1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa CIA Pompeo alikutana na Kim Jong Un kisiri

18 Aprili 2018

Mkuu wa shirika la ujasusi Marekani CIA Mike Pompeo hivi karibuni, alisafiri kwenda Korea Kaskazini kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un katika ziara ya siri na ambayo si ya kawaida.

https://p.dw.com/p/2wEiS
USA Mike Pompeo
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Ziara hiyo ilifanyika wakati ambapo mataifa hayo hasimu yanajiandaa kwa mazungumzo baina ya Rais Donald Trump na Kim katika miezi michache ijayo.

Maafisa wawili Jumanne walithibitisha ziara hiyo ya Pompeo kwa shirika la habari la Associated Press. Ingawa hawakuwa na idhini ya kulizungumzia suala hilo, walizungumza ila wakataka wasitambulishwe. Gazeti la Washington Post ambalo ndilo la kwanza kufichua mkutano wa Pompeo na Kim lilisema mkutano huo ulifanyika katika ile wikendi ya Pasaka karibu wiki mbili zilizopita, muda mfupi baada ya mkuu huyo wa ujasusi kuteuliwa kama Waziri wa Mambo ya nje.

Trump ambaye amemkaribisha Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe huko Florida alisema Marekani na Korea Kaskazini zinafanya mazungumzo ya moja kwa moja.

Ombi la Kim kukutana na Trump liliwasilishwa na Korea Kusini

"Tumekuwa na mazungumzo ya ngazi ya juu. Wacha nisiseme mengi lakini tumekuwa na mazungumzo ya ngazi ya juu," alisema Trump.

USA Mar-a-Lago US Präsident Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Ombi la Kim la kutaka mazungumzo liliwasilishwa kwa Trump na Korea Kusini mwezi uliopita na rais huyo akawashangaza wengi kwa kulikubali. Maafisa wa Marekani katika wiki mbili zilizopita wameeleza kwamba Korea Kaskazini imezungumza moja kwa moja na Marekani na kwamba iko tayari kujadili mpango wake wa silaha za nyuklia. Huu ndio utakuwa mkutano wa kwanza kabisa baina ya Marekani na Korea Kaskazini katika zaidi ya miongo sita ya uhasama tangu vile vita vya Korea.

Huku mkutano huo ukiwa unapangwa familia za raia wa Japan waliotekwa nyara na Korea Kaskazini zinamtaka rais Trump kufanya jitihada zaidi wapendwa wao waachiwe atakapokutana na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini.

Familia za raia wa Japan waliotekwa nyara na Korea Kaskazini zinamtaka rais Trump kushinikiza kiuachiwa kwa Wajapan hao wakati atakapoliibua suala hilo kwenye mazungumzo yao. Rais huyo wa Marekani alimwambia Shinzo Abe katika mkutano wao kwamba hilo suala la utekwaji wa Wajapan litakuwa miongoni mwa mambo atakayoyajadili.

Mkutano wa Trump na Abe ulichochewa na hofu ya Marekani na Japan kuhusu Korea Kaskazini

Korea Kaszini imekiri kuwateka nyara Wajapan 13 ila Japan yenyewe inasema idadi ni watu 17.

Huku hayo yakiarifiwa katika harakati za kumuhakikishia Waziri Mkuu Abe kwamba Marekani iko karibu na nchi yake, Trump amesema utawala wake uko tayari kuiondolea Japan ushuru katika bidhaa za chuma cha pua na bati. Lakini wachambuzi wanasema Marekani haitofanya hivyo bure. Yoshino Takashi ni profesa katika Chuo Kikuu cha Waseda nchini Japan.

Washington Abe bei Trump
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe akizungumza na Trump huko Florida, JumannePicha: Reuters/K. Lamarque

"Iwapo Japan ina matumaini itaondolewa ushuru wa chuma cha pua na bati ninahofia kwamba Marekani itaitaka Japan kufungua soko lake la magari na bidhaa za kilimo jambo ambalo imelikamia sana, lakini haiwezekani Japan kufanya hivyo," alisema Takashi.

Mkutano wa Trump na Abe ulipangwa kutokana na hofu inayozidi baina ya Marekani na Japan kuhusiana na Korea Kaskazini na biashara. Japan imeelezea wasiwasi wake kwamba huenda ikawa Kim anataka tu kupoteza muda na huenda pia Marekani ikashindwa kumshinikiza kiongozi huyo kuharibu makombora yake ya masafa mafupi na masafa ya kadri ambayo ni kitisho kwa Japan.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE

Mhariri: Caro Robi