1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kundi la G-8

9 Julai 2008

Mkutano wa kundi la G-8 umemalizika bila ya kuzaa matunda mengi.

https://p.dw.com/p/EZIS

Kwa muda wa siku 3 , mkutano wa kilele wa kundi la nchi 8 tajiri kabisa duniani-G-8 ikijumuisha Russia,ulizungumzia matatizo yanayoukabili ulimwengu wetu: kupanda mno kwa bei ya mafuta ya petroli na za chakula,msukosuko wa masoko ya fedha,msaada kwa bara la Afrika na mageuzi katika mfumo wa biashara ulimwenguni.

Lakini, mkutano huu wa 34 wa kundi hili la G-8 umezaa matunda gani ? Maazimio uliopitisha huko Hokkaido yana maana gani ?

Kila mwaka imegeuka desturi wakati wa majira haya ya kiangazi kukutana kwa viongozi wa dola na serikali wa nchi tajiri na zilizoendelea mno kiviwanda .Huamua kukutana katika vituo vya kifahari na ambako hawatakerwa ili kuzingatia matatizo yanayoisumbua sayari yetu.Mwishoe, daima hupiga picha pamoja na kutoa ahadi nyingi vipi kuifanya dunia hii kuwa bora na mahala pa kustarehe.

Kwahivyo, kwa muda wa siku 3 waakilishi hao wa kundi la nchi 8 tajiri wamekutana mjini Toyako,katika kisiwa cha Haokkaido,mwisho wa dunia.Ajenda zilikuwa nyingi na tofauti kuliko ilivyokua katika vikao vya miaka 33 iliyopita ya historia ya G-8.Hata idadi ya wageni walioalikwa mara hii ni rekodi.viongozi 22 vilikaa mezani.

Swali la kuzuwia kuchafuka zaidi kwa hali ya hewa ulimwenguni kwa mara nyengine uamuzi umeahirishwa.Ingawa nchi zilizowakilishwa mkutanoni ndizo dhamana ya uchafuzi huo kwa kima cha hadi 80 %.kilichoamuliwa ni hatua ndogo tu usoni.

Kwani, imeafikiwa kupunguza moshi unaochafua hali ya hewa kwa kima cha nusu hadi ifikapo mwaka 2050.

Kwa jicho la kwanza hii yaonekana ni hatua madhubuti, lakini hiyo ni miaka 42.ufumbuzi wa kitandawili hiki cha uchafuzi wa hewa kinaachwa mabegani mwa kizazi kijacho.

Kinachotia tamaa tu ni kumuona muakilishi mmmoja George Bush, rais wa Marekani mara hii akiaga madarakani ameregeza kidogo kamba .

Saa ya kuukabili ukweli itgonga baada ya kupita siku 500 pale utakapofanyika mkutano ujao wa hali ya hewa mjini Copenhagen,Denmark,2009.Huko itadhihirika dhahiri-shahiri maana hasa ya ahadi zilizotolewa Toyako.Yamkinika sana ulimwengu unasubiri kuvunjwa moyo sana.

Hata mnamo siku 3 za mkutano huu wa kilele wa hivi punde, binadamu tena wamefariki dunia kwa kuwa hawakuwa na chakula cha kula au maji safi ya kunywa .Msukosuko mkubwa wa chakula unazidisha maafa yao.Barani Asia, 60% ya pato la watu linakwenda kununua chakula tu. Na viongozi wa dola kuu 8 tajiri wanafanya nini ?

Wametoa sadaka mabilioni machache na kuahidi kuimarisha miundo-mbinu ya kilimo barani Afrika.

Lakini ni nani hasa alieporomoa na kuichafua miundo mbinu ya kilimo chao ? Bila shaka ni mataifa tajiri ya kaskazini mwa dunia hii.

Na sasa yanatoa ahadi kubwa kubwa kurahisisha biashara ya bidhaa zao za ngambo.Lakini inapokuja kuregeza masharti yao ya kibiashara,wanatia munda.Hata katika sekta hii,tutumai kuvunjwa moyo.

Jambo jengine jema kutoka G-8 ni swali la nishati ya bio -nishati inayotengezwa kwa mimea:Nishati hii sasa haitahimizwa sana ili uzalishaji wa chakula usiathirike.

Kwa jicho la matatizo makubwa yanayolikabili bara la Afrika,

msaada ulioahidiwa Afrika uliwekwa pembezoni.Ahadi zilizotolewa katika vikao vya kabla ulisisitizwa tena kuwa utatolewa na haukufutwa kama ilivyohofiwa.

Na ili kuzuwia masoko ya fedha yasiporomoke kabisa, kwa muda mfupi tu zimechangwa dala bilioni 1 kuyaokoa.Fedha tu zilizougharimia mkutano huu wa kilele huko Japan, zingetosha kuwsatibu wagonjwa milioni 4 wa Ukimwi.

Kimebakia nini kutoka mkutano huu wa G-8 huko kisiwani Hokkaido,Japan ? Nchi tajiri za kundi la G-8, zimeshindwa kutoa jibu linalostahiki.Ili kuyatatua matatizo ya sayari hii, wao sio jukwaa linalofaa.Kundi hili litapaswa kufungua milango yake kwa nchi kama China na India au sivyo, halitakua na maana yoyote.