1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maiti kutambuliwa kwa msaada wa Ujerumani

Josephat Charo
8 Aprili 2019

Mauaji hayo yalianza Aprili saba mwaka 1994, siku moja baada ya ndege iliyokuwa imembaba rais wa Rwanda wakati huo Juvenal Habyarima na rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira, kudunguliwa kabla kutua Kigali.

https://p.dw.com/p/3GROh
Ruanda 25. Jahrestag Völkermord | Zeremonie in Kigali
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Gazeti la die Tageszeitung ambalo wiki hii liliandika juu ya kutimia miaka 25 tangu mauaji ya halaiki ya Rwanda. Mauaji hayo yalianza Aprili saba mwaka 1994, siku moja baada ya ndege iliyokuwa imembaba rais wa Rwanda wakati huo Juvenal Habyarima na rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira, kudunguliwa wakati ilipojiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa mjini Kigali, na kuua kila mtu aliyekuwamo. Gazeti hilo lilikuwa na kichwa cha habari "Kufuata nyayo za mauaji ya halaiki". Miaka 25 baada ya mauaji bado kuna miili 800 katika madarasa na mabweni ya shule ya zamani ya Murambi, mingi ikiwa ya watoto. Maiti hizo zisizojulikana ni za akina nani ni ushahidi wa kinyama wa yale yaliyotokea. Sasa maiti hizo zitatambuliwa, kupitia msaada wa Ujerumani.

Harufu ya maiti zilizooza bado imetanda katika anga miaka 25 baada ya mauaji ya halaiki. Makumbusho hayo ya mauaji yanayopatikana kusini magharibi mwa Rwanda bado ni mojawapo ya maeneo ya kuhuzunisha ya kumbukumbu katika taifa hilo dogo katikati mwa bara la Afrika, ambako zaidi ya watu milioni moja waliuliwa, wengi wao Watutsi. Murambi ni zaidi ya makumbusho. Ni mahala pekee ambapo maiti zimehifadhiwa, kipengee muhimu cha sera ya Rwanda kuhusu kuyakumbuka mauaji hayo.

Mwaka mmoja wa Abiy Ahmed madarakani

Gazeti la Neues Deutschland wiki hii limeandika juu ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kukamilisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani tarehe mbili mwezi wa Aprili mwaka uliopita. "Waziri Mkuu wa Ethiopia asiyetabirika," ndivyo lilivyoandika gazeti hilo katika kichwa chake cha habari. Mhariri aliandika kuwa Abiy Ahmed ameubadili mkondo wa mambo nchini Ethiopia na kuleta upepo wa mageuzi katika eneo zima la pembe ya Afrika.

Ruanda 25. Jahrestag Völkermord | Zeremonie in Kigali | Juncker & Ahmed & Michel
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, wa pili kutoka kushoto kwenye msitari wa nyuma, akihudhuria kumbukumbu za miaka 25 za mauaji ya halaiki RwandaPicha: Reuters/B. Ratner

Gazeti la Neues Deutschland lilisema tangu waziri mkuu huyo alipoingia madarakani, mambo hayako jinsi yalivyokuwa hapo kabla. Taifa hilo ambalo zamani lilikuwa likitawaliwa kwa mkono wa chuma, sasa linafungua milango yake ndani na nje.

Bouteflika ang'atuka

Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti kuhusu Abdel Aziz Bouteflika kung'atuka muhula wake utakapokamilika. Mhariri alisema Bouteflika ni mtu ambaye alikuwa Algeria yote. Alileta utulivu katika taifa lililokuwa limemezwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini baadaye nchi ikapoteza mwelekeo, mahusiano yakavurugika. Ilikuwa picha ya kusikitisha, iliyoonyeshwa na televisheni ya serikali ya Algeria Jumanne jioni. Alipokuwa ameketi kwenye kiti chake ha magurudumu, Abdelaziz Bouteflika alijitahidi kutoa barua yake ya kujiuzulu kwa mwenyekiti wa Baraza la Katiba.

Baada ya karibu miaka 20 madarakani, Bouteflika alikuwa labda na matumaini ya kumuachia kiongozi mwingine. Kwa hakika yeye alitaka kufungua msikiti mkubwa barani Afrika, uliojengwa na makampuni ya ujenzi ya Kichina mjini Algiers. Ikiwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 82 anaweza kujieleza mwenyewe na kusikia, hakuna aliyetaka kusema kwa uhakika kwa miaka sasa. Tangu Bouteflika alipopatwa na kiarusi miaka sita iliyopita, hajazungumza hadharani.

Burundi na Sudan zahamisha miji mikuu

"Afrika iko katika homa ya ujenzi". Ndivyo lilivyoandika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Mhariri alisema miji mikubwa inaandaliwa kwenye meza ya uchoraji wa ramani za majengo. Burundi na Sudan Kusini zinayahamisha makao makuu ya serikali. Wakosoaji wanalalamika kwamba matajiri pekee barani Afrika ndio wanaonufaika kutokana na uhamishaji huo. Kiongozi wa mielele" ndivyo alivyoruhusu rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuitwa tangu miezi kadhaa sasa. Imboneza yamaho. Mnamo mwezi Mei mwaka huu katiba ilibadilishwa katika taifa hilo dogo la Afrika Mashariki ili rais huyo mwenye umri wa miaka 55 aendelee kutawala mpaka mwaka 2034. Sasa mji mkuu Bujumbura ulio kando ya ziwa Tanganyika, pamoja na wakazi wake milioni 1.2, unahamishwa katika mji mdogo wa Gitega, ambako watu 30,000 wanaishi.

Mji wa Gitega unapatikana katikati mwa Burundi, takriban kilometa 100 mashariki ya Bujumbura. Mwishoni mwa utawala wa kifalme mnamo mwaka 1966, Gitega yalikuwa makao makuu ya ufalme wa Burundi, ambayo mtawala wake wa mwisho, Mfalme Mtutsi Ntare V. Ndizeye, aliuliwa kufuatia uasi wa Wahutu mwaka 1972. Wakosoaji wa rais Nkurunziza, wanaiona hatua ya kuhamia Gitega kama kurejea katika utawala wa kifalme ambao kauli mbiu yake ilikuwa Imana, Umwan, Uburundi, yaani Mungu, Mfalme na Burundi". Mji wa Bujumbura umeendelea kuwa ngome ya upinzani katika miaka ya hivi karibuni. Haifahamiki lakini vipi uhamaji huo utakavyogharimiwa.

Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe MagufuliPicha: DW/E. Boniphace

Burundi na Sudan Kusini sasa zinazifuata nchi kama Tanzania, ambayo rais wake wa kwanza, baba wa taifa, Julius Kambarage Nyerere aliuhamishia mji mkuu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma mnamo mwaka 1974, Nigeria, ambayo makao makuu ya serikali yalihamishwa kutoka Lagos hadi Abuja na Ivory Coast ambayo iliuhamisha mji wake mkuu Abdijan hadi Yamoussoukro. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, anataka kuikamilisha ndoto ya baba wa taifa kwa kuzihamishia Dodoma wizara zote na idara za serikali kufikia mwisho wa mwaka huu. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilimnukuu Anton Cartwright, mchumi kutoka Capetown Afrika Kusini akisema watu katika mataifa haya hawanufaiki sana na hatua hizi za kuihamisha miji mikuu na serikali zinatakiwa kuongeza jitihada kuboresha miundombinu iliyopo katika miji yao badala ya kutumia fedha nyingi kwa miradi ya kifahari.

Uwekezaji katika afya huleta tija

Mada nyingine katika magazeti ya Ujerumani wiki hii ilihusu uwekezaji katika sekta ya afya. Gazeti la Neue Zürcher liliandika hivi: Fedha huwekezwa vyema katika afya. Bara la Afrika limejidhirisha kama mfano bora kuhusu jinsi matumizi ya serikali katika afya ya umma na kuanzisha bima ya afya yanavyoleta tija.

Gazeti la Neue Zürcher liliripoti kwamba magonjwa husababisha dola trilioni 2.4 za kimarekani kupotea barani Afrika kila mwaka. Idadi hii ilichapishwa na shirika la afya duniani WHO katika kongamano lake la pili barani Afrika mjini Praia nchini Cape Verde. Mawaziri 750, wataalamu na wawakilishi wa mashirika mbalimbali kutoka nchi 47 za Afrika walikutana kuanzia siku ya Jumanne hadi Alhamisi wiki iliyopita katika kisiwa hicho cha bahari ya Atlantiki. Mhariri alisema upatikanaji wa huduma za afya unaweza kukuza uchumi wa Afrika kwa dola bilioni 796 kwa mwaka. Ukweli ni kwamba matumizi ya fedha kwa ajili ya afya katika nchi 25 barani Afrika yalipungua kati ya mwaka 2000 na 2015 ikizingatiwa bajeti jumla.

Mariano Castellon WHO
Mariano Castellon, mjumbe maalumu wa shirika la afya ulimwenguni WHO nchini Cape VerdePicha: WHO/V. Martin

Miaka 20 iliyopita mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara yaliahidi kutumia angalau asilimia 15 ya bajeti zao kwa ajili ya afya, lakini ni nchi tatu tu zinazofanya hivyo. Ripoti ya shirika la WHO inaonyesha iwapo hali hii itaendelea, Afrika itapata hasara inayotokana na magonjwa kufikia thamani ya dola trilioni 1.7 ifikapo mwaka 2030. Kipengee muhimu katika kutafuta suluhisho la tatizo hili kilichojadiliwa katika kongamano la WHO ni bima ya afya. Upatikanaji wa bima hiyo unakosekana kabisa au ni haba katika mataifa mengi ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Mifano mizuri ya kuigwa ni Cape Verde ambako asilimia 40 ya wananchi wana bima ya afya na Rwanda, karibu kila mtu ana bima ya afya.

Afrika yahitaji uhuru halisi

"Afrika ya Kesho". Ndivyo lilivyoandika gazeti la Der Tagesspiegel. Felwine Sarr, mhadhiri anayefundisha uchumi katika chuo cha Saint Louis nchini Senegal, ametoa mwito wa uhuru halisi wa bara la Afrika na kuushinda ukoloni mamboleo. Mhariri wa gazeti la Der Tagesspiegel anasema kichwa cha makala aliyoiandika Sarr kinaangazia mustakabali wa bara la Afrika.

Mhariri anasema hata hivyo Sarr anajipinga mwenyewe katika kurasa za mwanzo kwa kuzungumzia Afrika kama bara la siku za usoni, maneno anayopenda sana kuyatumia waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Gerd Müller. Mhariri anatilia maanani kwamba kwa kusema hivyo ina maana ya kufuta kabisa mazuri yote yaliyopo barani humo kwa sasa. Sarr aliandika kuwa mamilioni ya watu wanaambiwa kila siku kwa mifumo tofauti kwamba maisha yao wanayoishi hayana maana yoyote. Anataka watu wafikirie tofauti kuhusu mustakabali wa Afrika na ana shauku ya kutengeneza mfumo wa maisha ya kisasa utakaokuwa wa haki kwa Waafrika wenyewe. Nia yake ni kujenga aina ya umoja wa watu wote wa Afrika wenye hatima moja na mapambano yanayofanana.