1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkouzy Afrika

27 Julai 2007

rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa anaezuru sasa Senegal amechambua sera za nchi yake kuelekea Afrika.Amewataka waafrika kuweka upande ukoloni na kuangalia mbele.

https://p.dw.com/p/CB2Q

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, akiwa katika ziara yake ya kwanza barani Afrika tangu kuwa rais,ametoa sura ya ushirika inaopanga Ufaransa kuwa nao na bara la Afrika.Akiwa katika kituo chake cha pili cha ziara hii-Senegal,rais Sarkozy amelitaka bara la Afrika kuacha kuegemea mno enzi iliopita ya ukoloni na ijitolee kuheshimu utawala bora.

Alipendekeza kile alichokiita “Eurafrica”-ushirika baina ya Ulaya na Afrika ili kupambana na athari mbaya za utandawazi na kuhimiza maendeleo.

Katika hotuba yake kwenye chuo kikuu cha Dakar,rais wa Ufaransa alikiri athari mbovu zilizotokana na ukoloni hatahivyo, alisema ukoloni si chanzo cha maovu yote yaliozuka afrika miaka 50 baadae.

Rais Sarkozy,anaefahamika kwa msimamo wake mkali juu ya uhamiaji-sera ambazo zimemfanya asipendeze machoni mwa waafrika wengi, amelitaka bara la afrika kujitwika dhamana ya kukabiliana na rushua na vita visivyokwisha barani humo.Akasema na ninamnukulu,

“Mnataka aina nyengine ya utandawazi-utakaokuwa na ubinadamu zaidi,haki zaidi na kanuni zaidi.Ufaransa pia yataka hivyo.” Alisema rais Sarkozy.Akaongeza, “Mkiamua kufuata demokrasia,uhuru,haki na sheria,basi Ufaransa iko upande wenu.”

Rais wa Ufaransa ambae nchi yake iko nyuma wakati huu katika kujipatia soko la Afrika na mikataba ya mali-asili ukilinganisha na wapinzani wake wapya barani humo-China na India, aliwaonya waafrika kuchukua hadhari wasianguke mateka.

Kile Ufaransa itakacho Afrika, aliongeza rais Sarkozy, ni maendeleo ya pamoja,kile Ufaransa itakacgo Afrika ni kuiona inajiandaa kwa kuanza kwa “Eurafrica”-usuhuba kati ya Ulaya na Afrika –hatima ya pamoja inayoyasubiri mabara haya mawili.

Hotuba ya rais Sarkozy,iliotangulia yale mapatano yaliopelekea kuachwa huru kwa wale wauguzi wa kibulgaria nchini Libya wiki hii,imeonekana na baadhi ya wanabalozi ni kufungua pazia la sera mpya za Ufaransa kuelekea Afrika.

Wanafunzi wengi waliosikiliza hotuba ya Sarkozy walikasirishwa wakidai ilichukua mlio wa kuwafunza waafrika nini cha kufanya .Ilisikika kana kwamba akitaka kuwafunza waafrika historia.

Rais Sarkozy, alikwepa kijanja kabisa kulizungumzia swali nyeti la uhamiaji.Maalfu ya wasenegali hujasiri kufa kila mwaka baharini wakielekea visiwa vya Canary katika marekebu ili kutafuta maisha mema.

Sarkozy alisema inachotaka Ufaransa ni kutunga pamopja sera ya uhamiaji na Afrika; ili waafrika waweze kukaribishwa Ufaransa na Ulaya kwa heshima na taadhima.Akawataka wale waafrika waliohamia Ufaransa kurejea Afrika kutoa ujuzi wao mpya waliojipatia.

Kuchaguliwa kwa Sarkozy kama rais wa Ufaransa, kulitazamiwa kuleta mabadiliko makubwa katika uhusiano kati ya Paris na makoloni yake ya zamani na hasa kuachana na mtindo wa Ufaransa wa kun’gangania kuwabakisha madarakani viongozi wa kiafrika bila kujali wanakanyaga demokrasia au la.

Ufaransa na Senegal, zimetiliana pia saini makubaliano ya kukuza raslimali za Ufaransa nchini Senegal kutokana na mashindano yanayozidi na dola nyengine kama vile za kiarabu,India na China lakini pia Marekani.

Ziara ya rais Sarkozy barani Afrika, ilianzia Libya na kutoka Senegal anaelekea Gabon-tajiri kwa mafuta .Huko atakuwa na mazungumzo na rais wa muda mrefu Omar Bongo baadae hii leo.