1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yataka shinikizo zaidi dhidi ya Iran

27 Septemba 2019

Saudi Arabia imetoa wito kwa ulimwengu kutumia njia zozote kuongeza shinikizo ili kukomesha kile ilichokiita "mwenendo wa kichokozi wa Iran” ikisema njia madhubuti dhidi ya Iran ni kuifunga mirija yake ya kupata fedha. 

https://p.dw.com/p/3QK9L
Tunesien Treffen der arabischen Aussenminister | Ibrahim al-Assaf
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Saudi Arabia, Ibrahim al-AssafPicha: Reuters/Z. Souissi

Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia Ibrahim al-Assaf kwa mara nyingine ameilaumu Iran kwa mashambulizi ya Septemba 14 kwenye miundombinu muhimu ya mafuta ya Saudia.

"Tunafahamu kikamilifu nani aliyekuwa nyuma ya uchokozi huu” Al-Assaf aliwaambia wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linaloendelea mjini New York, Marekani.

Mwanadiplomasia huyo ameyataja mashambulizi hayo ya mwezi Septemba kuwa ukiukwaji wa kiwango cha juu wa sheria za kimataifa na kitisho kwa amani na usalama wa ulimwengu.

"Ndugu rais, mabibi na mabwana, tumeufahamu utawala huu kwa miaka 40. Hauna manufaa yoyote zaidi ya kuratibu milipuko, uharibifu na mauaji, sio kwenye kanda yetu pekee bali kote duniani. Huu ni utawala ule ule ambao tangu ulipoasisiwa umefanya mashambulizi ya kigaidi ndani ya Saudia Arabia, Bahrain, Kuwait, Lebanon pamoja na mataifa ya Ulaya na mbali ya hapo” amesisitiza al-Assaf.

Al-Assaf : Ulimwengu ulenge vyanzo vya fedha vya Iran

USA Hassan Rohani spricht vor der UN-Vollversammlung
Rais wa Iran, Hassan RouhaniPicha: AFP/D. Angerer

Said al-Assaf ameongeza kuwa ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kutambua kuwa kuvikata vyanzo vya mapato ya kifedha kwa Iran ndiyo njia sahihi ya kuilazimisha nchi hiyo kuacha kuyaunga mkono makundi ya wapiganaji wenye silaha, kuizuia kuunda makombora ya masafa marefu na kukomesha shughuli zinazotatiza uthabiti wa kanda ya mashariki ya kati na dunia kwa jumla.

Saudi Arabia inasisitiza kuwa silaha za Iran ndiyo zilitumika kuishambulia miundombinu yake ya mafuta na imewakaribisha wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kufanya tathmini ya wapi mashambulizi yalitokea.

Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pia zinailaumu Iran.

Iran kwa upande wake imekanusha madai ya nchi hizo na jana Alhamisi rais wa nchi hiyo Hassan Rouhani ametaka utolewe ushahidi wenye vielelezo kuthibitisha kuwa Tehran ilikuwa nyuma ya hujuma hizo.

Marekani yatuma wanajeshi na vifaa eneo la ghuba

Licha ya yote hayo rais Donald Trump amejizuia walau kwa hivi sasa kuchukua hatua zozote za kijeshi dhidi ya Iran.

US Truppen im Persischen Golf
Picha: Imago/ZUMA Press/USMC/Cpl. D. Morgan

Lakini ameidhinisha hatua pana za kuimarisha ulinzi nchini Saudi Arabia na kanda nzima ya eneo la Ghuba.

Hapo jana Washington ilitangaza kuwa inatuma vikosi zaidi vya kijeshi katika eneo la ghuba hatua inayoweza kuongeza mvutano kati ya Marekani na Iran

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema kuwa inapeleka wanajeshi 200 pamoja na mifumo ya kujilinda dhidi ya makombora ili kuimarisha ulinzi wa Saudi Arabia.

Uamuzi huo wa Marekani ambao unajumisha pia kupelekwa kwa rada nne za kijeshi ni matokeo ya mashambulizi ya Septemba 14 kwenye miundombinu ya kuzalisha mafuta nchini Saudi Arabia.