1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria kali kwa watumiaji dawa za kusisimua misuli

19 Novemba 2012

Shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini WADA limependekeza rasimu ya sheria ambayo itawezesha adhabu kali dhidi ya watumiaji wa dawa zilizopigwa marufuku

https://p.dw.com/p/16lfX
Australian John Fahey, President of the World Anti-Doping Agency, WADA, speaks during a WADA Media Symposium in Lausanne, Switzerland, Tuesday, Feb. 7, 2012. (Foto:Keystone/Jean-Christophe Bott/AP/dapd)
John Fahey WADA World Anti-Doping AgencyPicha: AP

WADA pia itakuwa mamlaka ya kufanya upelelezi wa kibinafsi kuhusu visa vya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku, kama mashirika ya michezo ya kitaifa yatashindwa kuchukua hatua. Rasimu hiyo ya WADA ambayo itatathminiwa mwezi ujao wa Desemba na kuidhinishwa mwaka wa 2013, inatoa wito wa adhabu ya miaka mine ya kushiriki michezo yoyote badala ya miaka miwili chini ya sheria ya sasa.

Mwenyekiti wa WADA John Fahey amesema ujumbe huo ni muhimu kwa watu wanaotumia dawa za kusisimua misuli. Fahey ambaye alikuwa nchini Kenya hivi karibuni, amesema alikasirishwa mno kwa sababu maafisa nchini humo hawafanyi uchunguzi kuhusiana na ripoti iliyotolewa na mwaandishi mmoja wa habari wa Ujerumani iliyosema kwamba watu wnaojifanya kuwa madaktari wanawauzia wanariadha wa Kenya dawa za kuongeza nguvu mwilini. Anaongeza kuwa alizungumza na waziri pamoja na Rais wa Kamati ya Olimpiki nchini humo kuhusu suala hilo. Kasha akawaandikia barua ya kuuliza kama uchunguzi huru umeanzishwa kuhusu madai hayo. Lakini kufikia sasa hajapata jibu lolote. Sheria hiyo ya WADA itaanza kutekelezwa mwaka wa 2015.

Mwendesha baiskeli Lance Armstrong alivuliwa mataji yake saba ya Tour de France
Mwendesha baiskeli Lance Armstrong alivuliwa mataji yake saba ya Tour de FrancePicha: Reuters

Ligi ya Mabingwa Ulaya

Mabingwa watetezi Chelsea na mabingwa wa Ligi Kuu ya soka Uingereza Manchester City wanakabiliwa na kibarua kigumu kitakachoamua hatima yao ya kuendelea au kutemwa nje ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Chelsea watakuwa nyumbani kwa mabingwa wa Ligi ya Italia Serie A Juventus katika mchuano wa kundi E kesho. Kama watashinda, basi watafuzu katika awamu ya timu 16 za mwisho, lakini kama watashindwa basi mambo yatakuwa magumu kwa sababu viongozi wa kundi hilo Shakhtar Donetsk hawatarajii kuteleza dhidi ya klabu ya Nordsjaelland.

City ambao hawajashinda mchuano wowote wanahitaji muujiza Jumatano katika kundi D, ushindi dhidi ya mabingwa wa Uhispania Real Madrid na mwingine dhidi ya mabingwa wa Bundesliga Borussia Dortmund katika awamu ya mwisho ili wawe na fursa ndogo ya kufuzu. Arsenal nayo itafuzu kama itawazaba Montpellier katika mchuano wa kundi B nao viongozi Schalke wawazabe Olympiakos Piraeus. Timu ya pekee ya Uingereza ambayo tayari imefuzu ni Manchester United, timu ya pekee katika kinyang'anyiro hicho na pointi zote 12 kutokana na mechi nne. Porto na Malaga pia wamefuzu kwa awamu ya 16 za mwisho.

Borussia Dortmund tayari imeweka mguu mmoja katika awamu ya 16 za mwisho ya Champions League
Borussia Dortmund tayari imeweka mguu mmoja katika awamu ya 16 za mwisho katika Champions LeaguePicha: picture-alliance/dpa

Paris St Germain, Schalke, Arsenal, Borussia Dortmund, Real Madrid, Shakhtar Donetsk, Chelsea, Valencia, Bayern Munich, Barcelona na Celtic wanaweza kujikatia tikiti ya awamu ya 16 za mwisho kama mambo yatawaendea vyema na wapate ushindi. Chelsea na Shakhtar zina pointi saba kila mmoja na Juve sita. Chelsea walishindwa magoli mawili kwa moja dhidi ya Westbrom katika mechi ya Ligi kuu Uingereza mwishoni mwa wiki. Nao Juve wakatoka sare ya bila kufungana na Lazio.

Real watakuwa bila ya huduma za Marcelo na Gonazlo Higuain na uwezekeno wa kuwa bila ya Michel Essien. Lakini Sami Khedira na Karim Benzema wako katika hali nzuri baada ya kuonyesha mchezo mzuri walipofunga magoli katika ushindi wao wa Jumamosi dhidi ya Athletic Bilbao wa magoli matano kwa moja. Borussia Dortmund wanaongoza kundi hilo gumu D na point nane mbele ya Real, Ajax Amsterdam na City na watafuzu kama watashinda mjini Amsterdam.

Real Madrid inaingia dimbani na matumaini makubwa baada ya ushindi wa La Liga
Real Madrid inaingia dimbani na matumaini makubwa baada ya ushindi wa La LigaPicha: picture-alliance/dpa

Barcelona iko mbele ya Cletic na hawatatarraji kuteleza mjini Moscow dhidi ya Spartak kesho nao Celtic wakipambana na Benfica katika mchuano mwingine. Barca wamesafiri Urusi bila huduma za majeruhi Adriano, Marc Bartra, Thiago na Alexis Sanchez, lakini wamepigwa jeki na beki wao Carles Puyol na Gerard Pique. Mlinda lango wa zamani Edwin van der Sar amejiunga na bodi ya klabu ya Ajax Armsterdam kama mkurugenzi wa mauzo. Klabu hiyo imesema Van der Sar ambaye alianza taaluma yake ya kandanda katika klabu ya Ajax na akamaliza miaka sita katika klabu ya Manchester United, amejiunga na bodi ya klabu hiyo pamoja na Michael Kinsbergen ambaye atakuwa Meneja Mkurugenzi: Van der Sar alistaafu mwaka wa 2011 baada ya taaluma ya kufana ambayo ilimpa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa na manane ya ligi za nyumbani.

Vettel akaribia ushindi wa tatu

Na katika mashindano ya mbio za magari ya Formula One, dereva wa timu ya Red Bull Sebastian Vettel na mwenzake wa Ferrari Fernando Alonzo watakabana koo katika mkondo wa kufunga msimu wiki hii mjini Sao Paolo, Brazil. Wawili hawa walimaliza katika nafasi ya pili na tatu jana katika mkondo wa Marekani ulioshindwa na Lewis Hamilton. Vettel angehitimisha ubingwa wake wa tatu mfululizo kama angeshinda mkondo huo naye Alonso asajili matokeo mabaya. Lakini Mjerumani Vettel amepata pointi tatu kutoka kwa Alonso na sas anaongoza na jumla ya 13 wakati akielekea Amerika Kusini kuandikisha historia. Kama Vettel mwenye umri wa miaka 25 atashinda taji lake la tatu mfululizo, atajiunga na Michael Shumacher na Juan Manuel Fangio kama madereva wa pekee kupata ubingwa mara tatu mfululizo.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu