1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa kupinga jinai dhidi ya waandishi habari

Isaac Gamba
2 Novemba 2017

Wakati leo kukiadhimishwa siku ya kimataifa ya kupinga vitendo vya jinai dhidi ya waandishi wa habari, huko nchini Tanzania waandishi wa habari wamekuwa wakikumbana na visa vya kuandamwa na dola.

https://p.dw.com/p/2msxi
Kajubi Mukajanga
Picha: DW/E. Boniphace

Ingawa waandishi hawa wa habari wanatajwa kama muhimili wa nne katika taifa lakini dhana hiyo inasalia kwenye makaratasi pekee kwani madhila wanayokumbana nayo hayafanani na nadharia hiyo ya kuwa mshirika muhimu katika ujenzi wa taifa.

Idadi ya waandishi wa habari wanakumbwa na matukio ya kupigwa, kutishwa na hata kutiwa korokoroni imekuwa ikiongezeka huku wengine wakijikuta wakiwa njia panda baada ya vyombo vyao kutiwa msukosuko.

Watendaji wa Serikali kama wakuu wa mikoa na wilaya, polisi na mamlaka nyingine za kiutendaji ndizo zinazotupiwa lawama kuwa sehemu ya kukwaza uhuru kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao.

Picha yenye ujumbe wa kukomesha mauaji dhidi ya waandishi wa habari
Picha yenye ujumbe wa kukomesha mauaji dhidi ya waandishi wa habariPicha: UNESCO

Akizungumzia siku hii ya leo na usalama wa waandishi wa habari nchini Tanzania, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari, Kajubi Mukajanga alisema usalama wao uko majaribuni kwa vile waandishi wengi wa habari walikumbwa na misukosuko wakati wakitekeleza majukumu yao.

Baadhi ya makundi ya kutetea haki za binadamu na utawala wa kisheria yakikua yakielezea wasiwasi wao kuhusu dhana ya uhuru wa vyombo vya habari, kutokana na mwenendo wa hivi karibuni wa kufungiwa kwa baadhi ya magazeti.

Ripoti zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita jumla ya magazeti 6 yalikumbwa na misukosuko ya kufungiwa huku Serikali ikionya kuchukua hatua zaidi ka magazeti yatakayokiuka weledi wa kazi. Magazeti hayo yaliyofungiwa kwa vipindi tofauti ni pamoja na Mseto, Mwanahalisi, Mawio, Tanzania Daima na Raia Mwema.

Brasilien Rios Polizei tötet Touristin aus Spanien
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika majukumu yao ya kaziPicha: Reuters/R. Moraes

Ama kutokana na kile baraza la habari imekieleza kuendelea kwa matukio ya ukandamizaji waandishi wa habari wawapo kazi, kuanzia sasa wale watakaoonekana kujichukulia sheria mikononi  mwao ama kutumia vibaya madaraka yao, watafikishwa mahakamani.

Hata hivyo, akizungumza wiki iliyopita katika mdahalo ulioandaliwa na idhaa hii, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali siyo adui wa waandishi wa habari na wakati wote inakaribisha mazungumzo kabla ya kutoa adhabu hizo.

Siku ya kupinga uonevu kwa waandishi wa habari duniani iliidhinishwa katika azimio lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha 68 kilichofanyika 2013.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman