1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Marekani zashambulia nyumba ya kiongozi wa kundi la al-Shabaab -Somalia

Kalyango Siraj1 Mei 2008

Anadaiwa kuwa na uhusiano na mtandao wa Al -Qaida

https://p.dw.com/p/Drji
Vijana wakisomali wakiubeba mwili wa mtu mmoja alieuawa wakati wa mapigano Mogadishu,kati ya wanamgambo na majeshi ya serikali ya Somalia, Jumatatu, April 21, 2008.Mashambulizi mengi ya wapiganaji yanasemekana kufanywa na kundi la al-Shabaab .Kiongozi wa kundi hilo, Aden Hashi Ayro, ameuawa katika hujuma za ndege zinazofikiriwa kuwa za Marekani. Anahusishwa na mtandao wa Al Qaida.Picha: AP

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia linasema kuwa kiongozi mmoja wa kundi linahusishwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ameuawa pamoja na watu wengine kadhaa katika shambulio la ndege katika eneo lililoko umbali wa kilomita kama 500 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo wa Mogadishu.

Kundi hilo linasema kuwa shambulio hilo limefanywa na ndege za kijeshi za Marekani,lakini Jeshi hilo halijatoa taarifa ya kuthibitisha madai hayo.

Msemaji wa kundi la wanamgambo la al-Shabaab la nchini Somalia,amesema kuwa shambulio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo alhamisi na kumuua Aden Hashi Ayro pamoja na watu wengine saba.

Aden Hashi Ayro ni kiongozi wa kundi la wanamgambo la al-Shabaab.

Habari za hivi sasa zinasema kuwa watu ambao wamefariki wamefikia wanane.Kifo cha Aden na wengine kilitokea baada ya nyumba yake kushambuliwa na maroketi matatu,kwa mujibu wa shirika la habari la kisomali la Garowe Online.Nyumba hiyo inapatikana katika eneo la Dusamareb,linalopatikana umbali wa kilomita 500 kaskazini mwa mji mkuu wa Mogadishu.

Hii ni kwa mujibu wa walioshuhudia pamoja na vyombo vya habari kadhaa mkiwemo lile la kisomali la Garowe Online.

Wakazi wa eneo hilo wanasema kuwa waliona ndege za kijeshi za Marekani.Lakini hadi sasa hakujapatikana hakikisho rasmi kutoka jeshi la Marekani kuwa limehusika na shambulio hilo.

Wiki chache zilizopita,ndege za kijeshi za Marekani ziliwashambulia wapiganaji wa kiislamu kusini mwa nchi hiyo. Pia inalichukulia kundi la al-Shabaab kama kundi la kigaidi ambalo inadai linauhusiano na mtandao wa unaoongozwa na Osama Bin Laden la Al-Qaida.

Duru za kiusalama pamoja na za kijasusi zinasema kuwa Ayro alipata mafunzo ya mbinu za kigaidi nchini Afghanistan katika miaka ya 1990.

Taarifa zaidi kumuhusu kiongozi huyo ni kuwa alikuwa na umri wa miaka 30 na amekuwa mafichoni tangu utawala wa mahakama za kiislamu ulipong'olewa madarakani mjini Mogadishu katika mwanzo wa mwaka wa 2007.

Katika matamshi yasio ya kawaida, kamanda huyo wa kiislamu, alioekana katika mkanda wa video ambao ulitolewa Novemba,akiwahimiza wafuasi wake kuanza kuwashambulia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika waliko katika mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu.

Raia wa kawaida wa mjini Mogadishu wameteseka sana kutokana na mapigano ya kila mara kati ya waasi na vikosi vya Somalia vikisaidiwa na na majeshi ya Ethiopia.Kundi la al-Shabaab linalaumiwa kuongoza mashambulizi hayo

Kundi moja linalotetea haki za binadamu nchini humo linadai kuwa mapigano ya mjini Mogadishu, mwaka jana pekee, yalisababisha vifo vya watu takriban elf sita Unusu.

Na jana jumatano chama cha msalaba mwekundu cha kimataifa kimesema kuwa kinasikitishwa na hali mbaya ya kibinadamu ilioko nchini Somalia.