1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaanzisha mazungumzo na Afghanistan

22 Desemba 2013

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeanzisha mazungumzo na Afghanistan kuhusu mpango uliopendekezwa wa kuyabakisha majeshi ya Jumuiya hiyo katika Afghanistan baada ya mwaka 2014.

https://p.dw.com/p/1Aenh
Katibu mkuu wa Nato Rasmussen na rais wa Afghanistan Karzai
Katibu mkuu wa Nato Rasmussen na rais wa Afghanistan KarzaiPicha: Reuters

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeanzisha mazungumzo na Afghanistan kuhusu mpango uliopendekezwa wa kuyabakisha majeshi ya Jumuiya hiyo katika Afghanistan baada ya mwaka 2014. Hata hivyo Jumuiya hiyo imeshasema kwamba hakuna makubaliano yoyote yatakayosainiwa hadi pale patakapofikiwa maridhiano mengine tofauti kati ya Marekani na Afghanistan kuhusu suala hilo.

Rais Hamid Karzai amekuwa katika mvutano na Marekani kufuatia hatuwa yake ya kukataa kutia saini makubaliano ya kiusalama na taifa hilo kubwa duniani,makubaliano ambayo kimsingi yangewafanya maelfu ya wanajeshi wa Marekani kupelekwa Afghanistan baada ya mwaka 2014. Awali mwafaka huo unaofahamika kama BSA uliridhiwa na Karzai lakini baadae akakataa kuutia saini kitendo kilichowakasirisha wabunge na maafisa wa Marekani ambao wametishia kuyaondowa kabisa majeshi yake kutoka taifa hilo.

Polisi wa Afghanistan wanaopewa mafunzo na jeshi la Ujerumani katika´eneo la Faisabad
Polisi wa Afghanistan wanaopewa mafunzo na jeshi la Ujerumani katika´eneo la FaisabadPicha: Michael Kappeler/AFP/Getty Images

Taarifa iliyotoka wizara ya ulinzi ya Marekani kupitia msemaji wake John Kirby imeeleza kwamba Nchi hiyo pamoja na washirika wake barani Ulaya zinasisitiza mkataba huo wa kiusalama lazima usainiwe bila ya kuchelewa. Katibu mkuu wa Jumuiya ya NATO Anders Fogh Rasmussen kwa upande mwingine amefahamisha kwamba majadiliano yameanza kati ya mjumbe wa ngazi yajuu wa Jumuiya hiyo Maurits Jochems na mshauri wa masuala ya usalama wa Afghanistan Rangin Spanta.

Binafasi Rasmussen ameweka wazi kwamba anayaunga mkono mazungumzo hayo lakini pia amesema hakuna makubaliano yoyote yatakayofikiwa kati ya Jumuiya hiyo na Afghanistan hadi Karzai atakapotia saini makubaliano ya kiusalama na Marekani. Halikadhalika waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesifu hatuwa hiyo ya kuanza kwa mazungumzo,akisema ni kitendo kinachoonyesha ni kwa jinsi gani Jumuiya ya Kimataifa ilivyo na nia ya utayarifu wa kuiunga mkono na kuisaidia Afghanistan baada ya mwaka 2014.

Ujerumani kwa upande wake inazungumzia kuridhishwa na hatuwa iliyofikiwa na majeshi yake Afghanistan ambapo waziri wake mpya wa Ulinzi Ursula Von Der Leyen amesema wako makini kuona kwamba Ujerumani inakamilisha kile kilichoanzishwa katika taifa hilo.Ujerumani inapanga kuchangia wanajeshi wake 800 katika juhudi za Kimataifa za kutowa ushauri na kuwapa mafunzo wanajeshi wa Afghanistan mwishoni mwa mwaka 2014.Von Der Leyen amewatembelea (22.12.2013) wanajeshi wa Ujerumani waliokita kambi Mazar-e-Sharif .

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula Von Der Leyen akitembelea wanajeshi Mazai Sharif
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula Von Der Leyen akitembelea Mazai SharifPicha: picture-alliance/dpa

Katibu mkuu wa NATO amebainisha kwamba mazungumzo hayo yanayojadili kile kinachofahamika kama SOFA yaani Makubaliano ya hadhi ya vikosi vya NATO,baada ya mwaka 2014 ni muhimu kwa ujumbe wa kijeshi unaoongozwa na Jumuiya hiyo kwa lengo la kutowa mafunzo, ushauri na msaada kwa jeshi na polisi wa Afghanistan baada ya mwaka huo wa 2014.

Rais Hamid Karzai ambaye anatarajiwa kung'atuka madarkani baada ya uchaguzi wa mwaka ujao ameonya kwamba hatokubali kuacha jeshi la NATO kuendelea kuwepo katika ardhi ya taifa lake ikiwa jeshi hilo linadhamiria kutumia mabomu na kuuwa raia wa nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini kuondoka kabisa kwa wanajeshi wa kigeni katika nchi hiyo kutozidisha hofu na wasiwasi wa kuanguka kabisa kwa vikosi vyake ambavyo hadi sasa havijawa imara na kusababisha kurudi kwa utawala wa wanamgambo wa itikadi kali wa kundi la Taliban uliong'olewa madarakani mwaka 2001 kufuatia uvamizi wa jeshi lililoongozwa na Mareakani.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/DPA

Mhariri: Sudi Mnette