1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote wakwama Tanzania

Deo Kaji Makomba
9 Februari 2023

Awali, ratiba ya Bunge iliyotolewa mnamo Januari 30, mwaka huu, ilionesha kuwa muswada huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa, ulipaswa kuwasilishwa leo

https://p.dw.com/p/4NIC2
Mhe Dr. Tulia Ackson, Spika wa bunge la Tanzania
Mhe Dr. Tulia Ackson, Spika wa bunge la TanzaniaPicha: Ericky Boniphace

Muswada huo unakwama wakati ambapo Wizara ya Afya nchini Tanzania imekuwa ikiunadi kwa wananchi na wadau wengine wa sekta ya afya, wakiwemo viongozi wa dini na waandishi wa habari ili kupata maoni yao kabla ya kuwasilishwa bungeni.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na mswaada huo kutowasilishwa bungeni hii leo, Spika wa Bunge Tulia Ackson amesema kuwa muswada huo ulishindwa kusomwa mara ya pili kwa sababu Serikali na Bunge bado walikuwa wakiendelea na majadiliano.

Aidha Spika Tulia amesema kuwa Bunge lilikuwa likiendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na wabunge, wadau mbalimbali waliojitokeza katika kamati na nyingine Serikali.

Hata hivyo, mnamo  tarehe 20 Januari mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo, alinukuliwa akisema kuwa kazi ya uchambuzi wa muswada huo ilikuwa imekamilika.

Hisia mseto za wananchi

Muswada huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa
Muswada huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwaPicha: DW

Kukwama kwa mswaada huo kwa mara nyingine tena kumepokelewa kwa hisia mseto hapa nchini kwani ulikuwa unasubiriwa kwa hamu. Baadhi yao wanasema ni jambo la kusikitisha kuwa hadi sasa serikali haijajipanga kwa suala hilo.

Mbali na mswada huo wa bima ya afya kukwama, kadhalika mswaada wa marekebisho ya mabadiliko ya sheria ya habari nchini ya mwaka 2016, uliokuwa uwasilishwe katika bunge hili unaonekana kukwama, huku kukiibuka maoni mseto kutoka kwa wadau wa habari nchini Tanzania. 

Miongoni mwa vipengele ambavyo vimekuwa vikipigiwa kelele katika sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 ni pamoja na kile cha kiwango cha elimu ambacho kinasema ili kutambulika kuwa mwandishi wa habari mtu anatakiwa kuwa na kiwango cha elimu kuanzia ngazi ya diploma na kipengele kingine ni kile kinachotoa adhabu ya makosa ya madai kuwa jinai.

Majadiliano baina ya serikali na bunge

Kwa upande wa muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, hii ni mara ya pili kukwama tangu usomwe kwa mara ya kwanza bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge na kupelekwa katika kamati ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuchambuliwa. Ikiwa kuna siku kila Mtanzania atakuwa na bima ya afya bila kujali kipato chake binafsi, linaendelea jambo la kungoja na kuona.