1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kiir kukutana na Machar mjini Khartoum

Josephat Charo
25 Juni 2018

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amewasili mjini Khartoum kukutana na hasimu wake Riek Machar kwa duru mpya ya mazungumzo leo.(25.06.2018) Viongozi hao wanakutana katika hatua mpya ya kutafuta amani Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/30DOw
Äthiopien Friedensgespräche in Addis Abbea | Salva Kiir & Riek Machar
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Ayene

Rais wa Sudan, Omar Hassa al Bashir, atakuwa mwenyeji wa duru ya pili ya mazungumzo kati ya mahasimu hao wawili wakubwa, yanayolenga kuvifikisha mwisho vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vilivyodumu kwa muda wa miaka minne na nusu. Duru ya kwanza ya mazungumzo iliyosimamiwa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed mjini Addis Ababa Alhamisi iliyopita, haikufua dafu katika kuleta mapatano.

Viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wameanzisha juhudi mpya kuhakikisha amani inapatikana Sudan Kusini, ambako pande zinazohasimiana zinakabiliwa na tarehe ya mwisho kuepuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Mnamo mwezi Mei mwaka huu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilizipa pande zinazohasimiana muda wa mwezi mmoja kuafikia makubaliano ya amani vinginevyo zikabiliwe na vikwazo.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Sudan, Al-Dierdiry Ahmed, alisema katika duru hii ya pili ya mazungumzo wanatafuta kuuvunja mkwamo uliopo kuhusiana na suala hili nyeti na gumu. Mkutano kati ya rais Kiir na Machar utakuwa wa kwanza mjini Khartoum tangu mapigano yalipozuka Sudan Kusini, na unafanyika baada ya viongozi hao kukutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza mjini Addis Ababa baada ya kipindi cha karibu miaka miwili.

Matumaini ya kupatikana muafaka ni madogo

Wachambuzi wanasema hakuna matumaini makubwa ya kupatikana suluhu la mzozo wa Sudan Kusini katika mazungumzo ya mjini Khartoum, lakini ni ishara ya kutia moyo kwamba viongozi hao wanakutana.

Sudan 5. Jahrestag Friedensabkommen
Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, katikati, na rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, kushotoPicha: picture-alliance/dpa/T. Mckulka

Bobby Mkangi, mchambuzi wa masuala ya siasa na mwanasheria nchini Kenya aliyehusika katika mchakato wa kuaiandika katiba ya Sudan Kusini alisema, "Kwa sababu ya ule mkutano wa wiki iliyopita uliotibuka, linalotazamiwa na kutegemewa pakubwa kwa leo pengine ni mazungumzo ya kuleta upatanishi yataweza kuendelea. Wataweza kuwa na muafaka ambao utakubalika na pande zote utakaosaidia na kurahisisha kuendeleza haya mazungumzo."

Mkangi aidha alisema "cha busara ni haya mazungumzo yazidi kuendelea hata kama mikutano inaitishwa, mara nyingine inatibuka. Ni kuwe na ile taswira kwamba hata kama kuna mikinzano, kungali na ule muafaka, makubaliano kwamba mazungumzo yataendelea."

Mazumgunzo ya mjini Khartoum yanafanyika baada ya serikali ya Sudan Kusini kutangaza imechoshwa na haimtaki Machar, hivyo kufuta kabisa matumaini ya kupatikana muafaka mjini Addis Ababa. Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Michael Makuei, alisema siku ya Ijumaa na hapa tunanukuu "Kama watu wa Sudan Kusini, sio rais pekee, tunasema imetosha." mwisho wa kumnukuu.

Makuei aidha alipinga kuwepo Machar katika serikali yoyote ya mpito, lakini hakufutulia mbali uwezekano wa kujumuishwa viongozi wengine wa waasi. Kauli yake inaonesha uhasama wa kibinafsi uliopo kati ya Kiir na Machar, ambao umejikita katika chimbuko la mzozo wa Sudan Kusini, ni mkubwa kama ilivyokuwa awali.

Kenya inatarajiwa kuandaa duru nyingine ya mazungumzo kati ya rais Kiir na Machar katika wiki zijazo.

Vita nchini Sudan Kusini vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimu watu kiasi milioni nne kuyakimbia makazi yao. Vita hivyo vilizuka baada ya rais Salva Kiir kukosana na makamu wake Riek Machar mnamo Desemba 2013, na hivyo kuyazika matumaini makubwa yaliyoandama na uhuru wa Sudan Kusini kutoka kwa Sudan, miaka miwili kabla. Kiir alimtuhumu Machar kwa kupanga njama ya kumpindua, hatua ambayo ilisababisha mapigano kati ya pande mbili za viongozi hao yaliyochochewa na chuki ya kikabila.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/ape

Mhariri: Iddi Sessanga