1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazohusika na suala la Mashariki ya kati zakutana Jerusalem.

Mohammed Abdul-Rahman26 Juni 2007

Ni mara ya kwanza tangu chama cha wapalestina cha Hamas kulitwaa na kulidhibiti eneo la Gaza, kukiwa na uvumi unaozidi kwamba , wajumbe hao huenda wakamteuwa Waziri mkuu wa Uingereza anayeacha madaraka rasmi kesho (jumatano)Tony Blair, kuwa mjumbe wao maalum.

https://p.dw.com/p/CHCB
Tony Blair anayetarajiwa kuteuliwa kuwa mjumbe maalum kuhusu Mashariki ya kati.
Tony Blair anayetarajiwa kuteuliwa kuwa mjumbe maalum kuhusu Mashariki ya kati.Picha: AP

Waakilishi maalum wa pande hizo nne zinazohusika na mashariki ya kati –Umoja wa Ulaya, Urusi, Umoja wa mataifa na Marekani-walikua na mazungumzo kwenye ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jerusalem, siku moja baada ya mutano wa kilele wa eneo hilo uliofanyika jana mjini Sharm el Sheijkh-Misri kati ya Rais Mubarak wa Misri, Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert , Mfalme Abdullah wa Jordan na Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas.

Mjumbe wa Umoja wa ulaya Marc Otte, mwenzake wa Urusi Sergei Yakovlev, Michael Williams wa Umoja wa mataifa na Waziri mdogo wa Marekani David Welch walikutana faragha kwa zaidi ya saa mbili , kabla ya kuondoka bila ya kutoa tamko lolite.

Msemaji wa umoja wa mataifa Brenden Varma alisema tu “ Mkutano sasa umekwisha Umemalizika punde hivi lakini bahati mbaya hakuna taarifa yoyote.”

Jumuiya ya kimataifa imeelekeza nguvu zake nyuma ya Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas , tangu majeshi yake yaliposhindwa huko Gaza na wanamgambo wa Hamas siku 11 zilizopita, baada ya mapigano makali ya risasi yaliowauwa zaidi ya wapalestina 110.

Msemaji rasmi wa kundi hilo la pande nne kwa upande mwengine, alikataa kuingizwa katika mjadala juu ya uwezekano wa awazieri mkuu wa Uingereza Tony Blair kuteuliwa kuwa mjumbe maalum wa kundi hilo. Bw Blair anaacha madaraka kesho akimkabidhi wadhifa wa Waziri mkuu waziri wake wa fedha Gordon Brown ambaye tayari juzi alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama tarala cha Leba´, akimrithi Blair.

Gazeti linaloheshimika mno nchini Uingereza Financial Times limeripoti kwamba kundi hilo la pande nne kuhusu mashariki ya kati, litakubaliana leo juu ya uteuzi wa Blair. Lakini binafsi Bw Blair hakuthibitisha wala kukanusha habari hizo, licha ya kusema kwamba yuko tayari kusaidia kuleta suluhisho katika mzozo wa Israel na Palestina, akiongeza kwamba “ kila mtu mwenye kuzpenda amani anajua kwamba suluhisho la kudumu la mzozo wa Israel na Palestina ni muhimu .”

Marekani imesema inataka kulipa upeo mpana zaidi jukumu la mjumbe maalum wa kundi hilo la pande nne, lakini aliyekua akishikilia jukumu hilo hapo kabla, rais wa zamani wa Benki ya dunia James Wolfensohn aliacha kazi hiyo mwezi Mei mwaka jana, akitaja kufadhahishwa kwake na kasi ya mwenendo wa kusaka amani kati ya Israel na Palestina.

Ingawa uteuzi wa Bw Blair umekaribishwa na Israel, hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanaashiria kwamba umepokewa kwa shingo upande katika Ulimwengu wakiarabu, kutokana na mchango wa Uingereza katika uvamizi wa 2003 nchini Irak ulioongozwa na Marekani, pamoja na hatua yake ya kuunga mkono vita vya Israel nchini Lebanon mwaka jana.