1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Serikali ya Sudan ishinikizwe"

6 Agosti 2007

Makundi kumi ya waasi wanaopigana katika eneo la Darfur yamekubaliana kuwa na msimamo wa pamoja kwenye mazungumzo ya amani na serikali ya Sudan. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika katika muda wa miezi mitatu ijayo. Lakini je, makubaliano kati ya waasi yaliyofikiwa huko Arusha kweli ni mafanikio makubwa? Soma uchambuzi wa mwandishi wetu Antje Diekhans.

https://p.dw.com/p/CH9y

Kwa wale walioandaa mkutano huu mjini Arusha, tukio lenyewe lilikuwa la mafanikio, hata kabla ya viongozi wa waasi kuwasili Arusha. Kwa kweli, wapatanishi hao wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika waliweza kuwashawishi wanamgambo hao kubadilisha nguo zao, kuvaa suti na kukubali mazungumo. Kwa hivyo, hatua ya kwanza kwenye ratiba ya kuelekea amani imefikiwa. Tukumbuke kidogo ratiba hiyo: Kwanza, viongozi wa waasi wakubaliane juu ya msimamo wa pamoja. Pili, serikali na waasi waanze mazungumzo. Tatu, mkataba ya amani utiwe saini na jeshi kubwa la amani la Umoja wa Mataifa litumwe Darfur. Huo ndio mpango wenyewe.

Lakini tayari katika hatua ya kwanza kuna shida fulani. Kiongozi mmoja muhimu wa jeshi la ukombozi wa Sudan, Abdelwahid el Nuur, amekataa kushiriki kwenye mkutano wa Arusha kwa sababu, kama alivyosema, matokeo yake ni ya karatasini tu. Abdelwahid el Nuur hana wanamgambo wengi lakini anaungwa mkono na sehemu kubwa ya wakazi wa Darfur. Bila ya yeye kuhusika, maafikiano ya Arusha hayana uzito.

Mtu mwingine muhimu kuhusiana na mzozo wa Darfur, Suleiman Jamous, ameshindwa kufika Arusha kwa sababu hana ruhusa ya kutoka Darfur, la sivyo, serikali ya Sudan imetishia itamfunga gerezani. Mara nyingi, Suleiman Jamous amepatanisha kati ya waasi na upande wa serikali. Kwa kutomruhusu kusafiri Arusha, serikali ya Sudan inatoa ishara kwamba haitaki makubaliano yafikiwe.

Kabla ya mazungumzo ya amani hayajaanza, serikali hiyo ilidanganya juu ya lengo lake. Upande mmoja inasema imesikitishwa kuwa Abdelwahid el Nuur hakuweza kushiriki kwenye mkutano wa Arusha, lakini, wakati huo huo, inamzuia muasi mwingine kwenda Arusha. Serikali ya Sudan inasifu juhudi za waasi kufikia msimamo wa pamoja, lakini wiki chache tu zilizopita ilipashambulia mahala pa mkutano wa waasi. Serikali hii inataka mkataba wa amani, lakini pia imewahamisha maelfu ya Waarabu waungane na wanamgambo wa Janjaweed pindi mambo hayataenda vizuri.

Kwa hivyo, kuwa na msimamo wa pamoja hakutawasaidia waasi katika mazungumzo ya amani. Kwanza inabidi serikali ya Sudan iachane na udanganyifu. Lazima serikali hii ishinikizwe na jumuiya ya kimataifa, kama Marekani na waziri mkuu wa Uingereza walivyofanya kwa kutishia kuiwekeza Sudan vikwazo iwapo itazisumbua juhudi za kusaka amani. Iwe wazi kuwa safari hii jumuiya ya kimataifa haitausahau tena mzozo wa Darfur.