1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier aiuma akiipuliza Uturuki

Mohammed Khelef
15 Novemba 2016

Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ameikosoa serikali ya huko kwa kuukandamiza upinzani, ingawa amesisitiza kuwa Uturuki iendelee kuomba kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2SjgY
Türkei Frank-Walter Steinmeier und Mevlut Cavusoglu
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Ziara hii inajiri katika siku ambayo magazeti kadhaa nchini Ujerumani kwenyewe yamechapisha tahariri za gazeti la Cumhuriyet linaloandamwa na serikali ya Rais Tayyip Erdogan kuonesha uungaji mkono wao kwa wapiganiaji demokrasia wa Uturuki. 

Akizungumza mchana wa leo (Novemba 15) katika mkutano na waandishi wa habari kati yake na mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, mjini Ankara na ikiwa ni siku moja tu baada ya mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kumaliza kikao chao kilichokuwa kikisaka msimamo wa pamoja kuelekea Uturuki, Steinmeier amesema baadhi ya mawaziri wenzake kwenye Umoja huo, wanataka kuachana kabisa na uwezekano wa Uturuki kujiunga nao.

"Baadhi kwenye Umoja wa Ulaya wanatetea wazo kwamba kusitisha mazungumzo na Uturuki litakuwa jambo linalofaa zaidi. Mimi natetea wazo jengine na nimeeleza hilo wazi hapo kabla. Nadhani uamuzi huo ni wa kufanywa na Uturuki yenyewe", alisema Steinmeier.

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yanakasirishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Rais Erdogan kuwaandama wakosoaji wake, yakisema kuwa rikodi ya haki za binaadamu ya Uturuki haiendani na viwango vya Ulaya.

Tangu jaribio la mapinduzi dhidi ya Erdogan kushindwa mwezi Julai mwaka huu, serikali yake imeendelea na kampeni kubwa kabisa ya kuvunja kila nguvu ya vyama vya upinzani dhidi yake. 

Akin Atalay Herausgeber Cumhuriyet
Mwenyekiti wa Bodi ya gazeti la Cumhuriyet la Uturuki, Akin Atalay, na wenzake tisa wako ndani kwa wiki ya pili, huku polisi ikidai wanahusika na kundi la wanamgambo wa PKK na ulamaa Fethullah Gulen.Picha: picture-alliance/dpa/V. Arik

Waziri Steinmeier amesema kuwa kwenye mazungumzo yake na viongozi wa Uturuki, amelieleza kwa upana suala hilo, huku akiwasilisha mtazamo na msimamo wa nchi yake na Umoja wa Ulaya, akitaka Uturuki iheshimu uhuru wa kujieleza, watu kukusanyika na wa vyombo vya habari.

Uturuki yaijia juu Ulaya

Mwenyeji wake, Casuvoglu, alitumia pia nafasi hiyo kuukosoa Umoja wa Ulaya kwa ujumla, akisema unaitendea visivyo nchi yake. Akitetea wazo la Rais Erdogan la kuitisha kura ya maoni hapo mwakani juu ya ikiwa wajiunge na Umoja huo, Cavusoglu alisema nchi yake haistahiki kuchukuliwa kama kituko na watu ambao inawachukulia kuwa ndugu zao.

"Kila siku, mmoja wa waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya anakuja na kusema: 'Tuitoweni Uturuki kwenye majadiliano, tuwatoweni kwenye NATO.' Mara hili, mara lile. Nyiye ni nani wa kutufukuza sisi? Kwanza hamuna mamlaka hayo. Kunapaswa kuwapo maridhiano. Na tunasema hatustahiki kutendewa hivi!" Alisema Cavusoglu.

Ziara ya Steinmeier nchini Uturuki imesadifiana na kampeni ya vyombo vya habari vya Ujerumani, ambapo siku ya leo magazeti kadhaa yaliamka na tahariri ya gazeti la Cumhuriyet linalopigwa vita na serikali ya Uturuki, yakisema ni sehemu ya kuwaunga mkono waandishi wa habari wanaokabiliwa na kifungo nchini Uturuki.

Tangu jaribio la mapinduzi la mwezi Julai kushindwa, gazeti hilo limesimama kidete dhidi ya utawala wa Rais Erdogan na chama chake cha AKP. 

Kwa wiki mbili sasa, polisi inamshikilia mhariri wake mkuu, Murat Sabuncu, mwenyekiti wa bodi Akin Atalay na wafanyakazi wengine wanane wa gazeti hilo, wakidaiwa kuhusika na chama cha Kikurdi cha PKK na pia ulamaa wa Kiislamu, Fethullah Gulen, anayeishi uhamishoni nchini Marekani, ambaye Rais Erdogan anasema alihusika na jaribio la mapinduzi dhidi yake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba