1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK:Iran yaendelea kukaidi agizo la Umoja wa Mataifa

24 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CByy

Shirika la kimataifa la mguvu za atomic limesema kuwa Iran inaendelea na mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium kwa ajili ya vinu vyake vya nuklia kinyume pamoja na kutakiwa kusitisha mpango huo na Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya siri ya shirika hilo iliyopelekwa Umoja wa Mataifa hata hivyo imesema kuwa, haifahamiki wazi ni kwa kasi gani Iran inaweza kuendelea na kazi hiyo, kwani shirika hilo halina nafasi ya kukagua shughuli hiyo.

Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yanahofu kuwa Iran kwa siri inaunda bomu la nuklia kwa kivuli cha nishati hiyo kutumika kwa matumizi ya kiraia, kitu ambacho Iran imekanusha.

Wakati huo huo Marekani imetishia kuchagiza vikwazo vipya kwa Iran, kutokana na ukaidi wake na imezitaka nchi rafiki zake barani ulaya na asia kuitenga Iran

Hayo yakiendelea hofu imetanda huko ghuba baada ya Marekani kupeleka meli mbili kubwa za kivita zikiwa na ndege kadhaa, ambapo zinafanya mazoezi.

Afisa mmoja wa juu wa kituo cha utafiti huko Ghuba, Mustafa Alani amesema kuwa hatua hiyo ya Marekani inaonekana kuwa ni ujumbe kwa Iran ya kwamba hatua za kijeshi ziko njiani.