1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa kijeshi wadai kuwauwa waasi 165 Yemen

Sudi Mnette
18 Oktoba 2021

Majeshi ya muungano yanayoongozwa na Saudi Arabia kwa lengo la kuinga mkono serikali ya Yemen yamesema yamewauwa waasi 165 katika mashambulizi yake lililofanyika kusini mwa mji wa Marib.

https://p.dw.com/p/41nQB
Jemen Explosion in Aden
Picha: AP Photo/picture alliance

Katika muendelezo wa kuwania mji huo wa kimkakati, shirika la habari la Saudi Arabia limesema  vifo hivyo vimetokana na mashambulizi ya gari za kijeshi 10, ambayo yamefanyika katika kipindi cha masaa 24, yakijikita katika wilaya ya Abdiya.

Taarifa ya muungano huo wa kijeshi kwa ujumla imesema imewauwa takribani waasi 1,000 katika mashambulizi yake ya eneo hilo kwa juma lililopita na hivyo kuifanya idadi kubwa ya vifo vya waasi kwa kila siku.

Waasi wa Huthi hawajazungumzia athari za vifo

Hata hivyo waasi wa Huthi ambao kwa kawaida mara chache sana wanatoa taarifa ya athari za vita, hawakuweza kupatikana mara moja kuweza kuthibitisha taarifa hizo.

Kundi hilo lenye kuungwa mkono na Iran, lilianza mapigano ya kutaka kuudhibiti mji wa Marib, ambayo ni ngome ya mwisho ya serikali yenye kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, lakini pia mji wenye utajiri mkubwa wa mafuta huko kaskazini mwa Yemen. Na kwamba limekuwa likirejea kutekeleza mashambulizi yake katika wiki za hivi karibuni baada ya kuwa kimya katika kipindi kirefu.

Nani anaudhibiti mji wa Marib kati ya Huthi na Serikali ya Yemen?

Jemen Explosion in Aden
Mripuko katika mji wa AdenPicha: AP Photo/picture alliance

Lakini mapema jana Jumapili, kwa kupitia ukurasa wake wa Twitter kundi hilo la uasi liliandika limefanikiwa kuyadhibiti maeneo kadhaa ya mapambano karibu na Marib, likiwemo la wilaya ya Abdiya, ambalo lipo umbali wa kilometa 100 kusini mwa mji huo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen, vilianza 2014, baada ya Huthi kuudhibiti mji mkuu wa Sanaa, ambao upo umabli wa kilometa 120 magharibi mwa Marib, jambo ambalo lilisababisha majeshi yenye kuongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati kuisadia serikali ya taifa hilo.

Maelfu ya watu wameuwawa na wengine mamilioni wameachwa bila ya makazi, katika kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita janga baya kabisa la kiutu duniani. Hivi karibuni umoja huo ulitoa wito wa kusitishwa mapigano katika mji wa Abdiya, kwa kile unachosema usaidizi wa maelfu ya tani za misaada ya kiutu imezuiwa kabisa kufika katika maeneo hayo.

Kwa mwezi ulipita pekee umoja huo umetoa rekodi zinazoeleza kwamba karibu watu 10,000, wameachwa bila ya makazi. Na mratibu wa majanga ya kiutu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, David Gressly, na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ned Price kwa pamoja walitoa wito wa kufunguliwa kwa njia salama ya kuwafikisha raia misaada ya kibinaadamu.

Chanzo: AFP/RTR