  hayo hakuwapo  katika  ukumbi  wa  mkutano. Ni rais  wa  Marekani Donald Trump, anayetaka  kujitenga, na  kuudhoofisha  ushirikiano na  maridhiano. Trump  atahutubia kesho Ijumaa mjini  Davos. Matarajio ni  kwamba  atatetea  sera  zake  za Marekani  kwanza, kinyume  na wanavyotaka Merkel  na  Macron. Viongozi  hao muhimu  katika  bara  la  Ulaya  wanatoa  ishara kwamba bara  hilo lina  uwezo wa  kupambana  licha  ya  Marekani  kutangaza  vita vya biashara. Tatizo  lakini, kwa  Merkel  na  Macron  ni  muda , mhariri anaandika. Kwamba  ni  miezi  michache  mno  imebakia , kwa  Ulaya kuweza  kuonesha  ushindani. Baada  ya  hapo  mataifa  wanachama yatakuwa  wanaangalia  zaidi  kuhusu  uchaguzi  wa  mwaka  2019 na kwa  hiyo hali  hiyo  itadhoofika. Trump kwa  upande  wake muda anao."

Gazeti  la  Frankfuter Allgemeine,  kuhusu  mada  hiyo  ya  hotuba ya Merkel  katika kongamano  la  Davos  linaandika:

"Ni  sahihi  kabisa  kwa  Angela  Merkel  kutetea  utaratibu wa kuendelea  kuwa  na  uhuru  katika  dunia dhidi  ya  wakosoaji  wake na wale  wasiotaka  kumpa sifa yake. Kwa sababu  utaratibu  huu uko  kwa  maslahi  ya  kisiasa , kiuchumi  na  kimkakati  kwa Ujerumani. Lakini  pia Merkel  hana  budi  kuchukua  hatua  za kufanyakazi  pamoja na  makundi  dhaifu  ya  kimataifa , ili kuweza kuondoa  hali  ya  mtengano ,siasa za uzalendo na siasa  kali  za mrengo  wa  kulia katika  mataifa  ya  magharibi. Ili kutoleta  tena hali  ya  mivutano  kuhusu  utandawazi,  kutovuruga utaratibu  wa kidigitali, na  pia  uhamiaji. Katika  kongamano  la  Davos mtu anatarajia  kusikia  ulinzi  wa  faida za  utandawazi, na  kuzuwia kurejea nyuma na  kutumbukia  katika  siasa  za  kizalendo."

Kuhusiana  na hatua  ya  Uturuki  kuwashambulia  Wakurdi  nchini Syria , gazeti  la  Münchener Merkurs  linaandika:

"Hivi  sasa  kuna  mtafaruku  mkubwa. Hususan  kwa  kuwa  nchini Syria  jeshi  la  Uturuki  likiwa  na  vifaru  vilivyotengenezwa  nchini Ujerumani  linapambana  na  Wakurdi. Kuna  madai  kwamba  ni lazima kuzuwia  mauzo  yote  ya  silaha kwa  sasa. Hii  inapendeza masikioni ,  na  ni  sahihi, lakini  kimsingi ni  hatua  kubwa  zaidi. Hata  kama  haipendezi. Ulinzi  wa  nchi  yoyote  ni suala  muhimu sana  kwa  kila  serikali. Kwa  hiyo ni  lazima  kwa  kila  nchi kujihusisha  na  nyingine  na  kuipatia  silaha  za  kutosha. Kwa  hilo tunapaswa  kuwa  pamoja  na mwanachama  wa NATO  Uturuki. Na kwa  wakurdi kuwapa  silaha  kwa  ajili  ya  mapambano  yao muhimu dhidi  ya  IS. Hali  hii  inaonesha, ni ugumu  kiasi gani  kutoa  jibu muafaka."

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga