1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OIC yakutana Istanbul kulaani mauaji ya Wapalestina

Iddi Ssessanga
18 Mei 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameitisha kwa mara ya pili katika kipindi cha nusu mwaka, mkutano wa kilele wa jumuiya ya mataifa ya Kiislamu OIC, akitafuta kuonyesha mshikamano na Wapalestina na kuilaani Israel.

https://p.dw.com/p/2xw07
Türkei, Präsident Joko Widodo in OIC Istanbul
Picha: Laily Rachev/Biro Pers Setpres

Erdogan ameitikia kwa hasira kubwa mauaji hayo ya Wapalestina kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu, na kuituhumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari na kuwa taifa linaloendeshwa kwa misingi ya ubaguzi na utengano - yaani apartheid.

Matamshi yake yaliibua mgogoro wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Israel, na Erdogan ameitisha maandamano makubwa yaliyotarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya watu siku ya Ijumaa kupinga matendo ya Israel dhidi ya Wapalestina.

"Kunyamazia vitendo haramu vya Israel, vinavyokiuka maadili ya kiutu, na haki kunamaanisha kufungua mlango wa hatari kubwa. Jumuiya ya kimataifa haijafanya chochote kuhusiana na matukio ya Palestina. Katika matukio yote haya, Umoja wa Mataifa umemalizika.

Umechoka na kuporomoka. Ikiwa matendo ya Israel yataruhusiwa, dunia itatumbukia haraka katika machafuko yanayohodhiwa na wizi. Inamaanisha mwisho wa wanadamu ikiwa mwenye nguvu anapata kila anachokitaka," alisema Erdogan siku ya Jumatano.

Mkutano wa pili katika nusu mwaka

Türkei Sondergipfel der Organisation für Islamische Kooperation (OIC)
Rais Erdogan ameyataja mauaji ya Wapalestina siku ya Jumatatu kuwa ya kimbari.Picha: Reuters/K. Ozer

Tayari Erdogan aliitisha mkutano usio wa kawaida ya jumuiya ya nchi za Kiislamu, OIC Desemba mwaka uliopita, kulaani uamuzi wa Rais Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Ameapa kuwa mkutano wa leo unapaswa kutuma ujumbe mzito kwa ulimwengu kuhusiana na namna Israel inavyowatendea Wapalestina.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo mjini Istabul Ijumaa, waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, ameyataka mataifa ya Kiislamu kwa pamoja, kuhakikisha kuwa mataifa mengine hayafuati nyayo za Marekani na kufungua balozi zao za Israel katika mji wa Jerusalem.

"Katika tangazo la mwisho, tutasisitiza hadhi ya suala la Palestina kwa jamii yetu, na kwamba hatutoruhusu kubadilishwa kwa hadhi ya mji huo wa kihistoria," amesema Cavusglu na kuongeza kuwa, " laazima tuyazuwie mataifa mengine dhidi ya kufuata mfano wa Marekani.

Mgawanyiko wa mataifa ya kanda

Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwenye mkutano wa 2017, mivutano kati ya wanachama muhimu wa OIC -- hasa kati ya dola lenye nguvu la Kisunni Saudi Arabia na Iran inayofuta itikadi ya Kishia -- inaweza kuzuwia kupitishwa kwa maazimio yoyote zaidi ya maneno makali.

Riyadh, ambao inaonekana kulegeza msimamo wake dhidi ya Israel mnamo wakati ushawishi wa mrithi wa kiti cha ufalme mwenye nguvu Mohammad bin Salman unazidi kuimarika -- pamoja na washirika wake wanahofia kutengwa na Marekani kwa kuchukuwa hatua kali dhidi ya Israel.

Türkei Sondergipfel der Organisation für Islamische Kooperation (OIC)
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut CavusogluPicha: Reuters/A.H. Yaman

Baada ya kutangaza nia yake kuitisha mkutano huo siku ya Jumatatu, Erdogan ameweza kuja na orodha nzuri tu ya wahudhuriaji, wakiwemo Mfalme wa Jordan Abdullah II, Mfalme wa Kuwait Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Sabah na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, mshirika mkuu wa Uturuki katika kanda ya Ghuba. Saudi Arabia na Misri zinawakilishwa na mawaziri wake wa mambo ya nje, Adel Al-Jubeir na Sameh Shoukry.

UN yataka uchunguzi huru

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al-Hussein pia amelaani nguvu iliotumiwa na Waisrael katika maandamano hayo, wakati akizungumza katika kikao maalumu cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, na kuunga mkono wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa katika mkasa huo.

Lakini balozi wa Israel Aviva Raz Shechter, amaeutaja wito huo kuwa kurejea kwa baraza hilo katika chuki dhidi ya Israel, na kuogneza kuwa kuanzishwa uchunguzi huru hakutobadili chcochote.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, rtre

Mhariri: Grace Patricia Kabogo