1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria na DR Kongo zatinga nusu fainali AFCON

Iddi Ssessanga
3 Februari 2024

Nigeria na DR Kongo zimefuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika AFCON kwa ushindi dhidi ya Angola na Guinea. Sasa zinasubiria kati ya Cape Verde and Afrika Kusini, na Ivory Coast na Mali.

https://p.dw.com/p/4bzls
Kombe la mataifa ya Afrika 2024 ITimu ya taifa ya DR Kongo
DR Kongo imetinga nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu 2015.Picha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Bao la pekee la Ademola Lookman lilitosha kwa Nigeria kuishinda Angola usiku wa kuamkia leo na kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiungana nao kwa kutoka nyuma na kuishinda Guinea.

Lookman, mshambulizi wa Atalanta na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza ya chini ya umri wa miaka 21, alifunga mabao yote mawili katika ushindi wa Nigeria dhidi ya Cameroon katika hatua ya 16 bora na amefikisha matatu katika michezo miwili huku Super Eagles wakipata ushindi wao wa tatu wa 1-0 katika michuano hiyo.

Bao hilo lilipatikana dakika nne kabla ya kipindi cha mapumziko kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny, kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Moses Simon aliechukuwa pasi ya kushoto, na kumuacha Kialonda Gaspar na kuingia eneo la hatari kabla ya kurudisha mpira nyuma kwa Lookman kumaliza.

Goli hilo lilitosha kwa Nigeria kutinga nusu fainali ya 15 ya Kombe la Mataifa, ikiwa imefika hatua hiyo mara  nyingi kuliko nchi nyingine yoyote.

Kombe la Mataifa ya 2024 I Nigeria vs Angola
Mlinda mlango wa Nigeria Stanley Nwabali (katikati) akidaka mpira wakati wa mechi ya robo fainali ya AFCON kati ya Super Eagles na Angola, Februari 2, 2024 nchini Ivory Coast.Picha: Franck Fife/AFP

Mwanasoka bora wa Afrika wa mwaka Victor Osimhen alifumania nyavu ikiwa imesalia robo saa lakini jitihada zake zilikataliwa kwa kuotea na hivyo mshambuliaji huyo wa Napoli bado hajapata bao tangu sare ya ufunguzi ya Nigeria ya 1-1 na Equatorial Guinea.

Wakati huohuo Angola walipata nafasi moja ya pekee ya kusawazisha bao kabla ya dakika za lala salama, wakati Zini aliyetokea benchi alipopiga mkwaju lakini shuti lake likatoka nje ya lango.

Nigeria hivi sasa wamefikisha mechi nne mfululizo bila kufungwa bao, jambo linalothibitisha mbinu ya kocha Jose Peseiro ambayo imejikita katika kuhakikisha kwamba hawaruhusu mabao kabisaa.

"Ni timu nzuri, lakini kwa mara nyingine hatukuruhusu goli. Kwa mara nyingine tena tulifunga mara moja," Peseiro alisema.

"Ningetamani kufunga zaidi. Kwa umaliziaji bora tungeweza kufunga bao lingine moja au mawili, lakini nina furaha. Wachezaji wangu walistahili."

Nigeria inafuzu kwa hatua ya nne-bora Jumatano ijayo dhidi ya Cape Verde au Afrika Kusini katika mji wa katikati mwa Ivory Coast wa Bouake -- timu hizo zitakutana katika robo fainali baadae leo.

Angola, kwa upande wao, wanakwenda nyumbani lakini AFCON hii itakumbukwa kuwa ya mafanikio kwa Swala hao Weusi, baada ya kushinda mechi ya raundi ya mtoano kwenye michuano hiyo kwa mara ya kwanza kabisa.

Kombe la Mataifa ya Afrika 2024 I Nigeria vs Angola
Fowadi wa Nigeria Victor Osimhen, kulia, akishangilia bao lililokataliwa baada ya mapitio ya VAR.Picha: Issouf Sanogo/AFP

"Tulisema miongoni mwetu kwamba ikiwa tungefika robo-fainali basi tutajaribu kushinda mashindano hayo. Timu yoyote inayofika hapa ina matarajio hayo," alisema kocha wa Angola Mreno Pedro Goncalves.

Soma pia: Magoli 2 ya Lookman dhidi ya Kamerun yaipeleka Nigeria robo fainali

"Tunapenda kuota, lakini pia unahitaji kuwa halisi. Ukweli ni kwamba tulikuwa tunapambana na upande wenye nguvu sana wenye wachezaji wanaocheza kwa kiwango cha juu sana."

DR Kongo yazidi kupeta

Mechi ya pili ya Ijumaa ilishuhudia DR Kongo ikiilaza Guinea 3-1 mjini Abidjan kwenye Uwanja wa Olympic Ebimpe. Guinea walitinga hatua ya nane bora baada ya kushinda mechi ya mtoano ya Kombe la Mataifa kwa mara ya kwanza, na waliitangulia Kongo katikati mwa kipindi cha kwanza.

Mohamed Bayo aliangushwa kwenye eneo la kisanduku na alitia wavuni mkwaju wake wa penati kwa bao lake la tatu la michuano hiyo.

Hata hivyo, nahodha wa Leopards Chancel Mbemba alifunga bao maridadi la kusawazisha kabla ya nusu ya kwanza kumalizika, na Wakongo hao wakachua uongozi kwa penalti ya pekee katika dakika ya 65.

Silas Katompa Mvumpa aliangushwa kwenye eneo la hatari na Julian Jeanvier, na Yoane Wissa wa Brentford hakufanya makosa katika eneo la hatari.

Kombe la Mataifa ya Afrika 2024 I DR Kongo
The Leopards wametinga hatua ya Nusu fainali licha ya kutoshinda meshi hata moja katika duru ya makundi.Picha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

DR Kongo kisha wakajikatia tiketi ya nusu fainali ya kwanza tangu 2015 kutokana na mpira wa adhabu uliopigwa na beki wa pembeni wa Besiktas, Arthur Masuaku kutoka upande wa kushoto.

Soma pia: Bouchra Karboubi: Mwamuzi dhidi ya vikwazo vyote

Walifuzu kwa hatau ya mtoano licha ya kutoka sare katika mechi zote tatu, kisha wakaishinda Misri kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya 16 bora.

"Tuna furaha sana kwa sababu tulikuwa tumetoka sare katika michezo yetu yote hadi sasa na tulichagua wakati mzuri wa kupata ushindi," alisema kocha wao Mfaransa Sebastien Desabre.

DR Congo sasa wanasalia Abidjan kwa nusu fainali dhidi ya Mali au wenyeji Ivory Coast, ambao watakutana katika hatua ya nane bora leo Jumamosi.