1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mingine mitano kwa Magufuli?

Anaclet Rwegayura30 Julai 2020

Ni nani mwingine kama sio John Pombe Magufuli kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka mitano ijayo? Ndilo swali analoliuliza mchambuzi wetu Anaclet Rwegayura katika Barua kutoka Dar.

https://p.dw.com/p/3gBuo
Rais John Magufuli
Picha: Getty Images/AFP/M. Spatari

Kwa lugha ya kibiashara, mtu anaweza kusema dimba limefungwa kati ya ‘Bw. Buldoza' na chama cha wengi cha CCM kwa ajili ya uchaguzi ujao wa rais. Kwa kuidhinishwa kwa kishindo na wanachama ili Magufuli awanie urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, tayari kunadhihirisha ushindi wake. Pia baadhi ya viongozi wa vyama vidogo vya siasa wametangaza kuunga mkono msimamo huo wakikiri kwamba kwa utendaji wake amedhihirisha kuwa ni kiongozi bora wa kitaifa.


Kadiri uchumi wa ulimwengu unavyoibuka polepole kutokana na athari za janga la Korona, Tanzania inahitaji watunga sera ambao wataiweka thabiti kwenye msingi uliowekwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Licha ya msukosuko wa uchumi ulipo barani Afrika kwa sababu ya janga hili, uchumi wa Tanzania haujapata pigo la kukatisha tamaa.

Wafanya biashara wa ndani wanahitaji sasa, zaidi kuliko hapo awali, kutoa huduma bora na bidhaa kwa watumiaji wa ndani wakati wanatafuta taarifa sahihi juu ya wateja na masoko mapya katika uchumi wa kimataifa baada ya janga la Korona. Hali ya sasa siyo ya kusema tena shughuli ni kama kawaida.


Gharama na ugumu wa kupata taarifa kama hizi zinaweza kuwa kizuizi kikubwa kwa makampuni madogo kuingia katika ushindani wa soko la kimataifa kwa sababu yana rasilimali duni za kuyawezesha kukusanya na kuchambua taarifa zenye utata na zilizotawanywa katika vyanzo vingi.

Pamoja na miundombinu inayofaa ambayo Magufuli amejitahidi kuweka katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano ya urais, serikali inapaswa ichukue hatua za kijasiri kutumia gesi asilia ya Tanzania na rasilimali zingine, pamoja na uvuvi, ili kuibadilisha nchi kuwa uwanja wa ukuaji wa viwanda.


Wanasiasa wanaowania uchaguzi kama wawakilishi wa watu katika bunge lazima watambue kuwa taifa linafanya safari ya mabadiliko ya biashara ambayo itawahusisha wazalishaji wadogo na wakubwa katika kila nyanja pamoja na watoa huduma, ili kuongeza kasi ya kufungua nafasi za ajira katika biashara ndogo, za kati na kubwa vile vile.

Hatutarajii kwamba kipindi cha  pili cha miaka mitano ya uongozi wa Magufuli kitakuwa rahisi. Hiki ni kipindi ambapo inabidi atimize ndoto ya kuliongoza taifa hili kufikia mafanikio na watu wapate fursa ya kushuhudia ahadi hiyo ikitimizwa kabla hajakabidhi madaraka kwa mrithi wake.

Jinsi atakavyokabidhi joho la madaraka ndiyo itakuwa kipimo cha mwisho cha mafanikio yake ya uongozi.

Siku ambayo alitangaza rasmi nia yake kuwania madaraka, alisema kwamba bado ana kazi nyingi mikononi mwake kama rais ambazo hazijakamilika. Kweli, ametoa mchango mkubwa katika hatua ya mwanzo ya kuzindua maendeleo ya Tanzania kama taifa la kipato cha kati.

Ili kutekeleza kazi iliyobaki kwa mafanikio, rais anahitaji msaada wa umma kupitia wanasiasa wengine maarufu watakaochaguliwa. Lazima hawa wawe watu walio na maono na uwezo mkubwa wa kimaendeleo katika kila fani ili kuiweka Tanzania juu katika uchumi wa kimataifa baada ya janga la Korona, ambapo misaada kutoka kwa wabia wa nje inatarajiwa kupungua sana.

Sekta za uzalishaji na huduma nchini, ziwe za umma au zinazoendeshwa kibinafsi, zinapaswa zikabidhiwe kwa usimamizi ambao unaenda sanjari na mwenendo wa biashara na soko na zifanye maamuzi madhubuti katika soko la kimataifa ambalo linabadilika haraka.

Tunapojitahidi kuinuka na kusimama kwa miguu yetu wenyewe kutokana na athari za janga la Korona ipo haja ya kutambua fursa tuliyonayo ya kutazama tena na kuboresha sera ya uchumi kwa kuweka mustakabali bora kwa taifa.


Itakuwa vizuri wananchi wakianzisha na kushiriki katika majadiliano katika ngazi zote za mitaa na kitaifa kwa lengo la kupata njia mbalimbali za kuchochea tija. Kuna shughuli nyingi ndogo na biashara za kibinafsi zinazokabiliwa na uwezo mdogo kifedha, lakini zikipata kichocheo cha fedha kutoka benki, zina uwezo wa kuongeza ajira zaidi na utajiri. Mwishowe, zitakuwa katika nafasi bora ya kuvutia wawekezaji wapya.
Tanzania ya kipato cha kati, ambayo ni lengo la maendeleo la Rais Magufuli, itajengwa juu ya uchaguzi tunaokaribia kufanya nchini sasa.