1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika Kati Magazetini

20 Desemba 2013

Mapigano katika jamhuri changa ya Sudan kusini,hali katika jamhuri ya Afrika kati na mazishi ya shujaa msuluhivu wa Afrika kusini ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa Ujerumani wiki hii.

https://p.dw.com/p/1Adve
Rais Salva Kiir wa Sudan KusiniPicha: Reuters

Tuanzie na kitisho cha kuzuka vita vya kikabila katika jamhuri changa ya Sudan kusini."Mamia wameuwawa kufuatia mapigano katika mji mkuu Juba na maelfu wamekimbia kuomba hifadhi katika vituo vya Umoja wa Mataifa huku Uganda ikitishia kuingilia kati" hivyo ndivyo lilivyoandika gazeti la die Tageszeitung la mjini Berlin linalosimulia hali namna ilivyo katika mji mkuu wa Sudan Kusini-Juba.Rais Salva Kiir anamtupia lawama mpinzani wake mkubwa,makamo wake wa zamani wa rais Riek Machar. Mashahidi wanasema watu kadhaa wa kabila la Machar- Nuer wanakamatwa na wengine kuuliwa.Wadadisi wanahofia rais Salva Kiir asije akawaachia watu wa kabila lake la Dinka kuwaandama wapinzani kwa sababu za kikabila.-Hali hiyo inaweza kusababisha vita vya wenyewe kuripuka katika nchi hiyo iliyoteketezwa kwa vita na ambayo imejipatia uhuru wake toka Sudan,miaka miwili tu iliyopita.

Die Tageszeitung limemalizia ripoti yake kwa kumnukuu msemaji wa jeshi la Uganda Paddy Ankunda akionya wanajeshi 2000 wa nchi yake wamewekwa karibu na mpaka wa Sudan Kusini,tayari kuingilia kati kuwavunja nguvu wale watakaotaka kuitumia hali iliyozuka ili kusababisha hasara miongoni mwa jamii."

Kitisho cha Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe

Der Tagesspiegel linaandika kuhusu kinyang'anyiro cha kuania madaraka kati ya rais Salva Kiir na makamo wake wa zamani Riek Machar kilichogeuka mapambano ya mtutu wa bunduki.Hata gazeti la Süddeutche Zeitung linazungumzia kuhusu kinyang'anyiro cha kuania madaraka kati ya mahasimu hao wawili na kukumbusha mzozo huu umeanza tangu Julai pale rais Kiir alipomuachisha kazi kwa ghafla makamo wake Machar ambae hafichi azma yake ya kutaka binafsi kuwa rais wa nchi hiyo.Katika wakati ambapo katika mji mkuu Juba hali kidogo ni shuwari,mapigano yanaripotiwa kwengineko nchini humo.Süddeutsche Zeitung linahisi itakuwa shida kwa watu kumlaani shetani,hata kama makubaliano ya kisiasa yatafikiwa."

Bischof predigt von Frieden
Maaskofu wahubiri amani ipatikanePicha: DW/S. Schlindwein

Jamhuri ya Afrika kati pia imegonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii inayomalizika.Katka wakati ambapo Ufaransa iliyotuma zaidi ya wanajeshi 1600 kusaidiana na wanajeshi 6000 wa Afrika, inapigania uungaji mkono angalao wa fedha kutoka kwa washirika wake wa Umoja wa Ulaya kugharimia opereshini za kurejesha amani,katika jamhuri ya Afrika Kati kama lilivyoandika gazeti la Süddeutsche Zeitung" lile la mjini Berlin,Berliner Zeitung linajiuliza kama wanajeshi hao watatosha kuzuwia mapigano kati ya makundi ya waasi yaliyoangamiza maisha ya zaidi ya watu 450 pekee katika mji mkuu Bangui.Ufaransa inategemea uungaji mkono wa washirika wake,,lakini hadi sasa Ubeligiji peke ndiyo iliyoelezea utayarifu wa kutuma wanajeshi 130 linamaliza kuandika gazeti la Berliner Zeitung.

Mti Mkubwa Umeng'oka

Mazishi rasma ya Mandela pia hayakusahauliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.Baada ya kuwataja wageni wa hishima kutoka kila pembe ya dunia waliyohudhuria mazishi rasmi katika kijiji alikozaliwa cha Qunu,akiwemo mwanamfalme Charles wa Uingereza,mawaziri wakuu wa zamani wa Ufaransa Lionel Jospin na Alain Juppé sawa na mwanaharakati wa haki za binaadam wa Marekani Jessie Jackson ,Bild Zeitung limemnukuu chifu wa kabila la Madiba-Xhosa,aliyevalia ngozi ya chui akisema "mti mkubwa umeng'oka,sasa unarejea nyumbani ili kupumzika pamoja na babu wa mababu zake."Mandela amezikwa katika bustani ile ile alikokuwa akicheza zamani alipokuwa mdogo" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Bild" linalohisi hata kama"maiti yake haijateremshwa kaburini saa sita juu ya alama,mchana kama desturi na mila za kabila yake zinavyotaka,mababu wa mababu zake hawatomkasirikia.

Nelson Mandela Statue enthüllt
Sanamu la Mandela,akinyosha mikono-kuashiria kuishi pamoja kwa amani watu wa makabila yote nchini Afrika KusiniPicha: Reuters

Mwadishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Mohammed Khelef