1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini kukabiliwa na vikwazo vya silaha?

Lilian Mtono
25 Januari 2018

Tume ya kufuatilia usitishwaji mapigano Sudan Kusini imeuomba Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo vya silaha Sudan Kusini kutokana na kushindwa kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/2rWVH
Nikki Haley
Picha: picture-alliance/M.Altaffer

Timu inayofuatilia zoezi la usitishwaji mapigano na inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa nchini Sudan Kusini imesema, imeliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutamka iwapo viongozi wanaokiuka makubaliano ya amani wataweza kukabiliwa na hatua za kukamatwa mali zao, kuzuiwa vibali vya kusafiri nje ama kuwekewa vikwazo vya silaha. 

Taarifa hiyo inakuja siku chache baada ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley kuliomba baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo vya silaha Sudan Kusini kufuatia kushindwa kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano, kwa lengo la kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka minne nchini humo.

Balozi Haley ameliambia baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba serikali ya rais Salva Kiir imezidi kujidhihirisha kwa kile alichoeleza kama "mshirika asiyefaa", katika juhudi za kurejesha amani na kuomba viongozi wa Afrika kuiwajibisha kuhusu hilo, akiwataja marais wa Uganda na Kenya kumshinikiza Kiir, akisema wao ni watu muhimu katika kufikia mafanikio ya kweli ya amani.  

Sudan Kusini imekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013 baada ya makabiliano kati ya wanajeshi wanaomtii makamu wa zamani rais Riek Machar na rais Salva Kiir. Mapigano hayo yalisababisha mauaji ya mamia kwa maelfu ya raia, kusababisha kusambaa kwa baa la njaa na theluthi ya raia kuyakimbia makaazi yao.

Südsudan Juba - Riek Machar, Salva Kiir
Aliyekuwa makamu wa rais wa Sudan Kusini, Riek Machar akiwa na rais Salva Kiir baada ya mkutano wa kwanza wa kuunda serikali ya mpito, mwezi Aprili, 2016 Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

Jumanne hii, mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto, UNICEF aliyekwenda nchini Sudan Kusini hivi karibuni Henrietta Holsman Fore aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba hali nchini humo si ya kuridhisha, na hususani kwa watoto wanaokabiliwa na utapiamlo, kupotea na unyanyasaji wa kijinsia.

Tume hiyo inayofuatilia usimamishaji wa mapigano, inayosimamiwa na rais wa Botswana Festus Mogae inatakiwa kuyasimamia makubaliano yaliyofikiwa mnamo mwaka 2015, ambayo hata hivyo yanaelezwa kuwa yamepuuzwa kwa kiasi kikubwa. Mara kadhaa, pande zote zimekiuka makubaliano hayo. Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Disemba mwaka jana yalianza kuvunjwa ndani ya saa moja tangu yalipofikiwa, tume hiyo imesema.

Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini Michael Maueli Lueth ameliambia shirika la habari la Reuters hii leo kwamba tume hiyo ya kufuatilia usitishwaji wa mapigano haikuzingatia haki na ilitegemea taarifa kutoka vyanzo vingine.

Alisema "Inasikitisha na taarifa yao ni ya kupotosha. Na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halikutakiwa kuisikiliza ripoti hiyo, na kuongeza kuwa walikuwa wakifanya jitihada za kuidhoofisha serikali ili kuwapa nafasi waasi waweze kujiimarisha na kuchukua nafasi."

Kaimu msemaji wa waasi Lam Paul Gabriel amesema, watakaribisha uingiliaji wowote kutoka jamii ya kimataifa ili kutekeleza hatua ya kusimamisha mapigano.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga