1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo katika eneo la Nagorno-Karbakh wapamba moto

Tatu Karema
30 Septemba 2020

Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashiyan amezungumza na rais wa Iran Hassan Rouhani kwa njia ya simu kuhusu mzozo katika eneo la Nagorno-Karbakh-. Rouhani ameelezea wasiwasi kuhusu ghasia katika eneo hilo

https://p.dw.com/p/3jDzB
Aserbaidschan Konflikt um Berg-Karabach
Picha: Defence Ministry of Azerbaijan/Reuters

Iran inashiriki mpaka wa pamoja na Armenia na Azerbaijan ambazo vikosi vyake vimehusika katika mapigano mapya yanayohusu mzozo wa eneo la Azerbaijan lililojitenga la Nagorny Karabakh linalosimamiwa na raia wa Armenia.

Viongozi hao wawili pia wamezungumza kuhusu kuhusika kwa Uturuki katika mzozo huo madai yaliokanushwa na Azerbaijan ambayo ni mshirika wa karibu wa nchi hiyo. Siku ya Jumatatu, rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alisema kuwa lazima Azerbaijan ijitetee na kwamba Uturuki itaisaidia kwa namna yoyote ile.

Hii leo rais wa Ufaransa Emmanuel Macro alituhumu kile alichokitaja kuwa matamashi ya kiholela na hatari kutoka kwa Uturuki inayoiunga mkono Azerbaijan katika juhudi zake za kulitwaa eneo hilo lililojitenga la Nagorny Karabakh.

Macro ameongeza kusema anasisitiza wito thabiti na wazi wa kusitisha mapigano bila masharti ambao Ufaransa ilituma Jumapili asubuhi na kwamba amezungumza na Waziri Mkuu Waarmenia Nikol Pashinian na Rais wa Azabaijani Ilham Aliyev kwa njia ya uwazi. Macro ameongeza kuwa aliuliza haswa kwa sababu imethibitishwa kuwa kumekuwa na ufyatuaji risasi unaokuja kutoka Azabaijani na kwamba mashambulizi hayo yanapaswa kusitishwa mara moja.

Libanon Beirut Pressekonferenz Emmanuel Macron
Emmanuel Macron- Rais wa UfaransaPicha: picture-alliance/AP Images/G. Fuentes

Lakini Uturuki imejibu kwa kumtuhumu Macron kwa kuunga mkono hatua ya Armenia ya ''kulikalia'' eneo hilo ambapo mapigano makali yamekuwa yakiendelea tangu siku ya Jumapili. Macron ameongeza kusema kuwa Ufaransa bado ina wasiwasi mkubwa kuhusu matamshi ya uchochezi ya Uturuki katika  masaa machache yaliopita ambayo yanaoondoa vizuwizi vyovyote kwa upande wa Azerbaijan katika kile kitakachokuwa kinyang'anyiro cha eneo la Kaskazini la Karabakh.

Uturuki inaichukulia Azerbaijan taifa lililo na idadi kubwa ya waislamu wa madhehebu ya Kishia kuwa mshirika wake wa karibu na taifa la Armenia lililo na idadi kubwa ya wakristo kuwa hasimu wake wa kihistoria.

Mapigano yamekuwa yakiendelea kati ya vikosi vya Armenia na Azerbaijan kwa siku ya nne leo katika mzozo mkubwa zaidi katika muda wa miongo kadhaa ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu na kujeruhiwa kwa wengine wengi. Wizara ya ulinzi ya Azerbaijan imesema kuwa vikosi vya Armenia vilianza kushambulia mji wa Tartar leo asubuhi na kuharibu miundo mbinu pamoja na kuwajeruhi watu huku maafisa wa jeshi la Armenia wakiripoti kuwa vikosi vya Azerbaijan vilikuwa vikilenga kwa mabomu vituo vya jeshi la Nagorno-Karabakh Kaskazini mwa eneo hilo lililoghubikwa na vita.