1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya Ujerumani na Uturuki wachacha

Saumu Mwasimba
20 Julai 2017

Wanasiasa wa Ujerumani waghadhabishwa na Uturuki kwa kukamatwa raia wake katika mazingira yanayoonekana kuwa ya kisiasa zaidi na kubadikwa tuhuma zisizo na msingi

https://p.dw.com/p/2gtzQ
Berlin Außenminister Sigmar Gabriel zur Lage in der Türkei
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amekatisha mapumziko yake na mara moja amemwita balozi wa Uturuki nchini Ujerumani na kuwasilisha malalamiko juu ya kukamatwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu. Serikali ya shirikisho ya Ujerumani imetangaza hatua kali zitakazochukuliwa dhidi ya Uturuki.

Mambo yameshavuka mpaka,baada ya kukamatwa mjerumani mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Peter Steudner na polisi wa Uturuki wanasiasa wa Ujerumani wanaonekana kukerwa na kupoteza subira.Waziri wa mambo ya nje Sigmar Gabriel amelazimika kukatiza mapumziko yake na badala yake kurudi kazini na kuitisha kikao cha dharura kujadili huku kuongezeka kwa hatua za ukandamizaji za Uturuki.

Polisi wa Uturuki Julai 5 waliwakamata wanaharakati 10 wa haki za binadamu mjini Istanbul waliokuwa wakishirika warsha iliyoandaliwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.Agenda kuu ya Warsha hiyo ilihusiana na suala zima la jinsi ya kushughulikia mfadhaiko na msongo wa mawazo lakini waliokamatwa katika warsha hiyo wanne waliachiwa huru siku ya Jumanne na wanne wakaendelea kuzuiliwa na kuhojiwa miongoni mwao yumo pia raia wa kijerumani Steudtner  na mkurugenzi wa shirika la Amnesty International  tawi la Uturuki Idil Eser.

Türkei Jahrestag Putschversuch- Rede von Erdogan vor dem Parlament
Rais Tayyip Erdogan wa UturukiPicha: picture-alliance/abaca/M. Kaynak

Kuendelea kuzuiliwa huko kwa wanaharakati hao akiwemo raia wa Ujerumani kumezidi kuchochea mvutano wa kidiplomasia kati ya Ujerumani na Uturuki, balozi wa Uturuki mjini Berlin ameitwa kuhojiwa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani kama alivyodokeza msemaji wa wizara hiyo Martin Schäfer ambapo ameweka wazi kwamba balozi huyo wa serikali ya mjini Ankara amehojiwa na kuarifiwa kinagaubaga kwamba Ujerumani haitokubali katu kuruhusu kuendelea kushikiliwa kwa mwanaharakati raia wake pamoja na wanaharakati wengine wa haki za binadamu na kitendo hicho hakiwezi kusamehewa hata mara moja.

Pamoja na hayo Serikali ya Ujerumani imetoa onyo kwa raia wake kujiepusha au kuchukua tahadhari endapo wanaamua kusafiri kwenda Uturuki huku pia ikitishia kuchukua hatua ambazo huenda zinasababisha kuzuia uwezekezaji wa makampuni ya kijerumani katika nchi hiyo ya Uturuki ishara ambayo inazidi kuonesha kwamba Ujerumani imeishiwa subira na nchi hiyo mshirika mwenzie katika Jumuiya ya NATO baada ya kuwakamatwa wanaharakati hao wa haki za binadamu.

Wanaharakati wanaoshikiliwa na Uturuki wanatuhumiwa na nchi hiyo kwamba wanahusika na ugaidi madai ambayo serikali ya Ujerumani imeyaita ya uwongo yasiyokuwa na msingi.Waziri wa mambo ya nje Sigmar Gabriel amesema raia yoyote wa Ujerumani anakabiliwa na hatari ya kukamatwa nchini Uturuki hasa kwa kuzingatia kwamba raia wa Ujerumani anayeshikiliwa mjini Istanbul Peter Steudtner hakuwahi kuandika chochote kuhusu Uturuki na hakuwahi kuwa na mawasiliano yoyote yanayohusu siasa nchini humo na wala hakuwahi kuonekana kuikosoa nchi hiyo.

Türkei - Deutscher Menschenrechtler Peter Steudtner in U-Haft
Peter Steudtner-Mwanaharakati wa Ujerumani anayeshikiliwa UturukiPicha: picture alliance/dpa/Privat/TurkeyRelease Germany

Hata hivyo Ibrahim Kalin msemaji wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema wajerumani watakaozingatia  sheria za Uturuki hawana cha kukhofia kuingia nchini humo.Ujerumani inafikiria uwezekano wa kuiondolea Uturuki uhakika wa kusafirisha bidhaa nchini Ujerumani pamoja na kuipunguzia fungu la mamilioni ya Yuro inalolipata  Uturuki kutoka Umoja wa Ulaya.

Kufikia sasa kuna wajerumani kadhaa ambao baadhi  wana asili ya kituruki wanaozuiliwa nchini Uturuki na ambao huenda wakashikiliwa hadi miaka mitano nchini humo ambao ni pamoja na mwandishi habari Deniz-Yücel na mkalimani Mesale Tolu Corlu licha ya serikali ya Ujerumani kujaribu kila iwezalo kutia mbinyo ili waachiwe huru.