1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya visa vya Ebola havigunduliwi DRC

Yusra Buwayhid
3 Agosti 2019

Mratibu mpya wa kukabiliana na Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema nusu ya visa vya mripuko huo mbaya huwa havigunduliwi. Wataalam wa afya wanaogopa ugonjwa huo, unaweza kuenea hadi Rwanda.

https://p.dw.com/p/3NH4l
BG Ebola-Ausbruch im Kongo
Picha: picture-alliance/dpa/J. Delay

Takriban nusu ya kesi za Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hazigunduliwi, mratibu mpya wa juhudi za kupambana na Ebola, Jean-Jacques Muyembe, amewaambia waandishi wa habari.

"Tukiendelea namna hii, mripuko huu unaweza kudumu kwa miaka miwili hata mitatu," Muyembe amesema Ijumaa katika mkutano ya waandishi habari Goma, mji ulio mashariki ya Kongo karibu na mpaka wa Rwanda. Ameongeza kwamba lengo ni kuwa na kiwango cha asilimia 80 cha kugundua ugonjwa huo ili kuimarisha mchakato wa uchunguzi.

Muyembe ametoa matamshi hayo siku moja baada ya serikali ya Kongo kujaribu kuudhibiti ugonjwa huo kufuatia mchimba migodi mmoja mwenye familia kubwa kuwaambukiza watu kadhaa mjini Goma kabla na kufariki kutokana na homa. Muyembe amesema mke wa mtu huyo aliyefariki na mtoto wao wa mwaka mmoja wamegunduliwa na maambukizi ya Ebola pia lakini wnaaendelea vizuri na wanapewa huduma za matibabu.

Ni kisa cha nne kuthibitishwa Goma, mji ulioko kilomita 350 kusini mwa eneo ambako ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza. Wataalamu wa afya wanahofia ongezeko la maambukizi ya Ebola mjini Goma linaweza kusababisha ugonjwa huo kusamaa nchi jirani ya Rwanda.

BG Ebola-Ausbruch im Kongo
Mwananmke akipimwa joto la mwili Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Soma zaidi: Mwaka mmoja wa Ebola Kaskazini Mashariki mwa DRC

Watu wapatao 1,8000 wamefariki dunia kutokana a ugonjwa huo hatari tangu ulipozuka mwaka uliopita -  ukiwa ni mlipuko wa pili mbaya wa Ebola kurekodiwa. Kati ya mwaka 2013 na 2016 watu wapatao 28,000 waliambukizwa Ebola Afrika Magharibi. Watu 11,300 wanakadiriwa kuwa walifariki nchini Liberia, Guinea na Sierra Leone.

Chanjo mpya Uganda

Wakati huo huo, watafiti nchini Uganda wamezindua majaribio makubwa zaidi ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola ambayo inatarajiwa kupelekwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iliyokumbwa na maradhi hayo hatari.

Majaribio hayo ya chanjo kutoka kampuni ya madawa ya Janssen yatajumuisha zaidi ya watu 800 na yanaungwa mkono na shirika la madaktari wasio na mipaka pamoja na shule ya afya na magonjwa ya kitropiki ya mjini London.

Pontiano Kaleeb ambaye anaongoza majarabio hayo amesema anasikitika kwamba chanjo ya Janssen haijafikishwa hadi sasa nchini DRC ambapo zaidi ya watu 1,800 wamekufa tangu maradhi ya Ebola yalipozuka mwaka uliopita.

Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzuka kwa ugonjwa huo, zaidi ya watu 180,000 wamepatiwa chanjo ya majaribio ya Merck ambayo imeonesha mafanikio lakini waatalamu wana wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chanjo hiyo wakati virusi vya Ebola vikisambaa hivi sasa kwenye mji wa Goma.

Chanzo: (ap,afp,dw)