1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia: Kenya itasalia kuwa ndugu kwa Tanzania

Shisia Wasilwa
5 Mei 2021

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo amehutubia katika kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa la Kenya na ameahidi kuwa atahakikisha Kenya inasalia kuwa ndugu, mshirika wa kimkakati na mbia.

https://p.dw.com/p/3t0Ia
Tansania Daressalam| Amtseinführung neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AFP/Getty Images

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Jumatano alihutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa la Kenya na kuahidi atahakikisha Kenya inasalia kuwa ndugu, mshirika wa kimkakati na mbia. Rais Samia ameweka historia kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa kike ulimwenguni kuhutubia katika kikao cha pamoja cha Bunge la Kenya.

Saa tisa kasorobo, Wabunge 112 waliketi kumsikiza Rais Samia Suluhu Hassan, 88 kutoka bunge la taifa na 28 kutoka bunge la seneti huku kila mmoja akiwa amevalia barakoa. Idadi hiyo ndogo ikizingatiwa kulingana na juhudi za kukabiliana na virusi vya corona, hata hivyo bunge la pamoja lina wabunge 416.

Uhusiano wa Kenya na Tanzania si wa kijiografia

Rais huyo wa Tanzania alichukua muda wa saa moja kuelezea ndoto za kutimiza mikataba waliyosaini na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Samia alibainisha kuwa alipokea mialiko mingi kutoka mataifa mengi ila aliamua kufika Kenya kwenye ziara yake rasmi tangu alipochukua wadhfa wa kuwa rais. Ziara yake nchini Uganda akielezea kuwa ilikuwa yenye sababu maalum ya kusaini mkataba.

Watanzania wazungumzia mgongano kati ya rais Samia na katibu mkuu

Samia amefafanua kuwa uhusiano wa Kenya na Tanzania si tu wa kijiografia, lakini ni wa kidamu kwani mipakani kuna makabila mengi yanayozungumza lugha moja.

Mataifa hayo mawili yana uhusiano wa miaka 56. Aidha amewaomba wawekezaji kutoka Kenya kuwekeza kwa wingi katika taifa la Tanzania, huku akiwataka wabunge kupiga msasa sheria zozote ambazo huenda zikaleta vikwazo vya kufanya biashara mipakani.

Vyombo vya usalama Kenya na Tanzania vishirikiane kumaliza uhalifu

Rais Samia ameelezea kuwa Kenya na Tanzania zina fursa nyingi za kuboresha uhusiano wake na kuinuana kama vile utalii, ikizingatiwa kuwa ikolojia za mataifa hayo zinafanana.

Aidha amevitaka vyombo vya usalama vya mataifa hayo, kushirikiana kuvunja mitandao ya uhalifu na ugaidi ili kuweka mazingira yenye amani na usalama. Mapema Rais Samia na Rais Kenyatta walikutana na baraza la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania.

Tanzania Dar es Sallam Jakaya Kikwete ehemaliger Präsident von Tanzania
Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete aliwahi kulihutubia bunge la Kenya piaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Punde tu Rais Samia alipokamilisha hotuba yake, mawingu yalitanda na mvua kunyesha, huku akikamilisha ziara yake ya siku mbili. Rais Samia anakuwa kiongozi wa tatu wa kigeni kulihutubia bunge la pamoja na wa pili kufanya hivyo kutoka Tanzania.

Wengine ambao wamewahi kulihutubia bunge hilo ni pamoja na Rais wa zamani Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2015 na Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan mwaka 2013.