1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa msituni wazusha sokomoko kusini mwa Ulaya

Daniel Gakuba
18 Julai 2022

Maelfu ya watu wamehamishwa kutoka makaazi yao nchini Ufaransa na Uhispania, kuwanusuru na moto mkali unaoteketeza misitu na mashamba kusini mwa bara Ulaya, sambamba na wimbi la joto kali linalovunja rekodi.

https://p.dw.com/p/4EGQi
Frankreich | Waldbrände Rehion Bordeaux
Picha: SDIS 33/AP/picture alliance

Kwa siku sita mfululizo sasa, moto mkali umeteketeza maeneo ya misitu ya misonobari karibu na mji wa Bordeaux kusini magharibi mwa Ufaransa, ambako watu 14,000 wamelazimika kuhamishwa, miongoni mwao wakiwemo waliokuwa wakifurahia mapumziko yao.

Soma zaidi: Moto wa msituni wateketeza kusini magharibi mwa Ulaya 

Wazimamoto wa Ufaransa na Uhispania wanajaribu kila wanaloweza kupambana na moto huo katika mazingira ya joto kali ambalo maafisa wanalifungamanisha na mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya maeneo ya Ulaya yanakabiliwa na viwango vya joto vya kuvunja rekodi mwanzoni mwa wiki hii.

Portugal Leiria | Evakuierung nach Waldbränden
Watu wamelazimika kuyapa kisoko makaazi yao kuepuka shari ya moto unaovinyemelea vijiji vyaoPicha: Rodrigo Antunes/REUTERS

Maelfu ya hekari za mashamba yaangamizwa

Katika mkoa wa Gironde wa kusini magharibi mwa Ufaransa, hekari 27,000 za mashamba zimeharibiwa na moto huo tangu Jumanne iliyopita, na watu 16,000 wameyapa kisogo makaazi yao na kukimbilia katika vituo saba vilivyowekwa maalumu kuwapokea. Mamlaka nchini humo zimesema zinapeleka ndege tatu za ziada kusaidia shughuli za kuzima moto huo, pamoja na maafisa 200 na magari yao ya kazi.

Soma zaidi: Joto kali kwenye eneo la Arctic laongeza kitisho ulimwenguni

Mbali na mkoa wa Gironde, wilaya nyingine 15 zimewekwa katika hali ya tahadhari kuanzia jana Jumapili. Idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema inatarajiwa kiwango cha joto kupanda hadi nyuzijoto 40 za Celsius leo Jumatatu.

Huko Uhispania nako hali si shwari, ingawa mkuu wa mkoa wa Andalusia Juan Manuel Moreno amesema maafisa wa zimamoto wameweza kuudhibiti moto wa msituni ulioangamiza karibu hekari 5000 za misitu na vichaka katika mkoa huo wa kusini.

Italien | Hitzewelle in Italien
Ulaya inakabiliwa na viwango vya joto vya kuvunja rekodiPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Joto latarajiwa kufika nyuzi 44 za Celsius

Katika mji wa mwambao wa kusini wa Malaga, watu 3000 walihamishwa kuepuka moto ulioyavamia maeneo yao ukitokea katika milima ya Mijas siku ya Ijumaa. Wengi wao walirejea baada moo huo kudhibitiwa. Hata hivyo hali bado ni tete, ikitarajiwa kuwa joto litapanda leo Jumatatu hadi kufika nyuzi 44 za Celsius. Taasisi ya Afya ya Carlos imesema hadi sasa vimetokea vifo vya watu 360 vinavyohusishwa na janga hili la joto kali.

Soma zaidi: Bara Ulaya lashuhudia viwango vya juu vya joto

Nchini Ureno moto huu wa msituni umeuwa watu wawili na kuwajeruhi wapatao sitini, na umeangamiza  hekari zipatazo 37,000 za mashamba. Nchi hiyo inatarajia kupigwa na wimbi la joto la nyuzi 42 za Celsius. Tayari vimesajiliwa vifo vya watu 238 vinavyohusiana na hali hii ya joto kali, wengi wakiwa wazee na watu waliokuwa na afya dhaifu.

 

AP, AFPE