1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa makampuni ya IPP Reginald Mengi azikwa

Grace Kabogo
9 Mei 2019

Mwili wa aliekuwa mmiliki wa vyombo kadhaa vya habari nchini Tanzania Reginald Mengi, umezikwa katika makaburi ya familia nyumbani kwa wazazi wake mkoani Kilimanjaro, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaongoza waombolezaji kwenye mazishi hayo. 

https://p.dw.com/p/3IFKE

Sikiliza taarifa ya mwandishi wetu Veronica Natalis.

Tulipokuwa barabarani kuelekea kijiji cha Kisereni takribani kilometa 35 kutoka Moshi Mjini, tumeshuhudia umati mkubwa wa watu waliojipanga barabarani wakipunga mikono juu huku wengine wakipunga hewani matawi ya miti, kama ishara ya kumuaga Dk. Regnald Mengi.

Na hatimaye msafara ukafika katika kijiji cha Kisereni Machame mkoani Kilimanjaro, ambapo ndipo mwili wa mfanyabiashara huyo maarufu umehifadhiwa katika nyumba yake ya milele. Eneo alilozikwa Dk. Mengi ni eneo la makaburi ya familia ambapo pia wamezikwa wazazi wake na ndugu wengine. 

Kassim Majaliwa, Premierminister von Tansania
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim MajaliwaPicha: Büro des Premierministers von Tansania

Akitoa salamu za rambi rambi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu Kassim Majaaliwa amesema kuwa taifa litamkumbuka Dk. Mengi kwa mchango wake mkubwa wa kukuza uchumi nchini hasa katika sekta ya madini, habari na viwanda na mazingira, kwani amewahi kuwa mwenyekiti wa baraza la mazingira taifa.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mchango wa Dk. Mengi katika kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalumu utaendelea kukumbukwa daima.

Awali, akitoa mahubiri katika ibada ya mazishi hayo iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT, usharika wa Moshi Mjini, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Fredrick Shoo, pamoja na mambo mengine, aliwaasa viongozi wa serikali hasa wale wenye umri mdogo kuacha kiburi cha madaraka na badala yake watende haki kwa wananchi wote bila upendeleo.

Tanzania - Beerdigung Dr. Reginald Mengi's Gründer und Vorsitzender der IPP Gruppe
Wanafamilia wakiwa kwenye ibada ya mazishi ya Reginald MengiPicha: DW/V. Natalis

Askofu Shoo alisema Dk. Mengi hakuwabagua maskini japo alikuwa tajiri na tabia hiyo inapaswa kuigwa na watu wote wenye nafasi za uongozi serikalini, wenye madaraka na wenye pesa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, Freeman Mbowe, amekemea tabia ya ubaguzi wa ukabila unaooneshwa na baadhi ya viongozi wa serikali, na kwamba ili kumuenzi Mengi ni muhimu kuyaacha matendo hayo kwani marehemu Dk. Mengi alikuwa ni mtu wa kujishusha japo alikuwa bilionea.