1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misitu ya Afrika Magharibi yanatoweka

Lillian Urio12 Julai 2005

Msitu mkubwa wa Afrika unaanzia kutoka nchi ya Cameron, kupitia nchi zilizo katikati mwa Afrika za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Guniea ya ikueta hadi Gabon. Huu ni msitu wa pili kwa ukubwa duniani, baada ya ule wa Amazon uliopo bara la Marekani Kusini. Lakini msitu huu unatoweka na hii hubadilisha hali ya hewa ya eneo hilo.

https://p.dw.com/p/CHfx
Misitu nchini Gabon
Misitu nchini GabonPicha: AP

Watafiti wanakadiria kuwa asilimia 40 hadi 60 ya aina zote za wanyama duniani zinapatikana kwenye msitu huu. Lakini kama ilivyo kwa msitu wa Amazon, msitu wa Afrika uko hatarini kutokana na ukataji miti ovyo na uchomaji moto, kwa ajili ya kutengeneza mashamba.

Shirika la kimataifa la kulinda mazingira, Greenpeace, limesema katika kipindi cha miaka 30 iliyopita zaidi ya nusu ya misitu ya Afrika imetoweka. Matokeo yake ni hali ya hewa katika maeneo hayo imebadilika.

Watafiti kutoka mji wa Bonn nchini, Ujerumani, wametengeneza mazingira bandia, yanayofanana na yale ya msitu wa Afrika, ili kuangalia ni jinsi gani mabadiliko katika mazingira hayo yanavyobadilisha hali ya hewa ya Afrika Magharibi.

Leo hii bado kuna misitu mikubwa iliyopo Magharibi mwa Afrika. Lakini kuna uwezekano itapotea katika kipindi cha wakati ujao na mazingira ya eneo hilo yatabadilika.

Makampuni ya mbao yanakata miti kwa wingi na wakulima wanachoma vichaka, ili kupata ardhi ya kulima kwa ajili ya jamii zinazokuwa.

Wakulima hugeuza maeneo waliotumia kama mashamba kuwa majangwa sababu walitumia mfumo mbaya wa kulima au walitumia sehemu ndogo kwa kulishia mifugo mingi.

Wanajiografia na watabiri wa hali ya hewa wa chuo cha Bonn wamefanya uchunguzi, kwa kutumia kompyuta, juu ya madhara ya mabadiliko hayo.

Mwanajeografia Heiko Päth amesema:

“Tumejaribu kuiga mabadiliko haya, kwa kutumia vipimo vya hali ya hewa vya eneo hilo. Tumegundua kwamba ongezeko la gesi inayodhuru hewa haibadilishi hali ya hewa kama ilivyokuwa hapo awali, ilikuwa inaongeza kipindi cha mvua, lakini sasa kiwango cha mvua kinapungua kwa kiasi kikubwa”.

Kama makadirio ya wanasayansi ni ya kweli, basi miaka 20 ijayo kiwango cha mvua kitakachonyesha Magharibi mwa Afrika, kitakuwa nusu ya kiwanga cha sasa hivi.

Sehemu za ukame kama Sahel zitegemee upungufu wa maji, kama misitu na sehemu zenye majani zitaendelea kutoweka kwa kasi ya sasa hivi. Barani Afrika, kiwango cha mvua kitazidi kama misitu itaongezeka.

Bwana Päth anaelezea:

“Mimea inachangia kama ifuatavyo. Idadi kubwa ya mvua inayonyesha kwenye mimea inaweza kuvukiza vizuri. Na kutokana na hilo, kunakuwa na mzunguko wa mvua kila mara na mzunguko huu utasita kama mimea itatoweka”.

Mvua nyingi za Afrika sio kama zile za Ulaya sababu zinatokana na mvua za radi. Mvua hizi hunyesha kutokana na unyevu kutoka ardhini hupanda kwenye hali ya hewa. Ndio maana katika sehemu za ukame, kama Sahara, pamoja na kuwepo kwa joto kali, hamna mvua za radi.

Kama ukataji wa miti ovyo utaendelea Afrika Magharibi kwa kasi ya sasa hivi, basi sehemu hiyo itazidi kuwa ya joto katika miaka ijayo. Misimu ya ukame itakuwa ya kawaida.

Bwana Päth anasema hali hii ikitokea, litakuwa janga kubwa kwa nchi za joto za Afrika. Anaeleza kwamba kuna uwezo wa kurekebisha mambo katika maeneo husika, ambayo sio tu gesi inayoharibu hali ya hewa ndio inadhuru maeneo hao.

Nchi hizo za Afrika zisingeweza kupambana na nchi zilizoendelea na kuzifanya zipunguze kasi ya kuachia gesi hizo hewani. Lakini nchi hizo zitaweza kulinda misitu yao.

Kadri nchi za Afrika Magharibi zitakavyoongeza maeneo ya hifadhi, basi zitaongeza uwezo wa kuwa na mvua. Na kama hazitafanya mabadiliko yoyote, basi Bwana Päth anahofu kwamba hali ya maisha ya watu itazidi kuwa ngumu.