1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aelekea Bahrain katika kongamano la kidini

Daniel Gakuba
3 Novemba 2022

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amekwenda nchini Bahrain kushiriki katika mkutano wa dini mbali mbali, unaohimiza utangamano kati ya nchi za mashariki na za magharibi.

https://p.dw.com/p/4J0Cr
Vatikanstaat Papst Franziskus, Generalaudienz
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa FrancisPicha: Massimo Valicchia/NurPhoto/picture alliance

Papa Francis anatarajiwa kuwasili nchini Bahrain mchana wa leo Alhamisi, hii ikiwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani katika taifa hilo la ghuba linaloongozwa na mfalme. Lengo kuu la ziara yake ni kukutana na viongozi wa kiislamu, na Papa atatoa hotuba baada ya kongamano hilo kesho Ijumaa.

Soma zaidi: Papa asema 'mauaji ya kimbari' yalifanyika Canada

Kabla ya kuondoka, Papa Francis aliomba sala za kila mmoja, ili mikutano yake na viongozi wa dini nyingine izae matunda na iwe fursa ya kuendeleza amani na udugu.

Ägypten Papst Franziskus in Kairo | mit Imam Ahmed al-Tayeb
Papa Francis (kulia) akisalimiana na Imam Mkuu wa Al-Azhar Ahmed al-TayebPicha: Reuters/M. Abd El-Ghany

''Itakuwa safari chini ya kauli mbiu ya mjadala. Kimsingi nitashiriki katika kongamano ambalo mada yake ni mahitaji yasiyoepukika, ya mashariki na magharibi kuja kwa ajili ya utangamano wa wanadamu,'' amesema Papa Francis.

Si mara ya kwanza Papa Francis kuizuru Ghuba ya Uarabu

Hii ni mara ya pili kwa Francis kuitembelea nchi ya Ghuba ya Uarabu, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2019 katika safari ya kihistoria nchini Abu Dhabi, ambako alikutana na Imam wa madhehebu ya Sunia Sheikh Ahmed al-Tayeb, ambaye pia ni Imam Mkuu wa Al-Azhar, kituo kikuu cha mafunzo ya kisuni kilichoko mjini Cairo, Misri.

Soma zaidi: Papa Francis afanya maombi ya uponyaji kwa ukoloni 'mbaya' nchini Canada

Mbali na viongozi wa Kiislamu, Papa Francis anatarajiwa kukutana pia na Wakatoliki wapatao 80,000 waishio nchini Bahrain, wengi wao wakiwa wafanyakazi wahamiaji kutoka Ufilipino na India.

Papst Franziskus zu Besuch in Abu Dhabi
Alipoitembelea Abu Dhabi mwaka 2019, Papa Francis alikutana na Wakristo waishio katika nchi hiyo.Picha: Reuters/Vatican Media

Bahrain ndipo lilipo kanisa la kwanza la Kikatoliki katika Ghuba ya Uarabu, la Moyo Mtakatifu lililojengwa mwaka 1939. Ni nchini humo pia ambako limejengwa kanisa kubwa zaidi katika ukanda huo, Katedrali ya Mama Yetu wa Arabia lenye uwezo wa kuwapokea waumini 2,300.

Shukrani kwa mfalme

Papa Francis atayetembelea makanisa hayo mawili, akitarajiwa kutoa shukrani zake kwa mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa al-Khalifa, kwa uvumilivu unaofanywa na serikali yake kwa waumini wa Kikristo, hususan ikilinganishwa taifa jirani la Saudi Arabia, ambako Wakristu hawaruhusiwi kufanya ibada hadharani.

Soma zaidi: Papa Francis akanusha kuwa anapanga kujiuzulu hivi karibuni

Hata hivyo, wakati Bahrain ikisifiwa kuwapa uhuru Wakristo, watetezi wa haki za binadamu wanaikosoa serikali yake inayoongozwa na Wasuni walio wachache, kuwabagua Washia ambao ndio wengi nchini humo.

Mashirika hayo yamemtaka Papa Francis kuitumia ziara yake kuiomba Bahrain ifute adhabu ya kifo, na iache ukandamizaji wake wa kisiasa.

-ape,dpae