1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita dhidi ya dola la kiislamu

Admin.WagnerD28 Julai 2015

Jumuiya ya kijeshi ya Nato inaiunga mkono thabiti Uturuki katika juhudi zake za kupambana na ugaidi. Msimamo huo ulisisititizwa leo kwenye mkutano wa dharura uliofanyika mjini Brussels kutokana na maombi ya Uturuki

https://p.dw.com/p/1G6W7
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Reuters/F. Lenoir

Mabalozi wa nchi za NATO walikutana mjini Brussels wakati ambapo Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesisitiza kwamba nchi yake itayaendeleza mashambulio dhidi ya wapiganaji wa kundi linaloitwa dola la kiislamu na dhidi ya waasi wa kikurdi. Akiufungua mkutano wa mabalozi hao Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa Nato Jens Stoltenberg alisema washirika wote wamesimama katika mshikamano na Uturuki.

Katibu Mkuu wa NATO Stoltenberg ameutilia maanani mchango wa Uturuki katika harakati za kupambana na ugaidi. Katibu Mkuu wa Nato amesema ugaidi wa aina yoyote hauwezi kuvumuliwa au kuhalalishwa .Amesema mkutano wa mabalozi wa NATO umefanyika katika wakati wa kufaa.

Uturuki iliomba kufanyika kwa mkutano huo baada ya kutokea shambulio la kujitoa mhanga katika mji wa Suruc kusini mashariki mwa Uturuki ambapo watu 32 waliuawa. Kundi la waislamu wenye itikadi kali la dola la kiislamu linalaumiwa kwa shambulio hilo lililofanywa wiki iliyopita.

Marekani na Uturuki kushirikiana

Kutokana na mauaji hayo Uturuki,ilifanya mashambulio dhidi ya wapiganaji wa kikurdi na dhidi ya kundi la magaidi wanaoitwa dola la kiislamu ingawa pande mbili hizo zinapingana vikali. Marekani na Uturuki zimesema zimekubaliana kushirikiana katika harakati za kuuanzisha ukanda usio na wapiganaji wa dola la kiislamu kaskazini mwa Syria. Hata hivyo mashambulo yaliyofanywa na Uturuki dhidi ya Wakurdi yamewashangaza washirika wake wa NATO.

Mashambulio hayo yamezua swali juu ya msimamo wa serikali ya Uturuki juu ya Wakurdi-iwapo Uturuki inaweka kipaumbele katika kuudhoofisha uwezo wa Wakurdi badala ya kupambana na magaidi wa dola la kiislamu nchini Irak na Syria.

Washirika wa NATO mpaka sasa wanawazingatia Wakudri kuwa wapiganaji wenye ufanisi mkubwa wa kijeshi katika kupambana na dola la kiislamu.Wakati huo huo Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesisitiza leo kwamba nchi yake itaendeleza mashambulio na itasonga mbele. Amesema Uturuki haitarudi nyuma.

Mchakato wa amani kuendelea

Katika kadhia nyingine Uturuki imesema mchakato wa amani na wapiganaji wa Kikurdi utaweza kuendelea ikiwa ,wale ambao Uturuki inawaita magaidi wataziweka silaha zao chini na kuondoka nchini.Msemaji wa chama tawala Besir Atalay ameeleza kuwa mchakato wa amani bado haujakufa. Hapo awali Rais Erdogan alisema ni vigumu kuendelea na juhudi za amani na alilitaka Bunge kuwafutia wanasiasa, wanaowaunga mkono magaidi, kinga dhidi ya kushtakiwa.

Mwandishi:Mtullya Abdu.rtre,afp,

Mhariri:Daniel Gakuba