1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msichana apambana na malaria kwa mishumaa

Mohammed Khelef
26 Juni 2018

Yumkini sasa ugonjwa hatari wa malaria unaweza ukawa historia nchini Tanzania, kutokana na mbinu mbalimbali zinazoibuliwa na wananchi wa kawaida kukabiliana na ugonjwa huu sugu katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/30I3S
Tansania Kerzen gegen Malaria
Picha: DW/E. Boniphace

Serikali imekuwa ikifanya juhudi katika kukabiliana na malaria kwa kunyunyizia dawa za kuuwa viluwiluwi vinavyosababisha ugonjwa huo kwenye makaazi ya watu, kugawa vyandarua vyenye dawa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na ugonjwa huu. 

Licha ya jitihada hizi kusaidia, lakini tatizo la msingi bado liliendelea kuwapo. Nalo ni uwelewa mdogo wa walengwa kwenye kampeni yenyewe. Lakini sasa matumaini ya kutokomeza malaria yamezaliwa upya baada ya kutengenezwa kwa mishumaa inayofukuza mbu, hatua itakayoongeza nguvu katika juhudi za kupambana na ugonjwa huu.

Beatrice Mkama ni mjasiriamali mwenye ndoto za kuisaidia jamii yake katika kuitokomeza malaria iliyosababisha kuondokewa na ndugu zake waliofariki baada ya kuugua ugonjwa huo.

Beatrice, ambaye kitaaluma amesomea uhazili ngazi ya stashahada katika chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam, anasema alitamani kujifunza ujasiriamali lakini alishindwa kuamua nini asomee mpaka alipokutana na mkufunzi mmoja kupitia mitandao ya kijamii kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).

"Tuliambiwa mwalimu huyo alikuwa anafundisha kutengeneza mishumaa, kichwani nilijua nakwenda kupata kitu kipya. Nilivyokuwa naangalia mishumaa, nilikuwa napata maswali inakuwaje utambi unakaa katikati?"

Hata hivyo, Beatrice na wenzake sita hawakufahamu kama mwalimu huyo alikuwa akifundisha utengenezaji wa mishumaa ya mbu. 

"Alipotaja kufundisha mishumaa hiyo, wote tulivutiwa nayo. Tulijifunza kwa masaa mawili na tulielewa somo".

Tatizo la gharama

Beatrice anasema alianza kutengeneza mishumaa hiyo mwezi Disemba mwaka jana na kuiuza Januari mwaka huu, lakini hadi sasa jamii inayomzunguka imeshindwa kumudu gharama za mishumaa hiyo anayoiuza shilingi 1000 kutokana na familia hizo kuwa na uwezo duni kiuchumi.

"Wanasema bei ni kubwa. Huwa najitahidi kuwaelimisha kuhusu mishumaa hii, ila wanataka iwe bei sawa na mishumaa ya kawaida".
Kutokana na changamoto hiyo, Beatrice huamua kugawa bure baadhi ya mishumaa anayoitengeneza kwa familia hizo ili wajiridhishe jinsi inavyofanya kazi.

"Wanasifu tu, wakiwasha mbu hakuna. Wengine wanahoji mbona hatuoni mbu wakifa? Hii dawa inafukuza mbu sio kila muda utakuwa kwenye chandarua".

Kama ulivyo usemi wa "Nabii hakubaliki kwao", naye Beatrice amefanikiwa kupata wateja nje ya eneo analoishi baada ya kufungua ukurasa wake katika mitandao ya kijamii kujitangaza kwa jina la ‘Moonlight_business:’ 

Kutokana na kufanya kazi katika mazingira ambayo sio rasmi na mtaji mdogo, Beatrice hutengeneza mishumaa 100 tu kwa siku, ambapo hutumia dawa aina ya ‘stronela’ yenye uwezo wa kuuwa mbu kisha huchanganywa na nta inayotokana na mafuta ya petroli. 

Lengo la Beatrice ni kuona jamii yake ikiondokana na adha ya mbu na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaougua malaria mara kwa mara.

Tansania Kerzen gegen Malaria
Beatrice Mkama akiweka uji uji wa nta katika kifaa chenye maumbo ya mishumaa katika eneo lake la kazi.Picha: DW/E. Boniphace
Tansania Kerzen gegen Malaria
Mishumaa ya kupambana na mbu.Picha: DW/E. Boniphace
Tansania Kerzen gegen Malaria
Mjasiriamali Beatrice Mkama akionesha mishumaa anayoitengeneza.Picha: DW/E. Boniphace

Mwandishi: Ericky Boniphace/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef