1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Tanzania kuunga mkono kilimo cha zao la Chikichi

Prosper Kwigize17 Septemba 2021

Waziri Mkuu wa Tanzania ametangaza azma ya serikali kujitegemea kwenye uzalishaji wa mafuta ya kula na kuepuka gharama kubwa za kuagiza bidhaa hiyo nje.

https://p.dw.com/p/40SxF
Malaysia Palmöl-Plantage in Slim River
Picha: Lim Huey Teng/REUTERS

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo mkoani Kigoma baada ya kutembelea shamba la michikichi la Kikosi cha 821 JKT Bulombora wilayani Kigoma, ambapo amesisitiza kuwa mbali na taasisi za majeshi kupewa dhamana ya kuwa mfano wa kulima chikichi mwananchi mmoja mmoja wamehimizwa kuanzisha mashamba na serikali inawajengea uwezo kwa kuwagawia miche bure.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha jeshi la kujenga taifa namba 821 JKT Bulombora Luteni Kanali Emmanuel Raphael Kukula, akimweleza Waziri Mkuu kuwa mpaka sasa wamepanda Zaidi ya ekali 500 za michikichi kati ya ekali elfu 2000 zilizokusudiwa.

Zigo la kuhakikisha malengo yanafikiwa linawaangukia wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maafisa wa kilimo katika wilaya zote za mkoa wa Kigoma ambapo Waziri Mkuu anatoa maelekezo mazito kwao

Changamoto ya mafuta nchini Tanzania imekuwa kubwa kila kukicha ambapo upatikanaji wake umekuwa duni na bei kupanda, mwelekeo wa serikali wa kusisitiza kilimo cha michikichi unaweza kuwa mwarobaini lakini si wa kutarajiwa katika kipindi kifupi kama anavyoelezea mwananchi huyu kutoka Kigoma. Waziri mkuu Kassim Majaliwa yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua shughuli za maendeleo hususani kilimo.