1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanogo atoa amri

MjahidA1 Aprili 2012

Kiongozi wa jeshi lililoasi na kupindua serikali nchini Mali, Kapteni Amadou Sanogo, ameliamrisha jeshi lake kutorefusha mapigano katika mji mmoja kaskazini mwa nchi hiyo

https://p.dw.com/p/14VxV
Kiongozi wa jeshi Mali, Amadou Sanogo
Kiongozi wa jeshi Mali, Amadou SanogoPicha: Reuters

Sanogo amesema ametoa amri hiyo kufuatia waasi wa Tuareg kujizatiti kudhibiti miji ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Habari zaidi zinasema, amri ya kusimamisha mapigano katika eneo hilo imetolewa ili kuwatoa wanajeshi wa serikali katika eneo hilo kutokana na kuondoka kwa majeshi kwenye sehemu nyengine kaskazini mwa Mali katika siku chache zilizopita.

Kwa sasa waasi hao wa Tuareg wamefanikiwa kusonga mbele na kuuteka mji mwengine wa Gao siku moja baada ya kuuteka mji wa Kidal. Hatua hii inazidi kudhoofisha hali ya usalama, baada ya wanajeshi walioasi kuipindua serikali kwa madai ya kushindwa kuwapa silaha za kutosha kupambana na waasi wa Tuareg.

Mmoja wa waasi wa Tuareg
Mmoja wa waasi wa TuaregPicha: picture-alliance/dpa

Maeneo mengi kaskazini mashariki mwa Mali yanadhibitiwa na waasi wa Tuareg na washirika wake wa kundi la Kiislamu lililo na msimamo mkali. Hata hivyo, hakujatolewa idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano baina ya waasi hao na serikali katika kudhibiti miji.

Mji wa Gao uko kilomita 1,200 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Bamako, ambapo wanajeshi walichukua udhibiti wa serikali siku 10 zilizopita. Mataifa jirani na Mali yamelaani mapinduzi hayo na kuipa nchi hiyo saa 72 kurejesha utawala wa kidemokrasia la sivyo wawekewe vikwazo.

Mazungumzo yafanyika

Jana jeshi hilo lilituma ujumbe wake kukutana na rais wa nchi jirani ya Burkina Faso, Blaise Compaore. Muakilishi wa jeshi hilo, Moussa Coulibaly, baadaye aliwaambia waandishi habari wana matumaini kwamba watakuwa na suluhisho la namna ya kurudisha tena taasisi za serikali kwa njia ambayo zitakubaliwa na dunia nzima. Taasisi hizo zilisimamishwa kufanya kazi baada ya mapinduzi.

Huku hayo yakiarifiwa, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Burkina Faso, Djibril Bassole, alikuwa na mazungumzo na kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi wa Mali, Amadou Sanogo. Baada ya mkutano Sanogo alinukuliwa akisema jeshi lake litatathmini suluhu ya kusawazisha mambo katika saa kadhaa zijazo bila kutoa maelezo zaidi.

Jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi Ecowas, imeweka wanajeshi 2,000 katika hali ya matayarisho, iwapo itahitajika kuingia kwa nguvu nchini Mali.

Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaoré
Rais wa Burkina Faso, Blaise CompaoréPicha: AP

Awali Sanogo aliomba usaidizi kutoka kwa mataifa ya kigeni ili kupambana na waasi wa Tuareg. kutokana jeshi hilo kupindua serikali, Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine ya magharibi wamekatiza miradi ya mamilioni ya pesa nchini humo hadi pale katiba ya nchi hiyo itaregeshwa na uchaguzi wa haraka kufanyika.

Kwengineko zaidi ya raia 25,000 mjini Bamako wameitika mwito kutoka kwa viongozi wa Kiislamu na Kikristo katika kuombea amani ya nchi hiyo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef