1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wauwa mmoja, wajeruhi wanane Iraq

Mohammed Khelef
20 Aprili 2024

Mtu mmoja ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa usiku wa kuamkia Jumamosi (Aprili 20) kufuatia mripuko katika kituo kimoja cha jeshi la Iraq, ambacho kinatumiwa na muungano wa makundi yenye silaha yanayoiunga mkono Iran.

https://p.dw.com/p/4f0PS
Waziri Mkuu wa Iraq, Shia al-Sudani.
Waziri Mkuu wa Iraq, Shia al-Sudani.Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Mripuko huo ulitokea kwenye kituo cha jeshi cha Kalsu katika jimbo la Babylon lililo kusini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambako kuna vikosi vya muungano wa Hashed al-Shaabi.

Umetokea siku kadhaa baada ya Iran kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel, ambayo nayo iliripotiwa kutumia droni kuishambulia Iran siku ya Ijumaa, ingawa Tel Aviv haijathibitisha hilo.

Kitengo cha habari cha jeshi la Iraq kilisema "mripuko na moto" ulipiga kituo cha Kalsu alfajiri ya Jumamosi, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi wanane.

Soma zaidi: Israel yaendelea kuitwanga Gaza, wasiwasi wa vita na Iran wazidi

Lakini kamandi ya jeshi la anga ilisema "hakukuwa na droni wala ndege ya adui kwenye anga la jimbo la Babylon kabla wala wakati wa mripuko huo."

Hapo awali, afisa mmoja kutoka wizara ya mambo ya ndani alikuwa ameripoti "mashambulizi ya anga" kwenye eneo hilo.

Kundi la Hashed al-Shaabi lilisema kwenye taarifa yake kwamba "mripuko umesababisha hasara kwa watu na mali" bila kufafanuwa zaidi, ingawa lilikiri kuwa majengo yake kwenye kituo hicho cha kijeshi yameshambuliwa na  kwamba wachunguzi wametumwa kwenye eneo hilo.

Vikosi vya Marekani nchini Iraq.
Vikosi vya Marekani nchini Iraq.Picha: Khider Abbas/EPA/dpa/picture alliance

Hakukuwa na kundi wala nchi iliyodai kwa haraka kuhusika na mkasa huo, wala vyanzo vya usalama havikumtaja yeyote vinayemtuhumu kufanya mashambulizi hayo, ambayo wizara ya mambo ya ndani ilisema yaliathiri vifaa, silaha na magari.

Marekani yakanusha kuhusika

Muda mfupi baada ya mripuko huo,jeshi la Marekani lilisema vikosi vyake havikuhusika. "Marekani haijafanya mashambuli ya anga nchini Iraq leo," ilisema Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kupitia mtandao wa kijamii wa X, ikiongeza kuwa ripoti kwamba wanajeshi wa Marekani wamefanya mashambulizi "si za kweli."

Afisa mmoja wa jeshi la Iraq aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mripuko huo ulitokea kwenye ghala la silaha. 

Wakati shirika hilo la habari lilipotaka kauli ya jeshi la Israel, liliambia kuwa jeshi hilo "halizungumzii taarifa zinazochapishwa na vyombo vya kigeni."

Soma zaidi: Kwa nini nchi za Kiarabu ziliisaidia Israel dhidi ya Iran?

Hashed al-Shaabi ni kitengo kwenye vyombo vya usalama vya Iraq ambacho kipo chini ya mamlaka ya waziri mkuu na kinachoyaleta pamoja makundi mbalimbali yenye silaha na yanayoiunga mkono Iran. 

Miongoni mwa makundi hayo yamewahi kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani ndani ya Iraq na Syria.

Shia al-Sudani
Waziri Mkuu wa Iraq, Shia al-Sudani (katikati), akiwa mjini Washington na Rais Joe Biden wa Marekani.Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Kamanda wa kitengo hicho, Abu Alaa al-Walai aliandika kupitia mtando wa X kwamba wangelipiza kisasi kwa yeyote aliyehusika na mashambulizi hayo. "Waliohusika na uhalifu huu watapata majibu yao." Alisema.

Soma zaidi: Marekani yafanya mashambulizi ya anga huko Iraq na Syria

Siku ya Ijumaa (Aprili 19) mashambulizi ya anga yanayoshukiwa kufanywa na Israel yalilenga kituo kimoja cha jeshi karibu na mji wa Isfahan katikati ya Iran.

Wizara ya mambo ya nje ya Iraq ilielezea wasiwasi wake kuhusu mashambulizi hayo, ikionya kwamba "yanaweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi unaotishia usalama na utulivu wa ukanda mzima" wa Mashariki ya Kati.

"Mambol haya hayapaswi kuruhusu kuondosha makini ya watu kutoka kile kinachoendelea kwenye Ukanda wa Gaza," iliongeza wizara hiyo.

Waziri Mkuu wa Iraq, Mohamed Shia al-Sudani, yuko mjini Washington, ambako alikutana na Rais Joe Biden wa Marekani wiki hii.