1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mufti wa Tanzania aomba kuarakishwa kesi ya masheikh

14 Juni 2021

Mufti Abubakar Zubeir ameitaka mamlaka Tanzania kutenda haki ili masheikh wa kundi la Uamsho wanaoendelea kushikiliwa gerezani kujua hatma yao.

https://p.dw.com/p/3utdS
Tansania Dar es Salaam | Kassim Majaliwa
Picha: Tanzania Presidents Office

Kiongozi wa huyo wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, BAKWATA, amesema siyo jambo la busara kuendelea kushuhuduia masheikh hao wakisota gerezani bila kujua hatma yao na kwamba ni wakati muafaka sasa mamlaka zinazohusika zikaharakisha kesi dhidi yao na hatimaye hatma yao ijulikane.

Mufti Zubeir ambaye alikuwa akizungumza mara baada ya kumaliza kikao cha pamoja na viongozi wa kidini waliokuwa wakijadili masuala mbali mbali ya nchini, amesema kwa kufanya hivyo hamaanishi kutaka kuingilia mamlaka za dola bali ni kiu ya wengi kutaka kuona suala linalowakabili mashehe hao linafikia tamati.

''Tuombe mamlaka husika,kuomba mahakama,mamalaka nyingine..., na kuiomba serikali kwa ujumla zile kesi zao ziharakishwe. Watakaoonekana wanamatatizo, sheria ichukuwe mkondo wake na wale ambao wataonekana hawana matatiizo basi waachiliwe.'', alisema sheikh Zubeir.

Masheikh hao ambao pia wamekuwa wakiendesha mihadhara, walitiwa mbaroni visiwani Zanzibar na baadaye walisafirishwa hadi jijini Dar es salaam, wakifunguliwa mashtraka kadhaa kikiwamo ya kuchochea vurugu na kushiliki vitendo vya uvujifu wa Amani.

Tangu kukamatwa kwao, kumekuwa na miito kutoka kwa makundi mbalimbali yanayohimiza kuachiwa kwao huru.

Miito ya kuachiliwa huru masheikh wa uamsho

Baadhi wanataka kesi dhidi yao iharakishwe huku wengine wakiisitiza kuwa, kuachiwa huru bila masharti ni jambo linalopaswa kutekelezwa hasa wakati huu ambako hali ya kisiasa visiwani Zanzibar ikiwa imetulia kutokana na kupatikana kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Kulingana na Mufti Zubeir, masheikh hao wamesota kwa muda mrefu gerezani hivyo, kuna haja sasa kulitupia kwa jicho la tatu suala linalowakabili viongozi hao.

Hivi karibuni pia, viongozi wa dini waliokutana huko Zanzibar walitoa taarifa ya pamoja wakisisitiza kuachiwa huru kwa mashehe hao. Kadhalika suala hilo limekuwa likiibuliwa bungeni mara kwa mara na baadhi ya wabunge wa chama cha ACT Wazalendo wanaotaka hatma ya viongozi hao ijulikane haraka.